HATIMAYE mawaziri saba kati ya nane wakiwemo wanaokabiliwa na tuhuma za
ubadhirifu,wanadiwa kukubali kuandika barua za kujiuzulu wenyewe kwa kile
kilichoelezwa kuwa ni kukinusuru Chama cha Mapinduzi (CCM).
Habari za
kuaminika kutoka mjini Dodoma zimesema kuwa mawaziri hao, walilazimishwa
kujiuzulu katika kikao cha dharura kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, kilichofanyika mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha
Bunge.
Taarifa zimewataja waliokubali kujiuzulu kuwa ni pamoja na Waziri wa
Viwanda na Biashara, Cyril Chami; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Uchukuzi
Omari Nundu; na Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda.
Wengine wanaodaiwa kujiuzulu
ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; Naibu Waziri wa Afya, Lucy
Nkya; na Naibu Waziri wa Viwanda, Lazaro Nyarandu.
Hata hivyo, Waziri wa
Fedha, Mustafa Mkulo, ambaye alishambuliwa vikali kwa kuitwa kinara wa ufujaji,
hakuwepo katika kikao hicho kwa madai kuwa yuko nje ya nchi, anasubiriwa aungane
na wenzake kuachia ngazi.
Kujiuzulu kwa mawaziri hao kumekuja baada ya kuzuka
kwa mjadala mzito ndani ya Bunge kwa siku mbili mfululizo kuhusiana na tuhuma za
ufujaji wa kutisha wa fedha za umma, kiasi cha kusababisha kuwepo kwa azimio la
kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wakati wa
majumuisho ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mashirika ya
Umma, mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alilitaka Bunge kuweka ushabiki na
itikadi za kisiasa pembeni na kuazimia kwa pamoja kupiga kura za kutokuwa na
imani na Pinda kutokana na uzembe wa mawaziri wake.
Kabla ya kujiuzulu huko
Spika wa Bunge, Anne Makinda, jana alizima hoja ya kumwajibisha Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda, akidai kuwa utaratibu mzima umekiukwa na hivyo hauwezi kufanyiwa
kazi katika kikao cha sasa cha Bunge.
Makinda alisema hayo alipokuwa akitoa
mwongozo uliyoombwa na Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (CCM) kuhusu suala
hilo na kudai kuwa wanaoendesha mchakato huo itabidi wasubiri hadi Bunge
lijalo.
Makinda ametoa hoja hiyo, wakati idadi kubwa ya wabunge wakiwa
wametia saini za kumwajibisha Waziri Mkuu kutokana na ubadhirifu mkubwa
unaowahusisha mawaziri watano wa serikali.
Mchakato wa utiaji saini
unaosimamiwa na Zitto Kabwe, ulikuwa ukiendelea kwa kasi na habari za kuaminika
zinasema kuwa idadi ya walio tayari kuweka saini zao inaweza kufika wabunge
200.
Akuzungumza jana mchana, Zitto alisema kuwa hadi muda huo alikuwa na
saini za wabunge 66, huku akidai kuwa wabunge wote wa CUF walikuwa wameandikiwa
barua na chama chao kusaini azimio hilo, jambo ambalo litafanya idadi ya wabunge
kufikia 80.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kusimamia
Mashirika ya Umma (POAC) alisema kuwa hadi jana majira ya saa 7 mchana, wabunge
wa vyama vyote walikuwa wameweka saini azimio hilo isipokuwa wa UDP.
Mawaziri
wanaotakiwa kuwajibika ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo; Waziri wa Viwanda na
Biashara, Cyril Chami na naibu wake, Lazaro Nyalandu; Waziri wa Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika; Waziri wa Nishati na Madini,
William Ngeleja; na Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu.
Zitto ambaye pia ni
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), alisema wabunge wa CUF 12 wameshasaini
azimio hilo na kwamba maagizo yametoka makao makuu ya chama hicho kutaka wabunge
wake kusaini kusudio hilo.
Alisema kuwa baadhi ya watu wanasema Waziri Mkuu
hana makosa na kwamba anaonewa na kueleza kuwa wanampenda sana, lakini
wanaiheshimu zaidi Tanzania.
Alisema kulingana na kanuni za Bunge, wabunge
wanaweza kumwajibisha Waziri Mkuu kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani
naye.
“Miongoni mwa majukumu ya Waziri Mkuu ni kusimamia shughuli za serikali
pamoja na utendaji wa baraza la mawaziri. Mawaziri wameonekana kusimamia wizara
zao ambazo zina wizi na ubadhirifu.
“Kuwepo kwa ubadhirifu ni kushindwa kwa
Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yake…tunajua hawezi kuwawajibisha mawaziri na
ndiyo moja ya mambo tunayotakiwa kuyarekebisha kwenye Katiba, lakini yeye tuko
naye hapa na sisi ndiyo tuliomthibitisha na tuna uwezo wa kuondoa uthibitisho
wake.
“Kwa hiyo katika hilo hatuna mbadala hatuna muafaka kama mawaziri
waliotajwa kuhusika na aina ya ubadhirifu kwenye wizara zao, idara zao,
mashirika hayo na halmashauri kama hawajachukua hatua tunaanzia na Waziri Mkuu.
Atakuwa Waziri Mkuu wa kwanza nchini kupigiwa kura au kutolewa hoja ya kutokuwa
na imani naye.
“Tumempa muda mpaka Jumatatu tutawasilisha rasmi hoja yetu kwa
Spika kwa mujibu wa mamlaka ya kanuni 133 inayotutaka kukusanya saini ya wabunge
asilimia 20 ya wabunge wote ambao kwa hesabu zetu ni wabunge 70 na tutapata
zaidi hao,” alisema.
Alisema kwamba wanatimiza matakwa hayo ya kikanuni na
kisha kuwasilisha kwa Spika, ili baadaye Bunge liweze kuonyesha meno
yake.
Alibainisha kuwa ili Waziri Mkuu aweze kutoka katika kitanzi hicho,
anapaswa kumshauri Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi mawaziri hao ama mawaziri
hao wajiondoe mapema.
“Lakini kama wanataka kumuweka kiongozi wao, kiraja wao
rehani, wanataka Waziri Mkuu aingie katika hoja ya kupigiwa kura ya kutokuwa na
imani naye ni jukumu lao, wachague wao wenyewe,” alisema.
Hata hivyo, Spika
kwa upande wake alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge ambazo zimetokana na
Katiba zinataka hoja kama hiyo iwasilishwe bungeni angalau siku 14 kabla ya siku
iliyokusudiwa, na sio wiki ijayo kama ilivyoelezwa juzi na Zitto Kabwe
bungeni.
“Sasa hii habari ya kusema waheshimiwa njooni njooni kusaini huo sio
utaratibu. Hiyo haikubaliki kwa sababu mimi sijapata hiyo hoja mpaka sasa. Bunge
hili tunaahirisha Aprili 23 maanake Jumatatu. Leo (jana), kesho (leo), Jumapili,
Jumatatu haikidhi siku 14 sana sana anaweza (Zitto) kukusanya nyaraka labda
kuwasilisha Bunge lijalo,” alisema Spika.
Aliendelea kusema kuwa kanuni na
utaratibu alioutangaza Zitto hauwezekani na kwamba zoezi la kukusanya saini za
wabunge ni batili. Aliwashauri wanaotaka hoja hiyo wavute subira hadi Bunge
lijalo, akidai kuwa kuitimiza ndani ya siku tatu zilizobaki ni kukosa
mashiko.
Hata hivyo alikiri kuwa wabunge wana madaraka na Waziri Mkuu
kulingana na Katiba kwa kuwa ndiyo wanaomwidhinisha baada ya uteuzi.
Alinukuu
ibara ya 53(a) (3) kwamba Waziri Mkuu anapitishwa na wabunge ambao
wanamthibitisha. “Msingi wa Zitto ni kwamba huyu ni mtu tuliyempitisha sisi
wenyewe. Kwa hiyo tuna mamlaka naye kwani ndiye tulimpitisha sisi,”
alisema.
“Waziri ndiye atakayekuwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni.
Serikali chini ya mamlaka ya Rais ndiyo itakayofanya maamuzi juu ya sera. Na
mawaziri chini ya uongozi wa Waziri Mkuu watawajibika kwa pamoja katika
utekelezaji wa shughuli za serikali. Hivi vifungu ndivyo vinatupa nguvu ya kuwa
na uwezo na Waziri MKuu.”
Wabunge wa CCM watishwa
Katika hatua
nyingine, imedaiwa kuwa wabunge wa Chama cha Mapinduzi, wameitwa na kutishwa
kuchukuliwa hatua ikiwa watasaini azimio hilo.
Mmoja wa wabunge wa CCM
aliyekiri kuitwa ni Deo Filikunjombe (Ludewa) ambaye alisema alilazimika kusaini
kabla ya kuitikia wito huo.
Filikunjombe, alikiri kuitwa na Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na kumtaka kutosaini
azimio hilo, lakini akamwambia alikwishasaini na alifanya hivyo kwa niaba ya
wananchi wa Ludewa ambao wamechukizwa na ubadhirifu mkubwa uliofanywa na
watendaji hao wa serikali.
Kuhusu wabunge wa CCM kutosaini azimo hilo,
Filikunjombe alisema kanuni haikusema wabunge wote, kwani inafahamika wengine
wanarudi nyuma alisema.
Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde alisema suala la
hoja ya kikanuni ina lengo la kuchelewesha mchakato wa kuwaondoa wanaolalamikiwa
na kuahidi kuwaondoa hata kama Bunge litawakingia kifua.
Alisema kama
mawaziri wanaolalamikiwa wataendelea kubakia katika nafasi zao ni bora wabunge
wa CCM wakaondoka na kuwaachia wao majukumu yote.
Alipoulizwa kama msimamo
wake hauwezi kuwakera viongozi wake na kuamua kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja
na kumuondoa katika chama, Lusinde alisema kuwa hilo halihofii kwa kuwa hana
hati miliki ya ubunge wa Mtera na zaidi ataendelea kubakia Mtanzania
anayepigania maslahi ya nchi yake.
Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole
Sendeka (CCM), alisema katika mapendekezo yaliyoafikiwa juzi hakuna azimio
katika kamati yoyote lililotaka waziri aondolewe na kusema kuwa alichokuwa
akikifanya Zitto ni usanii.
“Katika taarifa yake ile alipaswa asema Bunge
limependekeza mtu fulani awajibishwe, hivyo alitakiwa kuleta nyongeza katika
taarifa yake. Hakuna aliyeleta. Ile ni burudani tu,” alisema na kuongeza kuwa
hoja hiyo haina mashiko.
Alihoji kuwa iwapo Pinda alishindwa kumuondoa
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, atawezaje
kumuondoa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo.
Alisema kuwa ili hoja hiyo
ifanikiwe ni lazima Spika aridhike kwamba ilifuata taratibu na ina sifa hata
ikisainiwa na wabunge 200 kama haina sifa haiwezi kupita.
Zitto asema
wembe ni uleule
Akizungumzia vikwazo hivyo, Zitto alisema haviwatishi na
wanaendelea na mchakato huo, na kwamba watakabidhi hoja hiyo, Jumatatu baada ya
kukamilika.
Zitto alisema kama watashindwa kusaini fomu hizo watakuwa
wawakilishi wa ajabu kwa kuwa wao ndiyo waliokuwa wakipiga kelele juzi kutaka
waliosababisha ubadhirifu kuwajibika na kwamba kama watashindwa kuunga mkono
litakuwa ni jukumu la wananchi kupima uwakilishi wao.
Alisema ni jambo la
aibu kwa Bunge zima likimaliza kikao bila kuwawajibisha mawaziri waliohujumu
mali za taifa.
“Tukiondoka hapa bila kuwawajibisha watu, wananchi huko nje
watalidharau Bunge kwa hiyo tunalinda heshima ya Bunge na kulinda heshima ya
wabunge kwa kutaka kuona tunaimarisha uwajibikaji.
“Bila watu kuwajibika
madudu haya yatarudia na ndiyo maana tunataka uwajibikaji ufanyike,”
alisema.
Alisema kuwa anajua wabunge wa CCM wamechukizwa na wizi na
ubadhirifu na wamesema kwa nguvu sana juzi na jana na hakuna asiyeona
hilo.
“Mimi sijafanya kama mbunge wa CHADEMA, bali kama mbunge wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,” alisema.
Hivyo, alitaka wabunge wasigawanywe katika
misingi ya vyama na kwamba anayefanya hivyo hana maslahi na nchi na kuhoji iwapo
CCM ina hoja nzuri ambayo inaisimamia.
“Tusiruhusu maneno ya propaganda ya
kutugawa na ninyi ndiyo mashahidi mnalalamika na juzi mlimuuliza CAG,”
alisema.
Alisema katika masuala ya kitaifa wabunge wanapaswa kuweka pembeni
itikadi zao na kuwatumikia wananchi wanaowawakilisha na kusisitiza kuwa
wanachokitaka ni mabadiliko na si mapinduzi.
Wasomi waunga mkono
BAADHI ya wananchi wa kada na rika mbalimbali nchini wamesema mwenendo
wa Bunge la sasa ni ishara za kuamka kwa mhimili huo inayotokana na changamoto
za wabunge wa upinzani.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti
wananchi hao walisema msimamo wa wenyeviti ambao ni wabunge kutoka upinzani
wanaoongoza kamati tatu za Bunge umesaidia kuonyesha uozo wa watendaji
serikalini hususan mawaziri wasiotimiza vema wajibu wao.
Wenyeviti wa kamati
hizo ni Zitto Kabwe (CHADEMA) Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Agustine Mrema
(TLP) Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na John Cheyo (UDP) Hesabu za Serikali
(PAC).
Kwa mujibu wa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM) Profesa Issa Shivji, Katiba ya sasa inaruhusu kupiga kura ya kutokua na
imani japo ni mapema kufanya hivyo huku akisisitiza kwamba jambo la msingi ni
kusubiri uamuzi wa wabunge hao.
Kwa upande wake mhadhiri mwandamizi mstaafu
wa UDSM Dk. Azaveli Lwaitama alisema wabunge hao wanagombana na mfumo wa kumweka
Waziri Mkuu madarakani hali inayoonyesha wazi kwamba hawana imani na
Rais.
“Ninavyoona hapo kinachowachukiza wabunge hao ni uwaziri mkuu na mfumo
wa kumpata waziri mkuu kwa sababu wanalalamikia utendaji wa baadhi ya mawaziri
lakini waziri mkuu hana uwezo wa kuwafukuza mawaziri hao.
“…Hebu tukumbuke
wakati wa Jairo, Waziri Mkuu alitamani kumfukuza akashindwa lakini Katibu Mkuu
Kiongozi alikuwa na uwezo; ndiyo maana alimpa likizo yenye malipo.
“Tatizo ni
mfumo wa utawala walioteuliwa wanawajibika kwa aliyewateua lakini waliochaguliwa
wanatumwa na wananchi ndiyo,” alisema Dk. Lwaitama na kuongeza kwamba lazima
mambo hayo yaingie kwenye Katiba mpya.
Mjasiriamali Celina Ezekiel wa Isimani
Iringa alisema Bunge limeanza kutambua mamlaka yake ya kuisimamia serikali hasa
kwa wabunge wa CCM.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
Profesa Sifuni Mchome alisema wabunge wana uhuru wa kufanya hivyo kwa maslahi ya
nchi na kuongeza kwamba ni jambo la kawaida.
Mkazi wa Igunga mkoani Tabora
Nicholous Ngassa alisema haafikiani na suala la kumwondoa Waziri Mkuu madarakani
badala yake mawaziri walioguswa na ripoti ya CAG wanapaswa kuwajibika na
kupelekwa mahakamani.
“Hali ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu na serikali
yake kunashusha thamani Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jamii na kujiondoa
kwenye ramani ya siasa nchini na Afrika,” alisema Ngassa.
Naye Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala
Dk. Benson Bana alisema wabunge wametimiza wajibu wao na kuwataka mawaziri
wanaotuhumiwa kuchukua hatua.
Akitolea mfano wa ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dk. Bana ambaye ni mwenyekiti mwenza ya Taasisi
ya Utafiti wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet) alisema umaskini unaongezeka
kwa sababu ya wachache walio kwenye ngazi za uamuzi.
“Ripoti ya CAG
inaonyesha kushuka kwa kiwango cha uwajibikaji serikalini hususan eneo la
matumizi ya fedha za walipa kodi… kwa nini wanaotajwa kwenye ripoti hiyo
wasijiuzulu?” alisema Dk. Bana na kutaka wabunge washikamane katika
hilo.
Naye Mahadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislam cha Morogoro (MUM) Profesa
Juma Mikidadi alisema wabunge wako sahihi katika uamuzi wa kutaka kumjadili
Waziri Mkuu kwa sababu ya mawaziri wa chini yake kushindwa kuwajibika.
Sheikh
Jabir Ramadhan aliwashauri wabunge hao kutoa muda wa mwisho kwa mawaziri hao ili
kabla hawajaondoka waanze kuchunguzwa huku akiwashauri wasifanye hivyo kwa
chuki.
Mkazi wa Tabata Jamila Athuman alisema serikali ya awamu ya nne
imeongeza pengo kati ya matajiri wachache na maskini wengi hali inayowafanya
wananchi kuichukia serikali yao.
“Walioteuliwa hawana uchungu wa nchi ndio
maana wanafanya ufisadi huku Rais akiwakingia kifua kwa kuendelea kuwaacha
madarakani na wakati mwingine anawahamisha vituo vya kazi,” alisema
Jamila.
Joseph Mhimbilila alisema wananchi wamechoka kuvumilia wizi wa mali
ya umma unaofanywa na watawala wao sasa wananchi wamechoka hivyo wabunge hao
wakishindwa kuwasaidia watachukua hatua kali zaidi.
“Hili linaweza kuwa
fundisho kwa viongozi wenye ndoto za kuliibia taifa hili,” alisema.
Kwa
Upande wake Mwanasheria Alex Mgongolwa alisema sheria inampa mamlaka Waziri Mkuu
kusimamia shughuli zote za serikali na kuhakikisha kunakuwepo na
uwajibikaji.
Alisema katika Katiba ibara ya 53 (A 1-6) inasema hoja ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu inaweza kuwasilishwa bungeni kukiwa na sababu
za msingi juu ya majukumu ya Waziri Mkuu na kushindwa kuyatekeleza.
“Nafuu
inayoweza kupatikana ni kama anayetolewa hoja hajapitisha miezi sita tokea
kuteuliwa kwake au kabla ya miezi tisa kupita tokea hoja kama hiyo kuwasilishwa
bungeni, na hapa ni lazima Spika ajiridhishe kuwa masharti yamezingatiwa,”
alisema Mgongolwa.
source; tanzania daima