Augustine
Mgendi
BUHEMBA
WANANCHI vijiji Vitatu
wanaozungukwa na Mgodi wa Buhemba wilaya ya Butiama mkoani Mara
wamesema kuwa wanakusudia kuishitaki Serikali ya Tanzania katika Taasisi za
Umoja wa Mataifa zinazohusika na haki za binadamu ikiwa ni
shinikizo la kulipwa fidia ya shilingi Bilioni 30.
Mbali na kusudio hilo
la kuelekea umoja wa Mataifa lakini pia wananchi hao wamesema kuwa wanakusudia
kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete kumueleza madhara
yaliyosababishwa na Mgodi huo ambao ulidaiwa kumilikiwa na Serikali kupitia
Kampuni ya Meremeta.
Wananchi hao kutoka vijiji vya Tarani,Biatika na
Magunga huku wakiomba Wabunge kuungana na kutoipitisha Bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini had hapo Serikali itakapo wafidia.
Akiongea na waandishi habari katika eneo hilo la
Buhemba,Diwani wa kata ya Buhemba Boniphace Masero amesema kuwa Mgodi huo
umeachia athari kubwa kutokana na machimbo yaliyoachwa kuleta athari kubwa huku
Ardhi yao ikiwa haina rutuba kutokana na Kemikali zilizomwagwa katika eneo
hilo
Amesema athari zingine
zilizoletwa na Mgodi huo ni pamoja na Shule iliyokuwa katika eneo hilo
kubomolewa lakini walishindwa kuijenga kama walivyokuwa wameahidi wahuska hao wa
mgodi huku miundombinu ya barabara nao ikiwa haifai
kutumika.
“Huu Mgodi umetuachia
madhara makubwa sana maana Mashimo hayakufukiwa,Milima inaleta uchafuzi wa
Mazingira,shule iliyokuwa imejengwa hapa ilibomolewa,Nyumba zikabomoka kutokana
na Baruti za mgodi,katika hili sisi tunakusudia kumuona Rais ili tumueleze haya
Manyanyaso tunayoyapata” alisema diwani huyo
Diwani Masero ameongeza
kuwa athari nyingine ni pamoja na baadhi nyumba za wakazi wa eneo hilo kubomoka
kutokana na baruti zilizokuwa zikipigwa katika Mgodi huo lakini mpaka sasa
hawajalipwa fidia na hivyo wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutoipitisha Bajeti ya wizara ya Nishati na Madini mpaka walipwe fidia
yao
Aidha Pasta wa Kanisa
la Anglikana Samweli Nyakarungu alisema kuwa mgodi huo wa Buhemba ulikuwa ni
Mgodi wa kitapeli ambapo wahusika hao wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa
kufanya shughuli za Maendeleo katika Jamii.
Pasta Nyakarungu
alisema kuwa mbali na wawekezaji hao wa Kitapeli kuiba mali ya Watanzania lakini
pia wamesababisha madhara makubwa kwa jamii ya Buhemba kwa kushindwa kujenga
miundombinu ya barabara,kujenga shule kama inavyotakiwa.
Kutoka na adha hiyo
Pasta huyo alisema kuwa Serikali imeshindwa kuwajali wananchi wake na hivyo
wanawaomba Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoipitisha Wizara ya
nishati na Madini mpaka hapo wananchi wa eneo hilo watakapopata fidia
yao.
“Hawa
wawekezaji mimi naona hawakuja hapa kwa lengo la kumsaidia mtu wa Buhemba huu
Mgodi naona ulikuwa wa Kitapeli kabisa,wamechuma raslimali za Taifa na kushindwa
kumsaidia mtu anayezungukwa na mgodi na hata kurekebisha miundombinu huska na
hii inaonyesha jinsi Serikali isivyojali wananchi wake” alisema Pasta
Nyakarungu
Naye Mwalimu mstaafu
Sita Nyamhanga na bi Hadja Yasini walisema kuwa mgodi huo umewaachia matatizo
makubwa ikilinganishwa walivyokuwa wameahidiwa wakati wanaanza uchimbaji katika
mgodi huo.
“Tunavyojua ni kwamba wawekezaji wanapowekeza eneo lolote lazima watu
wanaozungukwa na Mgodi ule wanufaike lakini hapa Buhemba sisi wananchi ndiyo
tumepat tabu kabisa kwani mpaka sasa hatuna shule,barabara inayopitika muda
wote,eneo letu limebaki Jangwa huku wakina mama wanapata tabu kutafuta maji
kutokana na vyanzo vingi vya maji kuchafuliwa na mgodi” alisema Mwalimu mstaafu
huyo.
Kwa upande wake Bi
Hadja Yasini alisema kuwa wanapata tabu hata kutafuta kuni kutokana na eneo
kubwa la Buhemba kubaki Jangwa tofauti na ilivyokuwa hapo
awali.
Kulingana na adha hiyo
Bi Hadja alisema kuwa ni vyema Waziri mwenye dhama huska akawasaidia watu wa
Buhemba ili waweze kupata fidia zao kutokana na madhara waliyoyapata kutokana na
mgodi huo.
Mgodi wa Buhemba ambao
ulianza kuchimbwa mwaka 2002 ni moja ya mgodi ambao ulikuwa ni mkubwa hapa
nchini ukielezwa kumilikiwa na Serikali na kufungwa mwaka 2006 huku ukiacha eneo
hilo la Buhemba kupoteza rutuba yake
No comments:
Post a Comment