Dkt.Felician Kilahama Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na Nyuki nchini.
Na Theonestina Juma
KUWEPO kwa nyoka mwenye umri wa miaka 209 sasa katika msitu
wa akiba ya serikali ya Minziro wilayani Missenyi, serikali imeazimia kuanza
kumsaka kwa udi na uvumba .
Aidha kutokana na ukongwe wake duniani kote huenda akawa
kivutio muhimu katika sekta ya utalii na hivyo kuifanya serikali kuanza kupiga
mahebu yake ili kuweza kumnasa kirahisi.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa Misitu na
nyuki nchini, Dkt. Felician Kilahama wakati akizungumza na waandishi wa
habari mjini Bukoba.
Dkt. Kilahama alisema nyoka huyo mwenye futi 47 anapatikana baada ya kuona viashiria ya mapito
yake yakiwa yameburuzwa buruzwa katika
pori hilo, ambapo imekuwa vigumu sana kuonekana hadharani kutokana na kuishi
kwenye mapango.
“Huyu nyoka lazima tumfanyie mahesabu, ya kumpata kirahisi,
miaka 209…,sio mchezo…. ameweza kutambulika miaka baada ya kupima urefu wa
mapito yake, kuna chatu na nyoka wenye mapembe pia…. “alisema Dkt. Kilahama.
Alisema licha ya kumfuata fuata nyoka ni jambo la hatari na
inahatarisha maisha ya mtafiti hivyo lazima ifanyike uharaka wa kupandisha
hadhi msitu huo wa akiba ili iwe hifadhi ya taifa ambapo utaweza kuboresha hata
usimamizi wake, ambapo hata hivyo katika Kamati ya ushauri wa Mkoa Kagera (RCC)
ulipitisha msitu huo upandishwe hadhi.
Nyoka huyo ambaye ni aina ya Giant Forest Cobra kichwa chake
kina rangi nyekundu na sehemu ya kiwili wili ikiwa ni rangi ya kijani alianza
kufanyiwa utafiti tangu mwaka 2000 baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa
wenyeji wa maeneo hayo juu ya kuwepo kwa aina ya nyoka huyo katika msitu huo.
Kutokana na hali hiyo, ililazimu uongozi wa Halmashauri ya
Missenyi, kupitia Maofisa wa Misitu mwaka 2010 kumtengeshea sindano katika
mapito yake kwa lengo la kuchukua damu yake,
kwa ajili ya kupima vina saba yake iliyobainika kuwa na miaka zaidi ya 207 kwa mwaka
huo.
Dkt. Kilahama alisema nyoka huyo atakuwa ni kivutio muhimu
katika Mkoa wa Kagera iwapo atatafutwa na kupatikana licha ya kuwa wanakabiliwa na tatizo la
ukumbwa wa msitu huo ambao unajumla ya hekta 25,000 kwani nyoka huyo amekuwa akihama hama katika
harakati zake za mawindo.
Afisa Misitu wa Wilaya ya Missenyi, Bw. Wilbard Bayona
alisema nyoka huyo anayo uwezo wa kuishi siku 68 bila kula chochote zaidi ya
maji baada ya kumeza mnyama yeyote anayefanikiwa kumkamata.
No comments:
Post a Comment