Na Theonestina Juma, Bukoba
BAADHI ya wakazi wa mtaa wa Kyaya kata ya Kahororo katika
Manispaa ya Bukoba wanalazimika kulala porini na kushindwa kushiriki shughuli za maendeleo
kutokana na kuogopa askari polisi wanaowavamia katika majumba yao saa sita za
usiku wakiwa wamelala.
Hayo yamebainika jana wakati wananchi wa mtaa huo wapatao
wanane wakizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa ambapo walisema kuwa
Juni 30, mwaka huu saa 5 usiku askari polisi wapatao 12, wakiwa na baadhi ya
walinzi wa shule ya sekondari ya Nyashenye wakiwa na silaha huku wamevaa kiraia
waliwavamia nyumba tano na kuwakamata baadhi ya wananchi wenzao.
Wananchi hao walisema chanzo cha kuvamiwa na polisi hao ni
kutokana na mgogoro wa ardhi wa tangu mwaka 1987 uliopo kati yao na uongozi wa Shule ya sekondari ya Nyashenye
inayomilikiwa na Kituo cha Bukoba cha Waislam mjini hapa (Bukoba Islamic
Center) ambao wanataka wananchi hao wahame kwa madai kuwa wako katika ardhi
yao.
Wananchi hao walisema kwa kipindi kirefu sasa hawaishi kwa amani
katika mtaani hapo kutokana na mgogoro huo kuingiliwa na Polisi kwa shinikizo
na kiongozi mmoja wa kisiasa mjini hapa ambaye anawadhifa kubwa serikali
anayedaiwa kuulinda uongozi wa shule hiyo kwa maslahi binafsi ya familia yake.
Walisema kwa siku nne sasa amani imetoweka kabisa katika
eneo lao, ambapo wanakaa chonjo wakati wote kutokana na kutojua ni muda gani
polisi watafika katika eneo hilo kwasomba kwani inavyoonekana kwa sasa polisi
wanaonia ya kutaka kusomba mtaa mzima kuishia gerezani.
Waandishi wa habari waliolazimika kwenda katika mtaa huo
ambao uko umbali wa takribani kilomita
tatu kutoka katika kituo kikuu cha polisi mjini hapa, ulishuhudia woga
wa wananchi ambapo baadhi ya wananchi walipoiona teksi iliowapeleka waandishi
hao katika eneo hilo, kila mmoja alianza kutimua mbio, ambapo naadhi yao aliweza
kusitisha baada ya kuona kamera za
waandishi hao.
Aidha waandishi hao waliweza kushuhudia baadhi ya milango na
madirisha ya nyumba za wananchi hao zilizobomolewa na polisi hao usiku wa manane, ambapo wamiliki
wa nyumba hizo walikamatwa na polisi hao na hivyo kulazimu wanandugu kuwalindia
nyumba zao nyakati za usiku.
Baadhi ya watu waliovamiwa na polisi usiku huo wa manane na
kuharibiwa nyumba zao ni pamoja na Bw.Robert John (65), Richard Ifunya (60),
Charles Robert (27) na mwanamke pekee Bi. Joyce Anatory (22) na mwanae Debora Jairos mwenye umri wa mwaka mmoja na
nusu ambaye naye ameswekwa rumande pamoja na mama yake licha ya kusumbuliwa na ugonjwa wa malaria.
Nyumba ya Bw. John ilivunjwa dirisha, kwa Bw. Ifunya
waling’oa kabisa mlango wake huku kwa Bw. Robert mlango wa nyumba sehemu ya juu
ikiwa ilipigwa na kitu kizito na kutikisika.
Makazi mmoja wa mtaa huo, Bi. Mamerita Ntinabo (53) alisema
taasisi hiyo ya shule ilikuja kwa lengo
nzuri mwaka 1986 la kuomba ardhi kujenga shule ambapo walipewa eneo lakini cha
kushangaza ni kuwa walikuwa wakijiongeza eneo la wananchi huku wakiwapatia
vitisho ambapo wamefikia hatua ya kutumia wanafunzi wa shule hiyo kung’oa mazao
yao na kwamba hakuna hata mwanafunzi
yeyote kutoka mtaa huo anayesoma katika shule hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa huo, Bw. Gilbert Makwabe akizungumza na
waandishi wa habari juu ya tukio hilo alisema wakati wananchi wake wakivamiwa
usiku wa manane na kusombwa na polisi
alikuwa safarini Jijini Dar Es
Salaam.
Hata hivyo akizungumzia sababu za kukamatwa kwa wananchi hao
ni kutokana na mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na uongozi wa shule hiyo ya
Nyashenye, ambapo chanzo cha mgogoro huo ulianza mwaka 1987 wakati Rais awamu
ya pili Ally Hasan Mwinyi alipofika eneo hilo kuweka jiwe la msingi ambapo
katika taarifa ya uongozi wa shule hiyo kwa rais huyo ilieleza kuwa wananchi
tayari walishafidiwa zaidi ya sh. milioni 78.3 jambo liliowafanya wanachi
kushtuka ni kujihoji ni nani aliyechukua hela hiyo miongoni mwao.
“Unajua walipoanza kujenga wananchi hawakujua wanataka ardhi
kiasi gani, lakini kutokana na risala waliomsomea Rais Mwinyi mwaka 1987 ndiyo
uliosababisha mvurugano kuanza, kwani wananchi walianza kuona wakienda kulima
katika hilo mbuga uongozi wa shule ulianza kuwafukuza… hapa ndipo wananchi
walianza kusema kumbe hawa wanataka eneo hili lote”alisema
Bw. Makwabe alisema hadi sasa hekta 81 ndizo zinazogombaniwa
kwani ni kama kuchukua kijiji kizima, ambapo katika uongozi wa serikali za
mitaa hakuna kumbukumbu inayoonesha shule hiyo kumilikishwa eneo hilo.
Kwa upande wa Makamu Mkuu wa shule hiyo, Bw. Masoud Hussein
akizungumza na waandishi wa habari alisema wananchi hao walivunja vigingi
vipatazo 10 za shule hiyo ambapo walialazimika kutoa taarifa kituo cha polisi
ambapo alisema kuwa hakuna mlinzi wa shule hiyo aliyeambatana na polisi
kuwabomolea wananchi hao nyumba zao wala katika ukamataji wao.
Alisema wananchi hao wanao kikundi cha watu fulani ambao
wanawasukuma ili kuwafanyia fujo ambapo eneo hilo wanalimiki kihalali.
Hata hivyo kwa upande Kamanda wa polisi Mkoa Kagera, Phillip
Kalangi akizungumza na waandishi wa habari alidai kutokuwa na taarifa zozote
juu ya askari wake kuvamiwa wananchi usiku wa manane na kuwasweka rumande hali
iliowalazimu waandishi wa habari kuwa mgbogo kwa kauli yake kwani kwa wakati
huo kuna baadhi ya wananchi hao walipiga kambi katika eneo la kituo hicho
kuanzia asubuhi hadi jioni wakisubiri wenzao wafikishwe mahakamani ili waweze
kuwawekea dhamana ambapo jeshi hilo
liligoma wananchi hao kupewa dhamana.
Hata hivyo baada ya waandishi hao kumbana zaidi Kamanda
huyo, alifanya maarifa yake ambapo katika maelezo yake yasiokuwa na uthibitisho
alidai kuwa wananchi waliokamatwa ni wale walioruka mdhamana mwezi machi mwaka
huu, ambapo jeshi hilo walikuwa wakiwatafuta wananchi 15 walitakiwa kurudi kuripoti
polisi hawakuweza kufanya hivyo.
Kamanda Kalangi alisema katika sako wao si lazima kuwatumia
viongozi wa serikali za mitaa au kutokana na wao kwa asilimia kubwa vikwazo kwa polisi.
Pia alisema wananchi hao wanatuhumiwa kuvunja uzio wa shule
na kuingia eneo la shule bila kibali maalum, ambapo kwa uchunguzi waandishi
katika eneo hilo la shule haukuweza kuona uzio wa shule uliovunjwa na wananchi
hao hata kuvunjwa kwa milango na madirisha ya wananchi hao utafanyiwa uchunguzi
na jeshi hilo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment