Monday, September 16, 2013

Walimu Wakuu wawili wa shule za sekondari mkoani Kagera wafa katika ajali Biharamulo, walikuwa wakienda kwenye semina elekezi ya kuboresha elimu mkoani Kagera



Na Theonestina  Juma, Bukoba

WALIMU Wakuu wawili wa shule za sekondari  katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera,wamefariki dunia papo hapo huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani wakati wakienda katika semina elekezi ya kuboresha sekta ya elimu mkoani hapa inayofanyika Wilayani Ngara.

Kwa mujibu wa habari kutoka eneo la tukio, ajali hiyo imetokea Septemba 15, mwaka huu majira ya jana jioni Wilayani Biharamulo wakati wakiwa safarini kulekea wilayani Ngara baada ya kusaidiwa usafiri na Afisa vifaa na takwimu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera Bw. Johanes Katanga ambaye alikuwa dereva wa gari hilo, naye pia amejeruhiwa.

Chanzo cha ajali hiyo imeelezwa kuwa dereva wa gari hilo aina  Noah  ambalo namba yake ya usajili halijajulikana alikuwa akijaribu kumkwepa mwendesha baiskeli ambapo gari hilo lilipasuka matairi yote ya mbele na kupinduka.

Wakuu hao wa Shule za sekondari waliofariki ni pamoja na Bi. Agness Philipo wa shule ya sekondari ya Bunjunangoma na  Bw.Makoye Bloho wa shule ya sekondari ya Tunamkumbuka shule hizo zote ziko katika halmashauri ya  wilaya ya Bukoba.

Kwa mujibu wa Katibu wa Wakuu wa shule za sekondari Mkoani Kagera, Bw. Emmanuel Muganyizi, Bi.Philipo alifariki  dunia papo hapo baada ya kupata jeraha kubwa sehemu ya kichwani.

Aidha Bw.Bloho amefariki dunia leo njia wakiwa wamefika wilayani Sengerema wakati wakikimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

Alisema Bw.Brongo alifia njia wakati wakisafishwa pamoja na mwalimu mwenzake Bw. Themistocles Rwabangira  wakati wakipelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando  Jijini Mwanza baada ya wao kuonekana kuumia zaidi.

Hata hivyo, mwalimu Rwabangira  amefikishwa hospitalini hapo ambapo vipimo vimebaini kuwa amevunjika mbavu na mikono na mwili wa Bw. Bloho umehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando..

Aliwaja walimu waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na Bw. Shafii wa shule ya sekondari ya Ruhunga na Bw.Philbert Ferdinand wa Karagabaine.

Wengine ni pamoja na  Bi.Pelagia Thadeo, Bw. Malimbo wa shule ya sekondari ya Kalema na Bw. Katanga Afisa vifaa na Takwimu Mkoa Kagera ambaye alikuwa dereva wa gari hilo na mumiliki wake ambaye aliwasaidia usafiri walimu hao, wote wamelazwa katika hospitali teule ya Biharamulo.

Alisema Bi.Philipo anatarajiwa kuzikwa kesho Kemondo Bukoba vijijini na Bw.Bloho atazikwa nyumbani kwake Wilayani Magu jijini Mwanza.

Alisema kutokana na majonzi hayo kikao kilichotakiwa kianze leo kimeahirishwa hadi kesho.

Semina hiyo inawashirikisha walimu Wakuu wa shule za sekondari za umma kutoka wilaya zote za mkoa Kagera.


No comments:

Post a Comment