Sunday, September 22, 2013

Uzao wa shule ya sekondari WeruWeru wanogesha sherehe ya kutimiza miaka 50, wamo akina Dkt Asha Migiro na Dkt.Mery Nagu

IMG_0125Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizindua Bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru ya Moshi  Vijijini ikiwa na sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya shule hiyo Septemba 21, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) IMG_0143Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akipanda  mti kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru ya Moshi Vijijini  akiwa katika maadhimisho ya miaka 50 ya shule hiyo Septemba  21, 2013.  Wapili kushoto ni mkewe Tunu na Watatu kushoto ni Waziri wa  Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Wapili kulia ni Naibu Waziri  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) IMG_0183Baadhi ya Wanawake waliosoma katika  Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru ya  Moshi Vijijini  wakiimba wimbo wa Shule hiyo katika maadhimisho ya miaka 50  ya shule hiyo   Septemba 21, 2013. (Picha na Ofisi ya waziri
………………..

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania kuiga mfano wa shule ya Sekondari ya Weruweru ambao wahitimu wake wa zamani (Alumnae) wameamua kuchangisha fedha na kukarabati shule yao ya zamani.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Septemba 21, 2013) wakati akizungumza na mamia ya wanajumuiya waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae), wanafunzi waliopo pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema: “Watanzania wengi tuna nafasi za kuchangia shule zilizotusomesha. Tuige mfano wa wenzetu wa Weruweru, tukutane na kusaidia shule tulizosoma,” alisema.
Alisema yeye alisoma sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1965 na 1967 lakini kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwakutanisha wahitimu wa shule hiyo ambazo hazijawahi kufanikiwa. “Ninawataka mtembee kifua mbele kwa sababu shule yenu imeza yunda zuri sana,” alisema huku akiwasifia wana Weruweru waliohitimu zamani kwa kuamua kuja na wazo hilo jema la kukarabati shule yao ya zamani.
Mapema, akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Weruweru, Bibi Rosalia Frimini alisema shule hiyo iliyoanzishwa Oktoba 22, 1963 hivi sasa ina wanafunzi 570 wa kidato cha tano na sita tu wanaosoma michepuo ya PCB, EGM,ECA, HGE, HGK na HKL.
Alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa maabara, madarasa, mabweni na mifumo ya umeme. Alisema shule hiyo ina upungufu wa watumishi wakiwemo manesi, wapishi, mkutubi na walinzi.
“Shule pia inakabiliwa na tatizo la usafiri.  Landrover 110 iliyopo shuleni ni ya tangu miaka ya 80 na matengenezo yamekuwa makubwa, tunaomba utusaidie kutatua tatizo la usafiri… tunapata shida hasa ikitokea watoto wanaumwa na wanatakiwa kupelekwa hospitali ya mkoa,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Maria Kamm ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka 1970 hadi 1992, aliiomba Serikali irudishe mfumo wa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa shule kongwe ambao ulifutwa na Serikali. Alisema katika kujenga maadili kwa watoto, inabidi waanze tangu wanapoingia sekondari.
“Hawa wa kidato cha tano na cha sita ni wa kupita tu.. umri wa kuumba binti ni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Tunahitaji kuumba mabinti wa Taifa hili kama ambavyo tulikuwa tukifanya huko nyuma,” alisema.
Alisema Sera ya Taifa ya Elimu ya Kujitegemea ilikuwa ndiyo siri kubwa ya kuwaumba wasichana waliopitia shuleni hapo na kwamba ilileta usawa na kuondoa ubaguzi. “Sera hii ilifanya watoto wote wawe sawa, iliondoa ubaguzi shuleni kwa sababu wanafunzi wote walijifunza kazi na kujiamini. Na yote hii ni katika kujenga nidhamu kwa watoto wetu,” alisema.
“Elimu ya Kujitegemea siyo siasa kama wengi wanavyodhani, ni jadi ya mwafrika, ni jadi ya mwanamke. Kujitegemea ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa lolote ulimwenguni, tunaomba Serikali irudishe elimu ya kujitegemea shuleni ili tuwasaidie watoto wetu.”
Naye Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro ambaye ni mhitimu wa shule hiyo alisema Jubilei ya miaka 50 ya Weruweru ni sehemu ya kusherehekea ndoto iliyotimia na ndoto iliyokuwa kweli kwa wanafunzi wengi waliosoma kwenye shule hiyo.
“Shule hii ni ya pekee kwa sababu ilitoa fursa kwa mtoto wa kike pale ambapo hapakuwa na fursa… ilikuwa ni mchanganyiko wa watoto wa viongozi, wafanyakazi na wakulima”.
Akimnukuu Rais wa zamani wa China, Mao tse Tung, aliyesema wananwake wanashikilia nusu ya anga, Dk. Migiro alisema kutokanana usemi huo haiwezekani watu wanaoshikilia nusu ya anga wakaendelea kubaki nyuma.
Alisema shule hiyo imetoa wataalamu mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia, wanasiasa, viongozi mbalimbali wa mashirika, taasisi na serikali na pia imetoa rubani wa kwanza mwanamke hapa nchini.
Baadhi wa wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ni Dk. Asha-Rose Migiro, Dk. Mary Nagu, Balozi Mwanaidi Maajar, Bi. Anna Kilango Malecela, Dk. Mwele Malecela, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Hajat Amina Mrisho na wengine wengi ambao wameshika nafasi mbalimbali za uongozi katika mashirika, taasisi na Serikalini.

No comments:

Post a Comment