Sunday, September 22, 2013

Operesheni kimbunga awamu ya kwanza yakamilika, sasa ni nyumba kwa nyumba

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
http://www.fullshangweblog.com/wp-content/uploads/2013/09/Kamanda-Sirro-akizungumzia-vurugu-za-wamachinga-Mwanza.jpg

AARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Operesheni Kimbunga iliyoanza Septemba 6,2013 imemaliza utekelezaji wa Awamu yake ya Kwanza Septemba 20,2013 kwa kutimiza malengo yake kwa mafanikio makubwa.
Hadi kufikia mwisho wa Awamu ya Kwanza wa Operesheni hii, Timu ya Operesheni imefanikiwa kukamata wahalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na washirika wao na kuhakiki uraia wa watuhumiwa wa Uhamiaji haramu kwa kutumia maofisa wa Idara ya Uhamiaji kwa kuzingatia Sheria za Uhamiaji. Aidha, suala la Haki za Binaadam limezingatiwa katika Operesheni hii.
Jumla ya Wahamiaji haramu 12,704 wamekamatwa, kati yao Wanyarwanda 3,448 Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589 Wasomali 44, Yemen 1 na India 1.
Jumla ya Wahamiaji Haramu 194 walirudishwa na kupokelewa nchini baada ya kukataliwa na nchi zao. Watu hao wanasubiri  hatua za kisheria kuchukuliwa kwa kuwa hawana sifa ya kuwa Raia wa Tanzania na pia wamekosa sifa ya kuwa raia wa nchi jirani ambapo Serikali iliwapeleka baada ya vigezo vya kuthibitisha kuwa ni raia wa nchi hizo kukamilika.
Wakati Operesheni kimbunga inafanyika katika Awamu yake ya Kwanza kuanzia Septemba 6, 2013, jumla ya wahamiaji haramu 2,129 walikubali kuondoka nchini kwa hiari yao na Wahamiaji Haramu  8,696 waliondoshwa nchini kwa amri ya Mahakama baada ya kupewa hati ya kufukuzwa nchini. Watuhumiwa wa Uhamiaji Haramu 1,852 waliachiwa huru baada ya Serikali kuthibitisha uraia wao wakati wengine 2,286 wanaendelea na mahojiano ili kuthibitisha uraia wao. 
Operesheni Kimbunga pamoja na kushughulikia wahamiaji Haramu ilifanikiwa kukamata jumla ya Watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha na Majangili wa Tanzania 23. Mabomu 10 ya kutupwa kwa mkono, bunduki/silaha 61 zikiwemo bunduki aina ya SMG 5, Shot Gun 8, Mark IV 1, Riffle 1, Pistol 1, Pisto za kienyeji 3 na Magobole 42 pamoja na mitambo Miwili 2 ya kutengeneza silaha aina ya Magobole.
Risasi 665 zilikamatwa zikiwemo za bunduki aina ya SMG na SAR risasi 561, Shot Gun risasi 22, Gobole risasi 82 na Fataki 8, Suruali Sare za Jeshi na Kibuyu cha Maji vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
Jumla ya Ng’ombe 8,226 walikamatwa wakiwa wanachungwa katika maeneo ya Tanzania hususan katika hifadhi za misitu. Pia kiasi cha Tsh. 32,510,000/= zimepatikana ikiwa ni tozo za faini ya ng’ombe walioachwa kwenye hifadhi ya Taifa.
Ngozi za wanyama aina ya Duma(1), Swala (2), Nyati (1) na vipande 10 vya Nyama vinavyodhaniwa kuwa Nyara za Serikal, Vipande viwili vya meno ya Tembo pamoja na Mbao 2,105, Magogo 86, Mkaa Magunia 467,Gongo Lita 375, Mtambo wa Gongo mmoja (1), Bangi Kilo 77 na Makokoro yanayotumika kuvuna Samaki kinyume cha sheria  vilikamatwa katika kipindi cha Wiki Mbili za Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga.
Takwimu zinaonyesa kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa kukamata wahamiaji haramu 7,001 ukifuatiwa na Mkoa wa Kigoma ambaPo wahamiaji haramu 5,005 walikamatwa wakati mkoa wa Geita wamekatwa Wahamiaji Haramu 698.
Changamoto
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana kumekuwepo na changamoto zilizojitokeza ikiwa ni pamoja na hali ya maisha mchanganyiko ya Watanzania asilimia 60% na Wahamiaji asilimia 40% katika mikoa ya mpakani hii ni kwa mujibu wa tafiti mbali mbali za masuala ya kiuhamiaji zilizowahi kufanyika katika mikoa hiyo.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi wenye nia mbaya au kulipizana visasi walitaka kutumia zoezi hili kuweza kukomoana kwa kuwataja baadhi ya watu kuwa ni wahalifu kumbe ni uongo na baadhi ya wahamiaji baada ya kukamatwa walikosa sifa za uraia wa Tanzania na hata waliporudishwa kwenye nchi wanazodhaniwa kutoka walikosa sifa za uraia na kuleta mgongano kuhusiana na uraia wao yaani kwa kiingereza (Stateless citizenship) .
Changamoto nyingine zilizojitokeza ni pamoja na ukosefu wa Vitambulisho vya Uraia (Utaifa) ambako kulileta tatizo katika kuwatambua Wahamiaji Haramu na kutokuwepo kwa uzio wa kuzuia mipaka ya nchi yetu hivyo Wahamiaji Haramu wanapopelekwa kwao wanarudi kupitia vipenyo visivyo halali yaani njia za panya.
Sheria ya Maliasili na Utalii (The Forest Act & Wild Life Conservation Act) kutoendana na hali halisi ya uhalifu wa uhujumu wa Maliasilia, mfano kifungu cha 81 (2) kinatoa adhabu ya faini kuanzia shilingi Elfu Thelathini (30,000/=) hadi Milioni Moja na uzoefu unaonyesha kwamba wanaotenda makosa hayo hupigwa faini chini ya Shilingi Laki Tano (500,000/=) bila kujali thamani ya mali aliyokamatwa nayo, isipokuwa maamuzi hutegemea utashi wa Mahakama.
Matarajio
Baada ya kukamilisha Awamu ya Kwanza ya Operesheni Kimbunga tunatarajia Serikali kushughulikia changamoto zilizojitokeza ili kupunguza baadhi ya matatizo katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita hususan yanayohusia na uhalifu na masuala ya kiuhamiaji.
Tunatarajia kuanzisha kikosi kazi kila mkoa kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji wa wahalifu sugu wanaotumia silaha za kivita na wale wanaowafadhili.
Aidha, uhamasishaji utafanyika kuanzia ngazi ya familia, Kitongoji, Mtaa/Kijiji, Kata/Shehia, Tarafa, Wilaya Mkoa na Taifa kuhamsisha jamii kuimarisha misingi ya ulinzi na usalama kupitia kwenye kamati zilizopo na kutoa taarifa mara moja pindi panapojitokeza jambo lolote linalohusu ulinzi na usalama katika maeneo yao.
Aidha, tunatarajia kujipanga kimkakati ili kuona namna ya kushughulikia baadhi ya Wahamiaji Haramu waliokosa sifa za uraia na kurudishwa nchini mwao ambao bado wanang’ang’ania kwa kusema wao ni Watanzania (stateless citizenship).
Washiriki                                                                                                                                      
Operesheni Kimbunga ilishirikisha Vyombo Vya Ulinzi na Usalama wakiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, Uhamiaji, Magereza, TAKUKURU, Taasisi nyingine za Serikali zikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na  Idara za Mifugo,  Ardhi, Kilimo, Uvuvi, Misitu, Afya na Idara ya Wanyama Pori.
Hitimisho
Opereshi Kimbunga ilifanyika kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi. Aidha, suala la Haki za Binaadam lilizingatiwa na hadi sasa hakuna malalamiko yeyote yaliyopokelewa.
 Hata hivyo, juhudi na nguvu zaidi zitaelekezwa katika kukamata Majambazi, Silaha Haramu, Majangili na Wahamiaji Haramu. 
Mafanikio yaliyofikiwa yametokana na ushirikiano wa Maofisa Wakuu Waandamizi, Maofisa wa Kati, Wakaguzi na Askari wote wa vyeo mbali mbali walioshiriki kwenye utekelezaji wa operesheni hii. Kila mtendaji alitimiza wajibu na majukumu yake na ndiyo maana malengo ya utekelezaji wa operesheni hii yamefikwa kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo huu ni mwisho wa Awamu ya Kwanza ya operesheni na mwanzo wa Awamu ya Pili ya Operesheni Kimbunga kwa maana nyingine Operesheni inaendelea mpaka hapo hali ya usalama ya mikoa hii Mitatu itakapokuwa shwari.
 Taarifa hii imetolewa na:
Naibu Kamishna wa Polisi Simon Sirro kwa niaba ya Kamanda wa Operesheni Kimbunga Mwanza, Septemba22,2013

No comments:

Post a Comment