Thursday, September 12, 2013

Hadi 2015 kilomita 18,000 za bara bara zitakuwa zimejengwa nchi nzima-Rais Kikwete

Na Theonestina Juma
“SERIKALI inatumia pesa nyingi katika ujenzi wa barabara, hili ni jambo ambalo wananchi wanapaswa kujua, asilimia kubwa ya fedha zinazotumika katika ujenzi wa barabara hizo zinatokana na kodi zenu,  hivyo mnapaswa kuzilinda na kuzitunza kwa nguvu zote ili zidumu”.
Hiyo ni kauli ambayo haikuisha kinywani mwa, Rais Jakaya Kikwete aliyehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Kagera hivi karibuni ikiwa ni mara yake ya pili tangu awe Rais wa awamu ya nne, na ni mara ya kwanza tangu achaguliwe katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2010.
Hisia na msisitizo mkubwa anatoa katika Wiraza ya Ujenzi ambapo anasema kuwa barabara ni kitu muhimu katika maendeleo ya nchi hasa katika kipindi hiki ambapo shabaha yake kuu ni kuhakikisha kuwa mitandao za barabara kuu zote za mikoa na wilaya nchi nzima zinaunganishwa kwa kiwango cha lami, ili ziweze kuwa kichocheo ya uchumi nchini.
“Barabara ni kichocheo kikubwa cha uchumi hapa nchini, kwani ndiyo njia inayowawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya kuuza ikizingatiwa kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini, licha ya kuwa hazitakamilika 2015 bali atakayekuja atamalizia”anasema.
Rais Kikwete akiwa mkoani Kagera amezindua na kuweka jiwe la msingi miradi mitatu yalioko  chini ya Wizara ya Ujenzi.
Miradi hiyo ni pamoja na barabara ya Kagoma Lusahunga yenye urefu wa kilomita 154 , barabara ya Kyaka –Bugene pia  yenye urefu wa kilomita 56.1 na kivuko cha Mto Ruvuvu kilichoko katika wilaya ya Ngara mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
Rais Kikwete anasema fedha zinazotolewa na serikali, zinatakiwa zitumike kikamilifu katika ujenzi wa barabara na pale ambapo hazitumiki ipasavyo huo, ni udhaifu na uzembe wa madiwani wakishirikiana na watendaji wa halmashauri husika.
Anasema pamoja na mikakati ya serikali kujenga barabara kwa kiwango cha lami, lakini wapo maadui wa  barabara ambao ni  wanadamu, kimazingira kama jua mvuja na kutokana na vitendo wanavyotenda ndani ya barabara hizo, ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa mchanga kwenye madaraja ya barabara, watu kumwaga mafuta aina ya oil barabarani na kubeba mizigo mizito kuzidi kipimo.
Anasema kutokana na vitendo hivyo, ni wajibu kila mmoja kulinda barabara ikiwa ni pamoja na serikali kulazimika kuweka mizani kila sehemu ya barabara kwa lengo la kupima uzito.
Anasema wakati wakianza kujenga barabara ya Lusahunga hadi Kagoma, barabara ya Bwanga –Biharamulo ilikuwa bado baadaye serikali iliacha kidogo ujenzi wa barabara ya Lusahunga –kagoma baada ya kumfukuza mkandarasi wa awali kutokana na kutokuwa na vifaa ambapo iliibuka maneno,  kuwa Waziri wa Ujenzi John Magufuli alikuwa anajipendelea, lakini si kweli bali ulikuwa ni mpango wa serikali.
“Serikali ilitaka usafiri wa haraka kwenda Uganda, si kweli kuwa Magufuli alikuwa anajipendelea na kuwanyima raha wakazi wa Biharamulo, hapana kwani kwa sasa mtu anaweza kutoka Rwanda anaingia Bwanga,  Kyamunyorwa, Muleba, Bukoba kisha Uganda”anasema.
Anasema serikali haitaki mtu anayetoka Muleba, Bukoba  kwenda Isaka Burundi alazimike kwenda Geita, apitie usagara ndipo arudi Isaka kweli ni mzunguko hivyo wanatakiwa kutoka Nyakanazi kwenda Kigoma.
Anasema kwa sasa  baadhi ya barabara ambazo ziko katika mipango ya serikali ni pamoja na barabara ya Kidangwe hadi kigoma, Manyoni kuelekea  Chaya.
Halidhalika kutoka Karua kuelekea Urambo kuingia darajani  ambapo barabara kutoka Kidagwe kwenda darajani wamekubaliana na nchi ya Kuwait  wataijenga wenyewe.
Anasema mipango ya kuunganisha nchi kwa kiwango cha lami kwa sasa kimebakiwa kwa kiwango kidogo, ambapo barabara ya Nyakanazi hadi Kigoma kilomita 50 tayari benki ya Afrika wamekubali kuijenga kwa kiwango cha lami.
Anasema kwa sasa wameanza kujenga barabara ya Kidangwe kwenda Manyoni na Uvinza hadi Mpanda ambayo nayo imo katika mikakati  mpana wa kupanua nchi kwani wanataka ipanuke.
Kuhusu usafiri kutokea Bukoba hadi mbeya, anasema wakazi wa Kagera wamekuwa wakisumbuka kwa kipindi kirefu na usafiri kati ya Mbeya na Bukoba, ambapo mtu hulazimika kupita Dodoma lakini kwa sasa wanataka  mtu akitokea Bukoba akifika Zega, asipite Singida na Dodoma na badala yake wapitie barabara za Tabora, Rungwa,  Makongo ,Matinga tinga, Chunya na kisha Mbeya.
Dkt. Kikwete anasema kwa sasa wameanza kujenga barabara ya Mbeya hadi Chunya mpaka Makongo na baadaye hapo watatoka Tabora kwenda Rungwa.Anasema kutoka Tabora kwenda Mpanda kupitia Makongo Benki ya Afrika imekubali kusaidia serikali ya Tanzania kuijenga.
Kutokana na hali hiyo nchi itakuwa imekamilika kwa mikakati ya kujenga barabara na kuiunganisha kwa kiwango cha lami.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za serikali kuunganisha barabara za mikoa yote kwa kiwango cha lami, Rais Kikwete anatoa onyo kali kuwa serikali haitawaruhusu baadhi ya watu wachache kuzuia utekelezaji wa miradi mbali mbali kama miundombinu hasa barabara kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.
"Serikali itatumia mamlaka yake kupambana na baadhi ya watu
wanaokwamisha maendeleo ya wananchi, ujenzi wa barabara katika maeneo yao"anasema.
Halidhalika anatoa rai kwa makampuni ya Makandarasi nchini kuiga mfano wa kamapuni ya CHICCO ya nchini China inayojenga barabara ya Lusahunga –Kagoma kufanya kazi nzuri kwa kujisimamia na kujindesha wenyewe licha ya serikali kutokamilisha malipo yao kwa wakati.
Anasema hadi barabara hiyo inawekewa jiwe la msingi imebaki mita 500 tu kukamilika na kwamba Kampuni hiyo imejenga barabara hiyo kwa  muda mfupi ambapo hadi sasa bado wanaidai serikali sh.bilioni 40 ambazo watalipwa muda si mrefu.
Anasema pamoja na hali hiyo, serikali itaendelea kuingia gharama kuboresha na kuhudumia sekta ya usafiri kutokana na ukweli kuwa nchi yoyote ambayo watu wake hawawezi kusafiri, uchumi wake hauwezi kukua kwa kasi.
Rais Kikwete anasema maneno haya akiwa anazidua kivuko cha mto Ruvuvu ambapo kabla ya ujio wa kivuko hicho anabainisha kuwa wananchi wa eneo la Rusumo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 50 kwa kuzunguka, kupitia barabara kuu kwenda Ngara Mjini hivyo kupatikana kwa kwa kivuko hicho ni jambo la kujivunia.
Anasema  serikali itaboresha huduma ya usafiri katika sekta ya anga, majini na nchi kavu hii ni  ni lengo na shabaha kuu ya serikali hivyo kila huduma itakayohitajika mfano barabara na njia za reli watajenga ambapo vyote wanafanya ili kuboresha huduma ya usafiri.
Naye Mtendaji Mkuu wa Temesa, Mhandisi Marcelina Magesa akizugumzia juu ya kivuko hicho anasema kuwa matengenezo yake yamegharimu sh.bilioni 2.6 za Kitanzania na kuwa kimetengezwa nchini Uholanzi.
Anasema kivuko hicho kilisafirishwa vipande vipande hadi nchini kisha kuunganishwa hapo mto Ruvuvu.
Bi.Magesa anasema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba magari madogo manne, abiria 50 waliokaa na waliosimama 30 kwa wakati mmoja.
Kuhusu urefu wa kivuko hicho anasema kuwa ni mita 27.8 na upana ni mita 8.75 ambapo kimetengenezwa kwa vifaa maalum kwa ajili ya matumizi ya majini.
Halikadhalika  kivuko hicho kinaendana na ubora wa kimataifa ambapo ukaguzi wake umefanywa na Mamlaka wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) ambayo imewahakikishia kuwa kiko salama kwa usalama wa abira.Pia kivuko hicho kina vifaa vya kisasa vya kutosha kujiokolea kwa rika zote.
Kwa upande wa Waziri wa Ujezi, Dkt.Joh Magufuli anasema kivuko hicho kimewekewa waya maalum ambayo inazuia maji yakija kwa kasi hayawezi kukisomba na kukipeleka katika mto Kagera.
Anasema kwa nchi nzima hicho ni kivuko cha 25 ambavyo vimenunuliwa kwa fedha za serikali ambapo anabainisha matumizi yake kwa wanafunzi wote wa wilayani hiyo ya Ngara kuwa kwa wale wanaovaa sare huvushwa bure ambapo nauli za kuvushwa kwa mtu mzima ni sh.200, watoto  ni sh.50, mizigo chini ya kilo 50 ni sh. 200, pikipiki 500, baikeli 200 , ng’ombe 2,000 na gari yenye tani mbili hadi saba ni sh.7,500.
Dkt. Magufuli ambaye anasema kuwa hajawahi kumpongeza Mkandarasi wa ujenzi yeyote katika maisha yake lakini kulingana na utendaji kazi wa Kampuni ya CHICCO wanapaswa kupewa pongezi.
Pamoja na hatua hiyo, hata hivyo,  Dkt.Magufuli anakerwa na  baadhi ya wasimamizi washauri wa Makandarasi wa barabara ili wasifanye nchi ya Tanzania ni kama sehemu pa kuchotea hela.
Anasema kutokana na kukosekana kwa uadilifu, kwa baadhi ya Wasimamizi Washauri wa Makandarasi nchini wamekuwa wakishindwa kuwasimamia kikamilifu huku baadhi yao wakishirikiana na baadhi ya Makandarasi kufanya Tanzania kama sehemu pa kuchotea fedha na kuondoka.
"Mheshimiwa Rais, naomba kwa ruhusa yako tuzidi kuwafukuza na kuwa simamisha kazi baadhi ya wasimamizi washauri wanaoshindwa kuwasimamia kikamilifu makandarasi wa barabara na kufanya Tanzania kama sehemu pa kuchota hela na kuondoka"anasema.
Anasema katika ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene wasimamizi Washauri ya Kampuni ya Sai kutoka India na kwa kushirikiana na Kampuni ya Data walifukuzwa kazi Januari mwaka huu tayari wakiwa wameshalipwa sh.bilioni 1.9.
Anasema kwa sasa ujenzi wa barabara hiyo inasimamiwa na Wasimamizi washauri zaidi ya saba wote kutoka Wakala wa barabara makao makuomakuu ambapo ujenzi wake umeshafikia asilimia 36.
Hata hivyo anasema maradi huo wa barabara watu zaidi ya 400 tayari wameshalipwa fidia zao isipokuwa watu wane wakiongozwa na mtu mmoja anayemtaja kwa jina, Nehemia Kazimoto ambaye
amekataa kupokea zaidi ya sh.milioni 100 kwa madai kuwa ni kiasi
kidogo.
"Bwana Kazimoto, wewe ni Kazimoto, mimi ni 'moto kazi' nyumba zako zitabomolewa, na kama hutaki kuchuku fidia yako uende mahakamani, tunaheshimu uhuru wa mahakama lakini tutaendelea na kazi yetu"anasema kwa kumtumia salaamu.
 Anasema wananchi wanahitaji maendeleo hivyo tatizo la watu wachache haiwezi kukwamisha wananchi kupatiwa maendeleo.
Anasema  wakati Tanzania ikipata uhuru mwaka 1961 nchi nzima ilikuwa na barabara za lami kilomita 1,330 huku magari yakiwa ni 38,000 tu lakini baada ya miaka kadhaa barabara za lami zimeongezeka hadi kilomita 6,500 hadi 7,000.
Anabainisha kuwa Rais Kikwete ameweza kujega kilomita 11,154 za barabara za lami tagu ameigia madarakani ambapo huenda kilomita zikaongezeka hadi kufikia 18,000 kabla ya kumaliza muda wake.
Anasema kabla ya kujengwa barabara za kuunganisha baadhi ya mikoa hapa nchini, wakazi wa mkoa wa Kagera walilazimika kupitia Kamapala , Nairobi nchini Kenya na kisha kuingia mkoa wa Pwani na ndipo walifika Jijini Dar Es Salaam
Halidhalika kwa aliyekuwa akienda mjini Bukoba akitokea Wilaya ya Karagwe umbali wa kilomita 80 alilazimika kulala njiani siku mbili.
“Wananchi wa Kyaka Bugene, tangu nchi imeumbwa hawakuwahi kuona lami inafafanaje, hadi pale walipowekea lami nyepesi ya majaribio katika barabarakilomita 10 kutoka Kayanga- Omurushaka ndipo waliweza kuona aina ya lami inavyofafa”anasema huku wananchi wakiangua vicheko.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara Taifa, Mhandisi Aaron Mfugale anasema barabara ya Kyaka Bugene inajengwa na Kampuni ya Chicco kwa gharama ya sh.bilioni 64.61 ambapo muda wa utekelezaji wake ni miezi 27 na hatua ya ujenzi wake imefikia asilimia 30.
Anasema  upembuzi yakinifu ya ujenzi wa barabara hiyo ilianza Novemba 2009 na kampuni mmoja ya Kitazania kwa sh. Milioni 386.6 kwa miezi sita kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.
Anasema  jumla ya sh.bilioni 21 ameshalipwa mkandarasi na zaidi ya sh.bilioni 2.888 zimelipwa watu kama fidia kwa mujibu wa sheria, ambapo mradi wa barabara ya Lusahunga-Kagoma ujenzi wa barabara hiyo upembuzi yakinifu ulianza mwaka 1995.
Aidha 2003 alipatikana mkandarasi na kutimuliwa kazi kutokana na uwezo mdogo na baadaye wakapatikana Kampuni ya Chicco waliojenga barabara hiyo kwa miezi 36 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Jumla ya fedha zinazotumika katika mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ni sh.bilioni 191.
mwisho.
 
 

No comments:

Post a Comment