Na
Theonestina Juma, Muleba
KATIKA hali
isiyo ya kawaida baadhi ya wajumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Muleba nusura watwangane
makonde ukumbini wakigombania sababu ya CCM kumwongezea muda aliyekuwa katibu wa CCM wilayani, Bw. Wilbroad
Msafiri baada ya kustaafu kwa mujibu wa kanuni.
Tukio hilo
la aina yake ambayo lilikuwa kama kichekesho kwa wajumbe hao limetokea jana (leo) wilayani humo, baada ya wajumbe
hao kutofautiliana ukumbini hapo, huku kukiwa na kundi la wajumbe wachache
waliokuwa wakiunga mkono kurejeshwa huku asilimia kubwa wakipinga.
Hatua hiyo
ilikuja muda mchache kabla ya wajumbe hao kumkataa Katibu huyo kwa kupiga kura
za ndiyo au hapana.
Mkutano huo
maalum uliokuwa na agenda moja tu kulingana na maelezo ya Mwenyekiti wa CCM
Wilaya, Bw. Muhaji Bushako kilikuwa ni
kumpokea Katibu wao au kumkataa na ulihudhuriwa na wajumbe wapatao 151 kutoka
katika kata zote za wilaya ya uleba ambapo kura tano tu ndizo zilimkubali
Katibu huyo kuendelea huku kura 146 zikimkataa.
Hata hivyo,
kabla ya kufikia hatua ya kupiga kura ukumbuni humo kulikuwa hakukaliki, ambapo
Kamanda wa vijana CCM wilaya ya Mleba, Bw. Mushuti aliamuru vijana wake kuwatoa
nje kwa nguvu baasdhi ya wajumbe waliokuwa wakirushiana maneno makali, karibia
watwangane makonde.
Hata hivyo,
baadhi ya wajumbe wa mkutano huo maalum wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema kuwa sababu ya
kumkataa Katibu huyo ni kutokana na kutokuwa na ushirikiano na baadhi ya
wachama wilayani humo na pia ni mfitini.
Bw. Evad
Ernest alisema kamati ya siasa ilikaa tarehe tofauti mwezi jana baada ya kupata
fununu kuwa Katibu huyo ameongezewa
mkataba wa mwaka mmoja na sekretariet ya kamati kuu ya CCM Taifa kuendelea kukaa Muleba jambo ambalo
walipiga kwani walimtaka apelekwe katika wilaya nyingine.
Alisema
sababu ya kumkataa ni kutokana na kutokuwa na ushirikiano baina ya wanachama, pia anatumia vibaya fedha
za Chama
“Tunashangaa
huyu mtu anaongezewa muda tena anakuja Muleba, wakati alishatuaga kuwa
amestaafu na anarudi kwao kupumzika mambo ya siasa, sasa iweje tena aletwe
Muleba… sisi hatumtaki apelekwe wilaya nyingine”alisema
“Muda wote
aliokaa Muleba hakuna na ushirikiano na
viongozi wenzake, ni mtu mwenye fitina ana eneza majungu kwa baadhi ya
viongozi wenzake,ni mbinafsi amekigawa chama katika makundi, hali iliofanya CCm
kuendelea kushindwa katika chaguzi mbali mbali wilayani hapa”aliongeza.
Alitoa mfano
kuwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 Katibu wao ndiye alikuwa chanzo cha CCM
kupoteza kata 12 na kwenda upinzani baada ya kujitwisha madaraka ambapo aliondoa baadhi ya wagombea
walioshinda kura za maoni na kuwaweka watu wake.
Naye
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Muleba Bw. Bushako aliwazuia wajumbe hao kuacha
kufunga ofisi ya Katibu kama ambavyo baadhi ya wajumbe walivyopendekeza na
badala yake aliwataka wafuate utaratibu na kanuni ya Chama.
Alisema
mambo yanayofuata watalazimika kuyapeleka katika vikao vya ngazi ya juu ya CCM
ambapo waliwataka kila mtu kuheshimu mawazo ya watu wachache bila kuathiri
kanuni za Chama hicho.
“Kulingana
na kanuni za Chama sisis hatuna malmaka ya kumfungia ofisi ya Katibu na badala
yake mamlaka yetu yanafikia hapa ya kumkataa kwa kupiga kura”alisema Mwenyekiti
huyo.
Hata hivyo
kutokana na maelezo yake hayo, wajumbe hao walianza kumzomea ambapo wao walitaka ofisi hiyo
ifungwe mara moja na wala asiingie humo tena.
Hata hivyo
gazeti hili lilipompigia simu, Bw. Msafiri ili kuweza kusikiliza upande wake
baada ya kukataliwa na wajumbe hao simu yake ilipokelewa na mwanamke ambaye
hakutaka kuzungumza na baadaye kukata simu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment