Na
Theonestina Juma, Rorya
KUNDI la
wavuvi wapatao 168 wakiwa na boti 21
wamewatia kiwewe wavuvi wadogo wa mwalo
wa Busanga, Kata ya Nyamtinga wilayani Rorya kwa kuhofia samaki kuisha, baada
ya kuvamia hifadhi ya samaki ya Mang’ereng’ere katika Ziwa Victoria na kuanza kuvua
samaki wakitumia, sumu na makokoro yaliyo chini ya milimita saba na urefu wa
mita 120.
Kundi hilo
la wavuvi hao imeelezwa kuwa walifika
katika mwalo wa Busanga mwishoni mwa mwezi wa Julai, ambapo makokoro hayo
hunasa kila aina samaki ikiwemo na mayai hali inayowatia wasiwasi wavuvi wadogo
kuisha kwa samaki mwalo huo katika eneo hilo.
Wavuvi hao
wanadaiwa kutimuliwa kila mwalo walikofika katika ziwa Victoria upande wa mkoa
wa Mara kutokana na aina ya zana wanazozitumia mfano kama mwalo wa kinesi na
mto mara, kutokana na kuharibu mazalia ya samaki ambapo huvua hadi mayai na samaki
wachanga.
Wavuvi hao
wanadaiwa kuharibu hifadhi za samaki za mang’ereng’ere kata ya Nyamtinga na Nyabiwe kata ya kirogo
maeneo ambayo yametengwa na serikali kwa ajili ya mazalia ya samaki.
Wakizungumza
na gazeti hili baadhi ya wavuvi kutoka katika mwao huo, walisema kundi hilo la
wavuvi kutoka maeneo ya Kibui Kata ya Nyamunga kutokana kuendesha shughuli zao
za uvuvi kwa zana zisizoruhusiwa, wamekuwa wakifanya shughuli hiyo bila kutumia
taa za kama inavyopaswa na badala yake hutumia mwanga wa tochi tu.
“Hawa
wavuvi wanavua samaki wengi mno,kwa siku
hupata samaki kama madebe
30-50,wachanga, wakati na wakubwa, hali inayowafanya kusafirisha kwenda kuuza
nchini Kenya na wengine huwapeleka Musoma na Tarime”alisema mvuvi mmoja.
Wavuvi hao
walisema si kwamba wanawaonea gele, bali hofu
kwa baadhi ya walaji wa bidhaa hiyo kwani kuna wengine wanawavua kwa
kutumia sumu na pia kutoweka kabisa kwa samaki
aina zote za samaki katika
hifadhi hiyo na eneo hilo kutokana na kuharibu mazalia ya samaki.
Halikadhalika
walisema kundi hilo la wavuvi wanaojiita ‘By sisi ‘ wamekuwa wakiwatambia kuwa
hakuna anayeweza kuwachukulia hatua wala kuwazuia kwa sababu wanafahamiana na
viongozi wote na Busanga ndiko kwao.
Kutokana na
tambo hizo, baadhi ya wanawake wa kijiji
hicho, ambao ni wachuuzi wa samaki, wametishia
kuwauwa baadhi ya wanaume kwa kuwawekea sumu kwenye chakula kwa watakaosababisha wavuvi hao kutimuliwa
kijijini hapo.
“Tunapokuambia
taarifa hii, hatutaki hata majina yetu yafahamike, kwani hata baadhi ya
wanawake wa kijiji hiki hatutaki wasikie tunazungumza kuhusu nini, kwa
sababau imefikia hatua ya kututishia
maisha kama tutathubutu hawa watu wazuieliwe kuvua samaki kwa mfumo huu ama
kufukuzwa katika eneo hili”alisema mmoja wao kwa sauti ya chini mno.
Walisema
samaki wanaovua ni pamoja na Nembe, Gogogo, Mumi,Sangara, Furu, Ningu, Sato na
dagaa, ambapo wao hakuna aina ya samaki wanaolenga.
Hata hivyo,
wavuvi hao walionesha kutikishwa na uongozi wa kijiji hicho kuitisha mkutano wa
kijiji ghafla na kuondoa wasimamizi wa mwalo huo kwa madai kuwa wanakula fedha
, ambapo hayo yote yalitokana na baada ya wavuvi hao kuwasili kijiji hapo,na
walikuwa wakipingwa mfumo wa uvuvi wao na BMU.
Hata hivyo
upande wa mwenyekiti wa kijiji cha Busanga, Bw. Paul Festo hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya
mkononi kila alipopigiwa na gazeti hili.
Aidha Afisa wa Doria katika ziwa Victoria mkoa wa Mara,
Bw. Meela akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu , alisema malalamiko hayo
ameshayapokea katika ofisi yake kutoka kwa raia mwema ambapo anayashughulikia.
“Taarifa
hizo nimezipokea, nitakujulisha baada ya kuwasiliana na afisa uvuvi wa Wilaya
ya Rorya, na baadaye nitakueleza ni hatua gani tulizozichukua”.
Hata hivyo,
hadi mwandishi wa habari anatuma habari hizi, tayari Afisa doria, Bw. Meela
ameshawasili wiayani Rorya katika mwalo huo, na kushudia hali halisi, huku
akikosa ushirikiano kutoka kwa wavuvi wa kijiji hicho, ambapo kundi hilo
linadaiwa kupata taarifa mapema ya ujio wa afisa huyo na kufanikiwa kuficha
makokoro yao, ambapo wamebahatika kupata za wavuvi wa eneo hilo ambao nao
wanaendesha uvuvi haramu.
Hali hiyo
imethibitishwa na Bw. Meela ambapo
wakazi wa eneo hilo wanashindwa kutoa ushirikiano kwao, ambapo tayari
watu hao walishaficha nyavu zao na ameahidi kuzitafuta hadi zipatikane.
Habari zaidi
zinasema kuwa Afisa huyo ameshuhudia samaki waliovuliwa hadi mayai na kundi hilo na wavuvi wanaotumia
zana haramu ambapo amewataka kuondoka eneo hilo mara moja na kuacha kuendesha
uvuvi usiostahili katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment