Na Theonestina Juma,Bukoba
OPERESHENI kimbunga inayoendeshwa kwa kushirikisha vyombo
vyote vya usalama katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ya kuwarejesha
wahamiaji haramu makwao na kuwasaka majambazi wanaotumia silaha
imewezesha kuwakamata wahamiaji haramu 6,809 na watuhumiwa wa ujambazi 32.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu Kamisheni wa Operesheni Kimbunga,Simon Sirro ambaye pia ni Mkuu wa
Operesheni nchini wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba .
Kamanda Sirro alisema jumla ya wahamiaji haramu 6,809
waliokamatwa, Wanyarwanda ni 1,446,
Warundi 4,229, Waganda 647, Wakongo 443, wasomali 42, Yemen mmoja na India pia
mmoja na kwamba watu hao wamekamatwa katika mikoa yote mitatu.
Alisema kati ya hao wahamiaji haramu 2,367 wamerejeshwa
makwao kwa maamuzi ya mahakama, 1,866 wamerudi nchini mwao kwa
hiari ,396 wameachiwa huru huku wengine 2,170
wanaendelea kuhojiwa.
Mabomu sita risasi 265 zilizokamatwa
Watuhumiwa wa ujambazi 32 wa unyang'anyo wa wanaotumia
silaha wamekamatwa ambapo wote wamebainika ni raia wa
Tanzania baada ya kukimbiwa na wenzao kutoka nchi jirani wanaoshirikiana nao
katika kufanya uhalifu ambapo Kagera
wamekamatwa majambazi 20, Geita watano na Kigoma saba.
Kamanda Sirro alisema pamoja na majambazi kutoka nchi jirani
kuondoka baada ya kupewa wiki mbili, lakini anaamini kuwa watarejea tena na
hivyo kuwataka kuwachana na kazi hiyo
kwani hailipi.
“Biashara ya ujambazi hailipi, na tunaamini kuwa watarejea
tu, kuendelea kutumia silaha zao, tunawambia hata nasi tunatumia silaha tena ndiyo kalamu
zetu za kila siku, hivyo waachane na kazi hiyo watafute kazi nyingine”alisema.
Halikadhalika risasi 265 za bunduki aina ya SMG/SAR zimekamatwa huku za Mark iv 20 zikipatikana na 82
zikiwa ni za magobole ambapo pia
imekamatwa mitambo miwili ya kutengeneza magobole pamoja na sare za
jeshi la nchi jirani.
Kamanda Sirro alisema katika operesheni hiyo,wamefanikiwa kukamata mabomu sita ya kutupwa
kwa mikono na silaha 22 za aina mbali mbali za moto zilizokuwa zikitumika katika uhalifu.
Kuhusu mifungo, ng’ombe 2,809 nao wamekamatwa ambapo katika
mkoa wa Kigoma wamekamatwa 559, Geita wamepatikana 95 na Kagera ni 2,155, jambo
ambalo Kamanda Sirro ameoneshwa kusitikishwa kutokana na mapori yote yamejaa
mazizi ya ng’ombe na hivyo kufanya hata wanyama waliomo katika mapori hayo kutoishi kwa amani.
Upande wa baadhi ya wahamiaji haramu kulalamika kuwa wananyanyaswa
hasa na Maafisa Uhamiaji, Kamanda Sirro alisema kuwa hakuna mhamiaji haramu
anayenyanyaswa kama baadhi yao wanavyodai, kwani zoezi hilo linazingatia sheria, kanuni, utaratibu zilizopo na haki
za binadamu.
No comments:
Post a Comment