Na Theonestina Juma, Kagera,
RAIA mwingine wa Rwanda,
Bw.Michael John (70) amejinyonga kwa kutumia shuka lake chumbani kwake Wilayani
Missenyi,akihofia kurejeshwa nchini Rwanda na Operesheni kimbunga inayoendelea.
Akizungumza na gazeti hili Mtendaji wa kijiji cha Lwano,
Bw.Deusdedith NjunwaMulokozi alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamukia leo Septemba
16,mwaka huu, katika kitongoji cha Chaibumba kijiji cha Lwano kata ya Ishozi Tarafa ya Kiziba Wilayani Missenyi.
Alisema Bw.John alikutwa na mkewe Bi.Rahel Kagawa (66), mwili
wake ukiwa unaning’inia juu ya dari akiwa tayari ameshakata roho saa 1.07
asubuhi baada ya usiku kukorofishana na mumewe huyo na kuamua kwenda kulala kwa
jirani.
Alisema chanzo cha Bw. John kujinyonga ni baada ya kupata
taarifa kuwa wahamiaji haramu wote wanarejeshwa nchini mwao, ambapo toka siku
hiyo alikuwa akisema kuwa hawezi kurudi Rwanda na badala yake atajiua.
“Chanzo cha Bw. John kujiua ni kuhofia kurejeshwa nchini
mwake Rwanda, ambapo alikuwa akikataa kurudi huko kwa madai kuwa alitoka huko
akiwa kijana na hawezi kurejea tena nchini humo”alisema mtendaji huyo.
Alisema Bw. John aliingia kijijini hapo tangu mwaka 1983 hadi leo hadi
mauti yanamkuta, ambapo alioa mwanamke wa Kitanzania Bi. Rahel ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Ishozi
na kuishi naye kwa kipindi cha miaka 30
na hawakufanikiwa kupata mtoto.
Alisema kabla ya kuchukua hatua hiyo, Bw. John alikuwa
akikorofishana na mkewe na kukimbia
kwenda kulala kwa majirani kutokana na ulevi na kurudi kesho yake asubuhi na
kumkuta akiwa katika hali nzuri.
“Kwa siku ya jana mkewe aliamua kukimbia na kwenda kulala
kwa majirani kama ilivyo kwa wanadoa wanapokorofishana na alirejea asubuhi ili
kuweza kuangalia kama hali imetulia kutokana na ulevi, lakini matokeo yake
amemkutaka akiwa ameshajinyonga”alisema.
Alisema Bi. Rahel
aliporejea nyumbani alikuta mlango ukiwa umefungwa ambapo si kawaida yake, alilazimika kutumia nguvu kufungua mlango huo
na kukuta mumewe akiwa amejinyonga.
Alisema wanandoa hao walikuwa wakiishi maisha ya kawaida tu
na walikuwa wakijishughulisha na kazi ya kilimo pekee.
Mtendaji huyo ametoa wito kwa wahamiaji haramu walioko
katika kijiji hicho kuacha tabia ya kujiua kwani sio jibu na badala yake wafuate sheria na utaratibu unaotakiwa na
serikali kama wanapenda kuishi nchini.
Hili ni tukio la pili la wahamiaji haramu kujingonga, baada ya, Bw. Francis
Mathias (75),mkazi wa kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani kujinyonga
Septemba 9, mwaka huu baada ya mkewe kugoma kuuzwa mali zote ili warejee nchini
Rwanda
No comments:
Post a Comment