Na
Theonestina Juma, Bukoba
TANZANIA, Rwanda na Burundi zimesaini mkataba wa makubaliano ya awali ya
kuanza utekelezaji wa mradi wa kufufua
umeme katika maporomoko ya mto Rusumo ya megawati 80.
Mkataba wa
makubaliano hayo yamesainiwa jana (leo) katika
Manispaa ya Bukoba ambapo ulihudhuriwa na
wajumbe mbali mbali kutoka nchi
zote tatu.
Akifungua
mkutano wa kusaini makubaliano ya mradi
huo, Waziri wa Nishati na Madini nchini, profesa Sospeter Muhongo alisema hatua
hiyo inafungua mlango wa kuanza utekelezaji wa mradi huo.
Alisema
mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka 2015 hadi 2018 ambapo utakuwa takribani
miaka minne hadi kukamilika kwake.
Alisema
katika utekelezaji wa mradi huo umegawanyika katika sehemu mbili ambapo sehemu
ya kwanza wataanza kufufua nishati hiyo, ambayo itagharimu dola milioni 340 kwa pande za nchi zote tatu
na itafadhiliwa na Benki ya Dunia baada
ya kuonesha nia.
Halikadhalika
sehemu nyingine ni ujenzi wa njia ya kusafirishia nishati hiyo kutoka mto
Rusumo hadi Nyakanazi katika njia ya
kwenda nchi jirani ya Burundi, itakagharimu dola milioni 130.
Alisema kati
ya hizo fedha ndizo zitajumuisha masuala ya kufidia watu ambao watatakiwa
kuondoka katika maeneo yao kupisha utekezaji wa mradi huo, ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)imeshaonesha
nia ya kutoa dola milioni 95.
Halikadhalika
kati ya dola hizo milioni 130 benki zingine nazo zimekubali katika kuwasaidia,
ambapo alizitaja benki hizo kuwa ni pamoja na Beenki ya misaada ya ujerumani (
KFW), benki ya ujasiliamali ya ujerumani na benki ya Uholanzi.
Profesa
Muhongo alisema pindi mradi huo utakapokamilika
utaweza kuzalisha umeme megawati 80 ambapo kila nchi itapata mgawao sawa ambao ni megawati 27.
Hata
hivyo,Waziri Muhongo alitoa tahadhari kwa pande zote za nchi hizo tatu kuwa
makini katika harakati za utekelezaji wa mradi huo, kwa kuondoa ukiritimba
unaoweza kujitokeza na kusababisha kuvunjika kama ilivyotokea kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki
mwaka 1977.
“Katika harakati
za utekelezaji wa mradi huu, lazima nchi zote kuwa makini, kuondoa ukiritimba
unaoweza kujitokeza ya mtu kuajiri ndugu zake… hasa masuala ya
rushwa…,tunahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo ya wananchi”alisema.
Alisema
iwapo mradi huo utakamilika nchi zote tatu zitaweza kuwa na nishati hiyo ya
kutosha na hata kuanza kujenga mtandao kwa nchi jirani kwa lengo la kuwauzia.
Alisema hadi
kufika mwaka 2015 Tanzania itakuwa na megawati ya umeme 3,000 ambapo kwa
sasa nchi unao megawati 1,501.2.
Naye Waziri
wa Miundombinu kutoka nchini Rwanda, Profesa Silas Rwakabamba akizungumza
katika mkutano huo, kabla na baada ya kusaini mktaba wa makubaliano hayo,
alisema mradi huo utakapokamilika utawezesha wananchi kupata umeme wa kutosha
na hivyo kuwa kichocheo cha ukuwaji wa uchumi katika nchi hiyo.
“Mimi ni
shahidi katika makubaliano haya kwa nchi yangu, tunaamini nishati ya umeme ni
muhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi”alisema.
Mradi wa
kufufua umeme katika maporomko ya mto
Rusumo kupendezwa kuanza tangu mwaka 1974 , ambapo hata hivyo
utekelezaji wake haukuweza kuendelea hadi mwaka 2005 upembuzi yakinifu
ulipoanza na kwa sasa utekelezaji wake unaanza.
Mawaziri
waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Profesa Sospeter Muhongo kutoka
Tanzania, Waziri wa Miundombinu, Profesa Silas Rwakabamba wa Rwanda na Waziri wa nishati na Madini, Bw. Manirakiza
C'ome kutoka nchini Burundi na Naibu
Kamishna wa nishati ya masuala ya umeme nchini, Mhandisi Innocent Luoga.
Pia
wawakilishi kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika, Bi. Stella Mandago na wa
Benki ya Dunia, Bw. Paul Baringanire.
No comments:
Post a Comment