Operesheni Kimbunga Mnyarwanda ajitia kitanzi, baada ya kutakiwa kurejea kwao
Na Mwandishi Wetu, Kyerwa
RAIA mmoja wa Rwanda amejinyonga kwa kamba chumbani kwake, baada ya mkewe raia wa Tanzania kugoma mali zao kuuzwa ili waweze kurejea nchini Rwanda.
Kutokana na tukio hilo la kujinyinga ambalo linalohusishwa na zoezi linaloendelea hivi sasa nchini la kuwasaka
wahamiaji haramu na kuwarejesha makwao.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu amejulikana kwa jina la Bw.
Francis Mathias (75),mkazi wa kitongoji Kikukuru kata
Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
Habari hizo zina sema kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo ya kujinyoga
familia hiyo iliingia katika mafarakano, ambapo marehemu alipendekeza
wauze mali zao ili kuweza kurejea nchini Rwanda jambo ambalo Mwanamke
alikataa kwa adai kuwa yeye hawezi kwenda Rwanda.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru,Bw. Joseph Leo, jana alilithibitishia
blog kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa hizo kutoka kwa
binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.
“Baada ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango
wa chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja
tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na
kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.
Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania
zinazokadiriwa kufikia Shilingi milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000
na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.
Bw.Leo alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata
Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia
kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi.
Alipotakiwa na blog kuthibitisha kama kweli mwananchi wake
aliyejinyonga alikuwa raia wa Rwanda,Bw.Leo alithibitisha na kufafanua
kuwa tayari alikwisha kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika
opereshani iliyoanza Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu
wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Bw.Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.
Naye Ofisa Tarafa ya Mabira, Bw.Nicolaus Rugemalira, alisema uchunguzi wa
awali wa kimazingira umeonyesha kuwa kulikuwa na mgogoro wa familia
baada ya marehemu kutaka wauze mali zao zote warudi Rwanda, lakini
familia yake haikukubaliana naye kutokana na mkewe kuwa raia wa
Tanzania.
“Mke wake ni Mtanzania, inaonekana baada ya familia yake kukataa uamuzi
wake wa kuuza mali zote ili waondoke, aliamua kuchukua uamuzi huo,”
alisema Rugemalira.
Akizungumzia tukio hilo, binti wa marehemu, Bi. Melania Francis,
alithibitisha kuwapo ugomvi kati ya baba yake na mama yake hali
iliyosababisha mama yao kuondoka bila kufahamika alikoelekea.
Alisema siku ya tukio aliamka na kuwaandaa wadogo zake kwenda shuleni na
baada ya hapo alikwenda shambani kuona kama vibarua wameanza kazi ya
kulima, lakini aliporudi nyumbani alishangaa kuona mlango wa chumba cha
baba yake bado umefungwa wakati haikuwa kawaida yake kulala hadi saa
moja.
Melania alisema alibisha hodi bila majibu, akajaribu kufungua
ikashindikana na alipochungulia aliona fedha nyingi zimetapakaa ndipo
alipokimbia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.
“Nafahamu baba alikuwa na uwezo wa kumiliki fedha hizo, lakini sikufahamu anazihifadhi wapi,” alisema binti huyo wa marehemu.
Alisema wamezaliwa watoto watano katika familia hiyo na kwamba ndugu
zake wawili walitoweka na kubakia watatu na kuongeza kuwa kuwa anatambua
kuwa baba yake alikuwa raia wa Rwanda.
Alipotakiwa kueleza kama anafahamu alikoelekea mama yake, binti huyo
alidai kuwa hafahamu ingawa anafahamu kuwa ni mzaliwa wa Wilaya ya
Ngara, mkoani Kagera.
Kutokana na kutoweka kwa mama huyo pamoja na wanafamilia wengine,
uongozi wa eneo hilo unaendelea na ufuatiliaji ili kujua wanafamilia
wengine wamekwenda wapi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, akizungumza kwa njia
ya simu jana, alisema kwa sasa yuko katika operesheni inayoendelea ya
kuwasaka wahamiaji haramu na kuwa angefuatilia taarifa hizo baadaye
baada ya kuwasiliana na watendaji walioko chini yake.
No comments:
Post a Comment