Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizindua Bwalo la Shule ya Sekondari ya Wasichana
ya Weruweru ya Moshi Vijijini ikiwa na sehemu ya maadhimisho ya miaka
50 ya shule hiyo Septemba 21, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akipanda mti kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari
ya Wasichana ya Weruweru ya Moshi Vijijini akiwa katika maadhimisho ya
miaka 50 ya shule hiyo Septemba 21, 2013. Wapili kushoto ni mkewe
Tunu na Watatu kushoto ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Wapili kulia ni Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim
Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Baadhi
ya Wanawake waliosoma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya
Weruweru ya Moshi Vijijini wakiimba wimbo wa Shule hiyo katika
maadhimisho ya miaka 50 ya shule hiyo Septemba 21, 2013. (Picha na
Ofisi ya waziri
………………..
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania kuiga mfano wa shule ya
Sekondari ya Weruweru ambao wahitimu wake wa zamani (Alumnae) wameamua
kuchangisha fedha na kukarabati shule yao ya zamani.
Ametoa
kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Septemba 21, 2013) wakati akizungumza
na mamia ya wanajumuiya waliohitimu katika shule hiyo (Alumnae),
wanafunzi waliopo pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria sherehe za
Jubilei ya miaka 50 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Weruweru.
Waziri
Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo alisema:
“Watanzania wengi tuna nafasi za kuchangia shule zilizotusomesha. Tuige
mfano wa wenzetu wa Weruweru, tukutane na kusaidia shule tulizosoma,”
alisema.
Alisema
yeye alisoma sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1965 na 1967 lakini
kumekuwa na juhudi mbalimbali za kuwakutanisha wahitimu wa shule hiyo
ambazo hazijawahi kufanikiwa. “Ninawataka mtembee kifua mbele kwa sababu
shule yenu imeza yunda zuri sana,” alisema huku akiwasifia wana
Weruweru waliohitimu zamani kwa kuamua kuja na wazo hilo jema la
kukarabati shule yao ya zamani.
Mapema,
akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Weruweru, Bibi Rosalia
Frimini alisema shule hiyo iliyoanzishwa Oktoba 22, 1963 hivi sasa ina
wanafunzi 570 wa kidato cha tano na sita tu wanaosoma michepuo ya PCB,
EGM,ECA, HGE, HGK na HKL.
Alisema
shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa
maabara, madarasa, mabweni na mifumo ya umeme. Alisema shule hiyo ina
upungufu wa watumishi wakiwemo manesi, wapishi, mkutubi na walinzi.
“Shule
pia inakabiliwa na tatizo la usafiri. Landrover 110 iliyopo shuleni ni
ya tangu miaka ya 80 na matengenezo yamekuwa makubwa, tunaomba
utusaidie kutatua tatizo la usafiri… tunapata shida hasa ikitokea watoto
wanaumwa na wanatakiwa kupelekwa hospitali ya mkoa,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Dk. Maria Kamm ambaye aliongoza shule hiyo kwa miaka 22 kuanzia mwaka
1970 hadi 1992, aliiomba Serikali irudishe mfumo wa kidato cha kwanza
hadi cha nne kwa shule kongwe ambao ulifutwa na Serikali. Alisema katika
kujenga maadili kwa watoto, inabidi waanze tangu wanapoingia sekondari.
“Hawa
wa kidato cha tano na cha sita ni wa kupita tu.. umri wa kuumba binti
ni kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Tunahitaji kuumba mabinti wa
Taifa hili kama ambavyo tulikuwa tukifanya huko nyuma,” alisema.
Alisema
Sera ya Taifa ya Elimu ya Kujitegemea ilikuwa ndiyo siri kubwa ya
kuwaumba wasichana waliopitia shuleni hapo na kwamba ilileta usawa na
kuondoa ubaguzi. “Sera hii ilifanya watoto wote wawe sawa, iliondoa
ubaguzi shuleni kwa sababu wanafunzi wote walijifunza kazi na kujiamini.
Na yote hii ni katika kujenga nidhamu kwa watoto wetu,” alisema.
“Elimu
ya Kujitegemea siyo siasa kama wengi wanavyodhani, ni jadi ya mwafrika,
ni jadi ya mwanamke. Kujitegemea ndiyo msingi wa maendeleo ya Taifa
lolote ulimwenguni, tunaomba Serikali irudishe elimu ya kujitegemea
shuleni ili tuwasaidie watoto wetu.”
Naye
Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro
ambaye ni mhitimu wa shule hiyo alisema Jubilei ya miaka 50 ya Weruweru
ni sehemu ya kusherehekea ndoto iliyotimia na ndoto iliyokuwa kweli kwa
wanafunzi wengi waliosoma kwenye shule hiyo.
“Shule
hii ni ya pekee kwa sababu ilitoa fursa kwa mtoto wa kike pale ambapo
hapakuwa na fursa… ilikuwa ni mchanganyiko wa watoto wa viongozi,
wafanyakazi na wakulima”.
Akimnukuu
Rais wa zamani wa China, Mao tse Tung, aliyesema wananwake wanashikilia
nusu ya anga, Dk. Migiro alisema kutokanana usemi huo haiwezekani watu
wanaoshikilia nusu ya anga wakaendelea kubaki nyuma.
Alisema
shule hiyo imetoa wataalamu mbalimbali wakiwemo wanadiplomasia,
wanasiasa, viongozi mbalimbali wa mashirika, taasisi na serikali na pia
imetoa rubani wa kwanza mwanamke hapa nchini.
Baadhi
wa wanafunzi waliohitimu katika shule hiyo ni Dk. Asha-Rose Migiro, Dk.
Mary Nagu, Balozi Mwanaidi Maajar, Bi. Anna Kilango Malecela, Dk. Mwele
Malecela, Dk. Hellen Kijo-Bisimba, Hajat Amina Mrisho na wengine wengi
ambao wameshika nafasi mbalimbali za uongozi katika mashirika, taasisi
na Serikalini.