Tuesday, July 30, 2013

Maofisa wa TANESCO msiwaringie wananchi wanapohitaji kuunganishwa umeme ndani ya nyumba zao-Rais Kikwete



Na Theonestina Juma, Kagera
WANANCHI wametakiwa kuchangamkia fursa ya umeme mara ifikapo katika maeneo yao  kwa kuingiziwa ndani ya nyumba zao kwa ajili ya kuchochea maendeleo yao.
Rai hiyo imetolewa na Rais Jakaya Kikwete kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi Kata ya Nyaishozi Wilayani Karagwe na Manispaa ya Bukoba.
Rais Kikwete alisema  serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa nishati ya umeme na kufikia megawati 3,000 ifikapo mwaka 2015.
Alisema katika mpango huo pia itaiunganisha katika grid ya taifa mikoa yote nchini ili kuharakisha maendeleo ya wananchi  ikiwemo maeneo ya vijijini.
Alisema “ umeme wa grid ya taifa ndiyo tunaupa kipaumbele, kwa vile ndiyo kitakuwa kichocheo cha maendeleo kwa wananchi”alisema.
“Umeme wa Uganda hautoshi, kwani hata  Waganda wenyewe umeme huo hauwatoshi, huo umeme si kwa ajili ya uzalishaji kulingana na jinsi ulivyo”aliongeza.
Alisema mpango wa kuongeza uzalishaji wa umeme unakwenda pamoja na kuongeza uwezo wa  kuusambaza na kuunganisha mikoa ambayo haikuwa katika grid ya taifa.
Alitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Kagera,Mtwara, Ruvuma ,Lindi, Katavi, Ruvuma,Rukwa, na kigoma.
Hata hivyo Rais Kikwete aliwageukiwa Maofisa wa TANESCO na ksuema kuwa wanatakiwa kutambuwa kuwa wanaishi kwa kuuza umeme hivyo tabia ya kuwaringia wananchi pindi wanapotaka waunganishiwe nishati hiyo ndani ya nyumba zao waache.
“Kuna baadhi ya maofisa wa Tanesco wananchi wakihitaji waingizie umeme ndani ya nyumba zao, wanataka mpaka wabembelezwe, wahongwe … ofisa heshima yako inapungua kwa tabia hiyo”alisema Rais kwete.
Katika hatua nyingine Rais Kikwete aliwataka wananchi wanapokuwa wakidai haki yao lazima nao watimize wajibu wao  wa kuunganishwa nishati hiyo katika nyumba zao.
Halikadhalika alisema wananchi hao wakiwa hodari kudai nao wawe hodari katika utekelezaji ili uwekezaji wa nishati hiyo ilingane na usambazaji na uunganishaji.
Aidha  kwa upande wa Waziri wa Nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema bajeti ya wizara hiyo imeongeza kutoka sh. bilioni 600 hadi kufikia trioni 1.2.
Alisema kwa sasa serikali ina mpango wa kuachana na umeme wa mitambo ya mafuta kutokana na gharama kubwa ya uendeshaji  ambapo serikali imepanga kuongeza kasi ya kupeleka umeme maeneo ya vijijini.
Hata hivyo, Profesa Muhongo aliwataka madiwani nchini  kupunguza safari za halmashauri ili fedha zipatikane za kuunganisha umeme wa jua katika maeneo ya shule za sekondari nchini kupitia wakala wa umeme vijijini [REA]..
“Umeme wa jua kuunganishwa katika shule moja ya sekondari katika vyumba vinane  gharama yake sh. milioni 3.9, ni kiasi kidogo sana, shule za sekondari hasa maeneo ya vijiji wanaweza kuingiziwa umeme wa jua , kama madiwani watapunguza safari zao ndani ya halmashauri”alisema Profesa Muhongo.
Alisema halmashauri zinatakiwa kushirikiana na REA kupeleka umeme vijijini, badala ya kubaki kusubiria serikali kuu.

No comments:

Post a Comment