Rais Jakaya Kikwete ameingilia kati ugomvi uliopo kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Hamis Kaghasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Amani, kwa kuwataka wakae chini na kumaliza tofauti zao.
Rais aliyasema hayo katika uwanja wa Kaitaba alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku situ mkoani Kagera aliyoianza Jumatano wiki iliyopita.
“Mbunge na Meya wakiendelea kutiliana shaka wanaoumia ni wananchi, malizeni tofauti zenu kwa sababu hakuna lisilokuwa na mwisho,” alisema.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema masuala yaliyokuwa yakiwagonganisha Meya na Balozi Kaghasheki ambaye ni Mbunge wa Bukoba Mjini, ya ujenzi wa soko pamoja na viwanja ni mambo ya maendeleo.
Katika ugomvi huo, Kaghasheki anapinga ujenzi wa soko jipya mjini Bukoba kwa madai kwamba haukufuata maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani wakati Meya akisisitiza ujenzi huo kwa maelezo kwamba maamuzi ya ujenzi yamepitishwa kwenye vikao vya baraza la madiwani.
Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko ni suala la maendeleo na lazima lijengwe kwani wakazi wa Bukoba hawawezi kubaki katika mfumo wa analogia wakati sasa watu wanaingia katika giditali.
Alisema kabla ya wafanyabishara wa soko kuu hawajahamishwa lazima uongozi wa Manispaa iwatafutie eneo wajasiriamali wanaoendesha biashara zao kwenye soko la sasa ambalo litavunjwa na kujengwa jipya, kwani hapo ndiko asilimia kubwa wanategemea kupata riziki yao ya kila siku.
.
Alisema "lazima wale wafanyabishara watakoondolea ndani ya lile soko, baada ya kukamilika kwa ujenzi wake wao ndiyo wawe wa kwanza kupatiwa maeneo, na sio kupewa kipaumbele, kwani neno hilo limejaa walakini mwingi, labda wanaweza kufikiriwa wakati wengine wameshapewa maeneo ya biashara, .... wawe wa kwanza kupangishwa mule"alisema
“Ujenzi wa soko ni maendeleo na karne hii ni ya teknolojia, ni uamuzi mwema; mkitaka mambo ya zamani basi na nyinyi mtakuwa ni watu wa kizamani,” alisema.
“Katika mradi huu mpya wa viwanja 5,000 kwanza wapeni hao 800 wa zamani maana walikwishalipia hilo ni deni la manispaa wala haliwezi kukwepeka hata kama viongozi wa sasa hawakuwapo wakati huo, lakini halmashauri ilikuwepo” alisema Rais Kikwete.
Aidha kuhusus kutojulikana idadi kamili ya viwanja vilivyopimwa katika manispaa ya Bukoba, Rais Kikwete alisema viongozi hawawezi kuishi kwa kushukiana bali wanatakiwa kuaminiana.
Maelezo yaho ya Kikwete yalitoka na malalamiko yaliotolewa na Balozi Kagasheki pamoja na mambo mengine kuhusu kero ya soko kuwa imeleta malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na kutofuatwa kwa baadhi ya taratibu ikiwamo waliomo kutojua watahamishiwa wapi wakati soko hilo likijengwa na muafaka wao baada ya ujenzi.
Kuhusu ardhi, alisema viwanja 5,000 vilivyopimwa havifahamiki na kwamba baadhi ya wananchi hawakupewa fidia na wengine walilipwa kidogo na kwamba wanaodai viwanja ni 800 na walikwishalipa tangu mwaka 2003.
Alisema Manispaa inawataka wananchi hao kuongeza fedha ndipo wapewe viwanja vilivyopimwa katika mradi wa sasa.
Mgogoro kati ya viongozi hao ulianza baada ya uongozi wa Manispaa kutangaza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa soko jipya na la kisasa na upimaji wa viwanja 5,000.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jason Rwekiza, alisema bei ya kahawa inayotolewa na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo (KNCU), haikidhi mahitaji ya wakulima.
Kadhalika, alizungumzia utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein ya ujenzi wa barabara ya Bukoba –Bugabo Rubafu yenye urefu wa kilometa 42 lakini bado haijajengwa.
Kero nyingine alitaja kuwa ni mradi wa umeme vijijini akieleza kuwa baadhi ya vijiji havikuingizwa kwenye mpango wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Kivuko cha Kyanyabasa, pamoja na mradi wa maji vijijini kwamba kati ya vijiji 10 ni kimoja tu kilichotengewa fedha.
Akijibu hoja ya barabara na kivuko, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema itatengewa fedha pindi zitakapopatikana na kwamba kuhusu kivuko, serikali inaangalia utaratibu wa kujenga daraja.
Kuhusu kero ya maji, Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, alisema vijiji tisa vilivyotajwa na mbunge viko kwenye bajeti na kuzitaka halmashauri kutekeleza miradi ya vijiji vyote na kwamba wananchi watachangia baadaye.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema ni dhamira ya serikali kuviunganisha vijiji vyote kwa umeme ifikapo mwaka 2015.
Rais ameziagiza halmashauri zote nchini kutatua kero ndogondogo za wananchi kama ushuru wa mazao kwa kuwa ziko ndani ya uwezo wao badala ya kumsubiri yeye.
No comments:
Post a Comment