Thursday, August 1, 2013

Serikali Kagera yasitisha utoaji vibali kwa wageni, donge nono latangazwa kwa mwananchi atakayetoa taarifa ya anayemiliki silaha

Na Theonestina Juma,Bukoba
UONGOZI wa mkoa wa Kagera umesitisha utoaji wa vibali  kwa muda vya kuingia na kukaa nchini kuanzia leo  kupisha operation wa majambazi,wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, ikiwa ni kutekeleza agizo ya Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamesemwa  jana {leo} na Mkuu wa mkoa Kagera kanali Fabian Massawe katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Bukoba.
Alisema vibali hivyo vinasitishwa kutolewa na idara ya uhamiaji hadi pale msako huo utakapoisha.
Kanali Massawe  alisema mbali na hiyo pia imetangaza donge nono kwa wananchi ambao watawapatia taarifa sahihi kwa wale ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na wahamiaji haramu katika maeneo yao.
Kanali Massawe alisema “kwa mtu yeyote atakaye tupa taarifa sahihi juu ya mtu ambaye anamiliki silaha kinyume cha sheria tutampatia sh. 100,000”.
Alisema  watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanatakiwa kuzisalimisha kwa viongozi wa kata, vitongoji wenyeviti wa vijiji, tarafa, katika vituo vya polisi na hata katika ofisi ya mkuu wa mkoa.
“ kwa sasa zimebakiwa takribani siku 10 msako huo kuanza, hivyo kwa yeyote asiyetaka kusalimisha sihala na hata yule mhamiaji haramu ambaye hataki kuondoka nchini kwa utaratibu asije akatulilia”alisema.
Alisema si kwamba Watanzania hawapendi wageni, lakini wanatakiwa kuingia nchini kwa kufuata utaratibu wanchi husika, na si kuja kwa kujificha bali wanatakiwa kuja kifua mbele kwa kufuata sheria zilizopo.
Alisema ulinzi wanchi ni wa kila mmoja na ndiyo maana wanasisitiza ulinzi shirikishi na hii ni kutokana na polisi waliopo ni wachache  na hivyo hawawezi kuachiwa wao peke yao.
Aidha alitoa tahadhari kwa wale wananchi wanaowahifadhi wahamiaji kuwa wakipatikana nao watafanywa kama wahamiaji haramu hao.
Hatua hiyo inakuja baada ya Rais Kikwete kufanya ziara ya siku sita mkoani hapa, na kusitiksihwa na maisha wanaoishi wakazi wa mkoa kagera ambao hawawezi kusafiri bila kusindikizwa na polisi wenye silaha.
Julai 26, mwaka huu Rais Kikwete akiwa wilayani Biharamulo katika moja ya ziara yake hiyo, alitangaza nchi kuendesha msako mkali wa kuwasaka majambazi, wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Katika msako huo unaotarajiwa kuanza siku 10 zijazo majambazi , wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha watasakwa ndani ya nyumba zao, mapori na handaki walizochimba kuficha bunduki zao.
Alisema katika msako huo hakuna cha msalia mtume, kwani wahamiaji haramu wametakiwa kuondoka kwa  amani bila kusubiri msako huo  kwani hataki ugomvi na nchi jirani bali anataka watanzania wabaki waishi kwa amani na kwamba haiwezekani  Mtanzania akiwa kama mkimbizi ndani ya nchi yake.


No comments:

Post a Comment