Monday, July 29, 2013

Rais azindua kivuko kipya Mto Ruvuvu



Na Theonestina Juma,Ngara
 RAIS Jakaya Kikwete amesema serikali itaendelea kuingia gharama kuboresha na kuhumia sekta ya usafiri kwani nchi yoyote ambayo watu wake hawawezi kusafiri,uchumi wake hauwezi kukua kwa kasi.
Rais Kikwete amesema hayo jana  wakati akizindua kivuko cha mto Ruvuvu kilichoko kata ya Rusumo wilayani Ngara mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
"Nchi ambayo watu wake hawawezi kusafiri, vyombo vya usafiri ni kidogo uchumi wake hauwezi kukua, hivyo serikali itaendelea kuboresha sekta hiyo"alisema.
Alisema kabla ya kuletwa kwa kivuko hicho wakazi wa eneo la Rusumo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 50 kwa kuzunguka kupitia barabara kuu kwenda kwenda Ngara Mjini, hivyo kupatikana kwa kwa kivuko hicho ni jambo la kujivunia.
Alisema serikali itaboresha huduma ya usafiri katika sekta ya anga, majini na nchi kavu.
Kutokana na hali hiyo aliwataka wakazi wa eneo hilo kukilinda na kukitunza kivuko hicho ili kiweze kudumu.
Aliwataka wakazi wa eneo hilo kudumisha amani na utulivu ili waweze kupata maendeleo.
Naye Waziri wa Ujenzi,Dkt.John Magufuli katika  uzinduzi wa kivuko hicho alisema kivuko hicho kimenunuliwa na fedha ya serkali zaidi ya sh.bilioni 2.9.
Alisema fedha zote zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ununuzi wa kivuko hicho ambacho kilikuwa ni ahadi ya Rais zimetumika zote.
Dkt.Magufuli alisema kivuko hicho kimewekewa waya maalum ambayo inazuia maji yakija kwa kasi hayawezi kukisomba na kukipeleka katika mto Kagera.
Alisema kwa nchi nzima hicho kuna vivuko zaidi ya  25 ambavyo vimenunuliwa kwa fedha za serikali.
Alisema katika kivuko hicho wanafunzi wanaovaa sare huvushwa bure ili baadae huenda wakawa wahandisi wa nchi hii.
Awali  Mtendaji Mkuu wa TemesaTaifa, Mhandisi Marcelline Magesa akitoa taarifa ya kivuko hicho alisema matengenezo ya kivuko hicho kimegharimu sh.bilioni 2.9 na kimetengenezwa nchini Uholanzi.
Alisema kivuko hicho kilisafirishwa vipande vipande na baade kuunganishwa hapo mto Ruvuvu.
Bi.Magesa alisema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba magari madogo manne, abiria 50 waliokaa na waliosimama 30 kwa wakati mmoja.
Alisema urefu wa kivuko hicho ni mita 27.8 na upana ni mita 8.75 ambapo kimetengenezwa kwa vifaa maalum kwa ajili ya matumizi ya majini.
Alisema kivuko hicho kinaendana na ubora wa kimataifa ambapo ukaguzi wake umefanywa na Mamlaka wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) ambayo imewahakikishia kuwa kiko salama kwa usalama wa abira.
Hali kadhalika kivuko hicho kina vifaa vya kisasa vya kutosha kujiokolea kwa rika
zote.

No comments:

Post a Comment