Monday, July 29, 2013

Kushamiri kwa magendo ya kahawa Kagera , Rais Kikwete aunda kamati ya kufuatilia chanzo



Na Theonestina Juma
RAIS Jakaya Kikwete amelazimika kuunda kamati ndogo ya kufuatilia tatizo la wakulima kuuza kahawa nchi jirani kwa njia ya magendo badala ya kuuzia vyama vya ushirika vya mkoani hapa.
Rais Kkwete alilazimika kuunda kamati hiyo ndogo akiwa Wilayani Karagwe itakayoongozwa na Waziri wa ardhi na makazi, Profesa Anna Tibaijuka lengo likiwa ni kutaka kujua ni sababu zipi zinazopelekea wakulima kuuza kahawa yao nchini Uganda kwa njia ya magendo.
Alisema kitendo cha wakulima kuuza kahawa yao nje ya nchi kwa njia ya magendo ni kujinyima maendeleo yao pamoja na nchi na kukuza uchumi wan chi jirani.
“Nataka nijue ni kwa nini wakulima wa mkoa huu wanauza kahawa yao  nchi jirani tena kwa njia za magedo, na nini kifanyike,ndani ya miezi miwili naomba nipate taarifa hiyo”alisema.
Rais Kikwete alisema mbali na kamati hiyo kuongozwa na Profesa Tibaijuka pia itahusisha wakulima wa zao la kahawa pamoja ndizi, Wizara ya kilimo na ushirika na Wataalam wa kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera na vyama vya ushirika vya mkoani hapa.
Aidha idara ya viwanda na masoko  nao watahusishwa kwa jili ya kufuatilia bei ya masoko kama ndiyo sababu kuu inayowafanya wakulima kuuza kahawa nchi jirani.
Halikadhalika aliitaka kamati hiyo pia kuchunguza ni kwa nini watu wengi wanapenda kahawa kutoka Tanzania aina ya Organic ambayo wakulima hawatumii aina yoyote ya dawa za viwandani.
Alisema tabia ya wakulima kuuza kahawa yao nchi jirani wakati wao hakuna kahawa wanayoiuza humu nchini haliwezi kukubalika.
“kwa nini nyie muwauzie kahawa yenu wakati wao hakuna kahawa wanaowauzia hapa nchini? Kwa nini mdai maendeleo kama ya barabara hapa, kwa nini msiende mkadai huko Uganda mnakowapelekea?alihoji Rais Kikwete.
"Maendeleo mlilie, kahawa mnakimbiza kwingine, kustawisha uchumi wao unapopeleka sehemu nyingine, mnajinyima maendeleo yanu"aliongeza.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wakazi wa mkoani hapa kuacha kuuza kahawa yao nchi ya Uganda kwa njia ya magendo kwani kufanya hivyo wanajinyima maendeleo.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameiagiza kamati hiyo ndogo kuangalia ni kwa namna gani wakulima wanaweza kuuza ndizi zao wenyewe nje ya nchi badala ya nchi ya Uganda kuingia nchini na kuulangua na kupeleka nje ya nchi.
Alisema watanzania wanatakiwa kuondoa dhana ya kuwa hawawezi jambo lolote kama ya kuuza ndizi wenyewe nje ya nchi wakati uwezo huo wanao.
“Tatizo watu wanautamaduni ya wanatafuta baya hilo ndilo wanang’ang’abalo wakati kumbe wanaweza, lazima mtoke hapo”alisema
Hata hivyo kwa upande wa Waziri wa kilimo na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiiza alisema kwa sasa  kamati hiyo imekubaliana kufanya uchunguzi huo kwa mwezi mmoja ambapo baada ya hapo majibu yatakuwa tayari.
Alisema licha ya uchunguzi huo utafanywa kwa kutumia mbinu ya kiltelijinsia lakini anamaani kuwa watafanikiwa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment