|
Dodoma
SERIKALI
imesema eneo linalogombewa na Malawi katika Ziwa Nyasa ni mali ya Tanzania na
sasa imeziamuru kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa mafuta kuondoka eneo
hilo kuanzia jana.
Onyo hilo dhidi ya Malawi lilitolewa jana na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia amesisitiza
kuwa Tanzania itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la
kiusalama.
Hii ni mara ya pili Serikali kuionya Malawi katika mgogoro
huo. Wiki iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni
Samuel Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi.”
Sitta
alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey
Zambi aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana,
akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13,
bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo
Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano
zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda
kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika
eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo (jana),” alisema Membe.Alisema
Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na
haitaruhusu utafiti huo wa uchimbaji wa gesi na mafuta uendelee.
Alisema
chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania watakuwa
salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la
kiusalama.Kuhusu kiini cha mgogoro, Waziri Membe
huku akirejea historia ya mipaka tangu ukoloni, alisema ni hatua ya Serikali ya
Malawi kushikilia msimamo kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi wakati
Tanzania inashikilia kuwa mpaka upo katikati ya Ziwa.
“Wenzetu wanadai
ziwa lote lipo Malawi lakini, nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza
mwaka 1928 na 1938 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati,”
alisema.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa
kwa vile tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo baina ya Cameroon na
Nigeria.
Alisema katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Dunia,
iliamuliwa kuwa mpaka baina ya nchi hizo mbili upite katikati ya Ziwa Chad
ukifuata msitari ulionyooka.
“Ni dhahiri, tunalo tatizo kati ya Tanzania
na Malawi linalohitaji kutatuliwa kuhusu mahali hasa ulipo mpaka baina ya nchi
hizi mbili na lilianza tangu enzi ya awamu ya kwanza,” alisema.
Waziri Membe
alisema tatizo hilo lilishindwa kupatiwa ufumbuzi kutokana na Rais Kamuzu Banda
wakati huo akiwa madarakani kuamini kuwa ‘Tanzania ilikuwa ni kichaka cha
kuhifadhi maadui wa Serikali yake.’
“Baada ya mabadiliko ya uongozi,
tulianza kujadili tatizo hilo kwa njia za kidiplomasia na mwaka 2005 iliundwa
tume ya pamoja ya kushughulikia mgogoro huo,” alisema.
Alisema Rais Jakaya
Kikwete alipoingia madarakani alikutana mara mbili na Rais wa zamani wa Malawi,
marehemu Bingu wa Mutharika na kukubaliana iundwe Tume ya Pamoja ya wataalamu
kushughulikia mgogoro huo.
Hata hivyo, alisema wakati tume hiyo ikianza
kukusanya nyaraka mbalimbali, suala hilo lilichukua sura mpya na kuanza
kuhatarisha usalama wa Tanzania na wananchi wake.
Alisema Serikali
ilipata habari za kuaminika kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuwa
eneo lote la Ziwa Nyasa, kaskazini ya Msumbiji limegawanywa katika vitalu
mbalimbali.
“Kwamba Serikali ya Malawi ilitoa vitalu hivyo kwa kampuni za
kutafuta mafuta na gesi na yakaomba kibali cha kuruhusu ndege za utafiti ziruke
katika anga la Tanzania,” alisema.
Waziri Membe alisema ombi hilo
lilikataliwa na JWTZ lakini, Serikali imepata ushahidi kuwa ndege ndogo tano za
utafiti zenye uwezo wa kutua ufukweni na majini zilionekana zikivinjari na kutua
Ziwa Nyasa upande
wa Tanzania Januari 29 na Julai 2 mwaka huu.
Alisema
Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Malawi kwa maandishi na kuomba
ufanyike mkutano wa mawaziri na wataalamu wa nchi mbili kuhusu mustakabali wa
mpaka wa nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulifanyika Tanzania Julai mwaka huu
na baada ya majadiliano, pande zote mbili zilikubaliana kwa kauli moja kwamba
lipo tatizo baada ya kila upande kushikilia msimamo wake.
Alisema pande zote
mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo hayo Agosti 20 hadi 27 mwaka huu,
nchini Malawi ukihusisha wataalamu wa mipaka na sheria za kimataifa wa nchi hizo
mbili.
“Katika mkutano huo, Serikali ya Tanzania iliitaka Malawi
kutoruhusu mtu au kampuni yoyote kuendelea na shughuli za utafiti na tunaonya
hatutaruhusu utafiti huo uendelee,” alisema.
Alisema Serikali inathamini
uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuitaka Malawi kuheshimu makubaliano na
kuongeza kwamba njia nzuri na bora ya kutatua tatizo hilo ni ya mazungumzo ya
amani.
“Katika kipindi chote cha mazungumzo Serikali ya Malawi isiruhusu
shughuli zozote za uchimbaji wa madini na mafuta katika eneo hilo kwa sababu ni
eneo la Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa Serikali inayo dhamana ya kuwalinda
wananchi 600,000 wanaoishi na kutegemea Ziwa Nyasa.
Akichangia hotuba
hiyo, Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa alisema tamko hilo la
Waziri linaonyesha kwamba kilichopo sasa baina ya nchi hizo ni kutunishiana
misuli.
Alisema vita si suluhisho la mgogoro huo na kushauri kuwa iwapo
Malawi imeweka watafiti wa mafuta ziwani, Tanzania
nayo itafute wa kwake nao
waanze kutafiti.
Alisema inavyoonekana mgogoro huo hauwezi kumalizika kwa
mazungumzo yanayofanyika Dar es Salaam, bali kufikishwa kwa wasuluhishi wa
kimataifa, The Hague.
Malawi yajibu mapigo
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Malawi, Patrick Kabambe
alikaririwa na Redio Sauti ya Ujerumani jana jioni akisema kuwa wataendelea na
utafutaji wa mafuta na gesi katika Ziwa Malawi huku akidai kwamba amesikia
Tanzania inapeleka askari eneo hilo.
Waziri huyo alisema hilo ni Ziwa
Malawi na siyo Nyasa na kueleza kuwa utafutaji wa mafuta na gesi utaendelea na
hakuna wa kuwasimamisha huku akihoji Tanzania kuja juu sasa na si wakati
mwingine.
“Tutaendelea kutafuta mafuta na gesi katika Ziwa Malawi na
tunashangaa kwa nini sasa ndiyo wanalalamika na siyo wakati mwingine?”
alikaririwa akisema.
|
|
No comments:
Post a Comment