Na
Theonestina Juma, Bukoba
KILA Mwenyekiti
wa serikali za mitaa atayehusika kuwatembeza makarani katika zoezi la sensa ya
watu na makazi katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba watalipwa sh. 5,000 kila
siku, imeelezwa.
Hayo
yamebainishwa na Mratibu wa sensa ya watu na makazi ngazi ya vituo katika halmashauri ya Bukoba, Bw.
Melchior Komba wakati akizungumza na Wakufunzi wapatao 125 kutoka katika
Manispaa ya Bukoba na halmashauri ya wilaya ya Bukoba.
“Wenyeviti
wa serikali za mitaa na vitongoji ni watu muhimu sana katika zoezi hili,
tunawatambua, hivyo kila atakayehusika katika kuwatembeza makarani wetu wakati
wa zoezi la sensa linalotarajiwa kuanza Agosti 26, mwaka huu atalipwa sh. 5,000”alisema.
Alisema si
kwamba kila mwenyekiti atalipwa hata yule ambaye amekaa nyumbani, bali ni wale
watakaohusika katika kuongoza timu ya uhesabuji kaya moja hadi nyingine.
Alisema
fedha hizo zitakuwa kwa msimamizi katika eneo la kuhesabia, ambaye ndiye
atahusika zaidi na malipo yao hasa kwa wale watakaowaongoza katika zoezi hilo
katika eneo husika.
Aidha Bw.
Komba aliwataka wananchi kuwa makini kujibu maswali ya sensa watakayoulizwa na
makarani wa sensa pindi watakapokuwa wanawafikia, lengo ni kutaka kupata takwimu
sahihi kwa maendeleo ya taifa.
Agosti 12,
mwaka huu, Umoja wa wenyeviti wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Bukoba
walitishia kugoma kushiriki katika zoezi la sensa ya watu na makazi kwa madai
kuwa uongozi wa Manispaa ya Bukoba hauoneshi ushirikiano nao kuhusiana na zoezi
hilo.
Umoja huo
kupitia mwenyekiti wao Yusuf Mbagwa alisema licha ya kuwa vipeperushi
vinavyosambazwa vinaonesha wenyeviti
wanahusika moja kwa moja katika zoezi la sensa lakini hawajawahi kupewa mafunzo
yoyote yanayowaleza majukumu yao katika zoezi hilo.
Halikadhalika
walidai kuwa hawawezi kushiriki katika zoezi bila bila kujua mstakabali yao juu
ya maslahi yao.
No comments:
Post a Comment