Saturday, August 4, 2012

Mshauri wa mahakama ya mwanzo mbaroni kwa tuhuma ya kutaka kuwauzia majambazi silaha

 Pichani ni baadhi ni risasi 248 pamoja na bunduki aina ya SMG aliyokutwa nayo Mshauri wa Mahakama ya mwanzo ya Lusahunga wilayani Biharamulo, Bw. Enos Karoli katika harakati za kutaka kuzipiga bei kwa majambazi wasiojulikana.

Na Theonestina Juma, Bukoba
 JESHI la polisi Mkoani Kagera linamshikilia Mshauri wa mahakama ya Mwanzo ya Lusahunga kwa tuhuma ya kupanga njama ya kutaka kuuza bunduki moja na risasi 248 kwa majambazi.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Kamanda wa polisi Mkoani Kagera ambaye pia ni Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai Mkoani hapa,Peter Matagi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba.
Kamanda Matagi alimtaja Mshauri wa Mahakama hiyo kuwa ni Bw.Enos Karoli (43) Mkazi wa Kabukaishozi Nyakanazi Wilayani Biharamulo ambapo alikamatwa
akiwa na bunduki moja aina ya SMG yenye namba 4707 Magazine moja na risasa za SMG na SAR 248.
Alisema Bw.Karoli alitiwa mbaroni Agosti mosi mwaka huu saa 5 usiku baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna majambazi wanamiliki bunduki.
Alisema polisi walifanikiwa kukamata bunduki hiyo baada ya kuweka mtego.
Kamanda Matagi alisema kutokana na mtego huo wa mauziano ya bunduki walifanikiwa kumkamata Mshauri huyo akiwa ameiweka bunduki hiyo kwenye buti ya gari kwa ajili ya kwenda kuiuza.
Alisema msako wa kuwatafuta majambazi wengine waliokuwa wakishirikiana na mtuhumiwa unaendelea
ambapo mshauri huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.mwisho

No comments:

Post a Comment