UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, kufuatia
taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa kutoa hoja kwamba
Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi
ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha
2012/2013.
Mheshimiwa Spika, awali ya
yote napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza kwa
umahiri mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013. Napenda pia kuwapongeza
Mheshimiwa Job Ndugai (Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wanaokusaidia
kuongoza Bunge hili kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Spika, kwa namna
ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya
Nne. Chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha
amani, utulivu na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee kudumisha hali
hiyo ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa bei yoyote.
Mheshimiwa Spika, niruhusu
niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza kwa
dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa
na Mheshimiwa Rais mwezi Mei 2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa
Kamati za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko
yaliyotokea kwenye nafasi mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali.
Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, kwa njia
ya kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na
Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Wizara
yangu kwa kuwa ndiyo inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje, nawaahidi
Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima kwa kufanya
kazi kwa karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika, naomba
niwashukuru pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.), Waziri wa
Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao za kina ambazo zimetoa ufafanuzi na
miongozo kwa masuala mbalimbali muhimu ya Taifa letu kwa mwaka wa fedha
2012/2013. Kwa ujumla wake, naomba kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote
waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri walizozifanya. Hotuba zao
zote zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na jamii yanayohusu nchi yetu
na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au nyingine.
Mheshimiwa Spika, naomba
nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi mzima wa Wizara
kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya
uongozi madhubuti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati kwa
ushauri wao mzuri ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati
hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na
changamoto zinazoikabili katika kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara
walizozifanya kwenye nchi mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya
kujionea wenyewe na kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali
zinazotukabili kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri
Serikali.
Mheshimiwa Spika, natoa
shukrani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano anaonipa katika
kutekeleza majukumu ya Wizara. Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John
M. Haule, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu,
Wakurugenzi, Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika
kuiongoza Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika
kutekeleza majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea
maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, shukrani
za pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na
hasa wana-Mtama wote. Napenda pia nimshukuru mke wangu Mrs. Membe na watoto
wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha
kwangu.
Mheshimiwa Spika, kabla ya
kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane na Viongozi wote,
Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote
waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea Zanzibar. Kwa
wale wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza, namwomba Mwenyezi Mungu awape
nguvu waweze kupona haraka.
Mheshimiwa Spika, vilevile,
natoa salamu za pole kwa wale Wabunge wote waliopatwa na misiba ya wapendwa wao.
Kwa wote, namwomba Mwenyezi Mungu awape faraja na azilaze Roho za Marehemu
mahali pema peponi. Amina.
TATHMINI YA HALI YA DUNIA
KWA KIPINDI CHA 2011/2012
HALI YA
DUNIA
ULAYA NA
MAREKANI
Mheshimiwa Spika, kwa
ujumla, hali ya dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii katika mwaka wa fedha
2011/2012 imekuwa ya mashaka makubwa na hivyo kuathiri utulivu katika nchi
nyingi duniani. Hali hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi,
kijamii na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali
duniani.
Mheshimiwa Spika, eneo la
Ulaya limeathirika sana kiuchumi kutokana na madeni pamoja na mdororo wa uchumi
ulioikumba dunia katika kipindi cha mwaka 2008. Hali hii pia iliathiri kwa kiasi
kikubwa sarafu ya Euro, uchumi wa nchi zilizo katika ukanda wa sarafu hiyo
ujulikanao kama “Eurozone” pamoja na nchi ambazo zinafanya biashara na nchi za
Umoja wa Ulaya. Hali hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa Viongozi katika baadhi
ya nchi hizo kama vile; Ufaransa, Ugiriki, Italia, Hispania na Ireland kushindwa
katika Chaguzi Kuu au kushinikizwa kujiuzulu. Kwa upande wa Marekani nayo
ilikumbwa na misukosuko ya uchumi iliyosababishwa pia na mdororo wa uchumi wa
mwaka 2008. Hata hivyo, uchumi wake umeanza kutengemaa baada ya mdororo
huo.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na mdororo huo, nchi hizo zimelazimika kuchukua hatua kadhaa kunusuru uchumi wao
ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, kukopa zaidi ili kuwekeza katika sekta zenye
kutoa ajira na kupunguza kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania
kulingana na ahadi zao za awali. Kuna kila kiashiria kuwa uchumi wa Ulaya na
Marekani hautapata utulivu kwa muda mrefu na hivyo uwezo wao wa kutoa misaada
kupungua kadiri siku zinavyokwenda. Wizara na Balozi zetu za nje zinaendelea
kufuatilia kwa makini hali ya uchumi inavyoendelea duniani na kuishauri Serikali
kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na hali hiyo ili
kuimarisha uchumi wa Taifa letu na kuondokana na
utegemezi.
ASIA
Mashariki ya
Kati
Mheshimiwa Spika, eneo la
Mashariki ya Kati bado liko katika hali ya tahadhari. Nchini Syria hali
imeendelea kuwa tete kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo ambako waasi
wanapigana dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al – Assad tangu Januari mwaka 2011
na tayari wameshaingia kwenye Mji Mkuu wa Nchi hiyo. Umoja wa Mataifa na Jumuiya
ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zikiongozwa na Msuluhishi wa Mgogoro huo, Dkt.
Kofi Annan wameshindwa hadi sasa kufanikisha kusitishwa kwa mapigano. Aidha,
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika ambapo wajumbe wa kudumu
wenye kura ya turufu wametofautiana juu ya uamuzi wa kuchukua hatua za kijeshi
dhidi ya Serikali ya Syria. Tanzania inaunga mkono jitihada za Msuluhishi Kofi
Annan na kuwaomba wadau wote kutoingilia na kushinikiza matakwa yao nchini Syria
na badala yake kumuunga mkono Msuluhishi ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya
amani.
Mheshimiwa Spika, aidha,
kuendelea kukua kwa uhasama baina ya Iran na nchi za Magharibi kunaleta
changamoto ya ustawi wa amani katika ukanda huo. Uhasama huo unaletwa na hofu
kuwa nchi ya Iran inarutubisha madini ya urani yanayotumika kutengeneza silaha
za nyuklia. Tayari, Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani
ikishirikiana na nchi za Umoja wa Ulaya. Iran nayo imetishia kujibu mapigo kwa
kufunga mlango wa Bahari ya Hormuz ambao hupitisha asilimia ishirini 20 ya
mafuta yote ulimwenguni. Iwapo Iran itatekeleza uamuzi huo inaweza kuzusha vita
ambayo italeta madhara makubwa kwa uchumi wa dunia. Hali hii ya mtafaruku baina
ya Iran na nchi za Magharibi inaathiri pia mustakabali wa ukanda mzima wa
Mashariki ya Kati kwa kuwa Iran ina ushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi
nyingine zenye machafuko kama vile Syria. Kuendelea kwa migogoro na machafuko
katika ukanda wa Mashariki ya Kati kunaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia
kwa sababu asilimia kubwa ya mafuta yanayotumika duniani hutoka katika ukanda
huo. Pamoja na changamoto hizo, habari njema ni kwamba tayari Irani, Marekani,
Nchi za Ulaya pamoja na wadau wengine wameshakubaliana kurejea kwenye meza ya
mazungumzo na tayari mzunguko wa kwanza wa mazungumzo haya umeshafanyika. Imani
yetu kama nchi ni kwamba wahusika wote kwenye mazungumzo hayo wataonesha utashi
wa kweli wa kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo na si
vinginevyo.
Mashariki ya
Mbali
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Mashariki ya Mbali hali ni tulivu ukiachilia majanga ya asili
yaliyozikumba nchi za Japan, Ufilipino na Thailand na kusababisha athari za
kijamii na kiuchumi kwa baadhi ya sekta, hususan viwanda na makazi ya watu. Hali
ya kiusalama katika Peninsula ya Korea nayo imeonekana kutulia kidogo kufuatia
mabadiliko ya uongozi nchini Korea Kaskazini baada ya kifo cha Rais Kim Jong-il
aliyekuwa Rais wa Korea Kaskazini. Aidha, kwa upande wa Japan, hali ya kiuchumi
imeanza kuimarika hasa baada ya kukumbwa na tukio la Tsunami la mwaka 2011
lililoathiri kwa kiasi kikubwa kinu cha nyuklia cha Fukushima.
AFRIKA
Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwenye maeneo mengine duniani, Bara la Afrika nalo limeathiriwa na hali
ya mitikisiko ya aina mbalimbali duniani, ikiwemo ya kiuchumi, kisiasa na
kijamii. Maendeleo ya Bara hili yameendelea kukabiliwa na changamoto za
kiusalama, kisiasa, kiuchumi, kijamii, mabadiliko ya tabianchi, vitisho vya
ugaidi, uharamia wa baharini, kupanda kwa gharama za bidhaa muhimu kama vile
chakula, matatizo ya nishati ya umeme na kukosekana kwa ajira. Pamoja na masuala
hayo ya jumla, yapo baadhi ya masuala ambayo yanaweza yakaipambanua hali ya
Barani Afrika kwa sasa, hasa katika kipindi hiki cha miezi sita iliyopita.
Aidha, kuna masuala yanayozigusa baadhi ya nchi kama inavyoelezwa hapa
chini:
Uchaguzi wa Uongozi wa
Kamisheni ya Umoja wa Afrika
Mheshimiwa Spika, suala
kubwa lililotawala hali ya kidiplomasia Barani Afrika ndani ya mwaka wa fedha
2011/2012 ni uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Kama
itakavyokumbukwa, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika mwezi Januari, 2012 wakati wa
Mkutano wa 18 wa Umoja wa Afrika wa Wakuu wa Nchi na Serikali. Ushindani mkali
ulizuka kati ya wagombea wawili waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambao ni Bw.
Jean Ping wa Gabon, Mwenyekiti wa Kamisheni aliyemaliza muda wake na Bibi
Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afrika Kusini. Mvutano huo
ulisababisha Wakuu wa Nchi kushindwa kumchagua Mwenyekiti mpya wa Kamisheni hiyo
baada ya wagombea wote wawili kushindwa kufikia theluthi mbili za kura
zinazohitajika kisheria.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na kukosekana mshindi, Wakuu wa Nchi na Serikali waliamua kuahirisha uchaguzi
huo hadi kwenye mkutano wao wa 19 uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Julai
2012. Katika uchaguzi huo, Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma, Waziri wa Mambo ya Ndani
wa Afrika Kusini, alifanikiwa kuibuka mshindi. Hivyo, Mama Zuma anakuwa mwanamke
wa kwanza kuongoza Kamisheni hiyo. Ushindi wa Bi. Nkosazana Zuma ni ushindi wetu
pia kwa kuwa alikuwa ni mgombea wa SADC na Tanzania ilishiriki kikamilifu katika
kampeni zake.
Misri
Mheshimiwa Spika, hali ya
kisiasa nchini Misri ilishuhudiwa na matokeo ya machafuko yaliyopelekea
kuangushwa kwa utawala wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Mheshimiwa Hosni Mubarak.
Baada ya utawala wa Mpito ulioongozwa na Jeshi la nchi hiyo, hatimaye Chama
chenye mlengo wa kushoto cha Udugu wa Kiislam (Muslim Brotherhood) kimefanikiwa
kushinda uchaguzi huru uliofanyika Juni, 2012 kupitia mgombea wake Mheshmiwa
Dkt. Mohammed Mursi. Wizara yangu itashirikiana na Serikali mpya na kuendeleza
mahusiano mazuri baina ya nchi zetu mbili ikizingatiwa kuwa Misri ni mdau muhimu
katika kufanikisha matumizi ya rasilimali za Bonde la Mto Nile kwa maslahi ya
pande zote husika.
Mheshimiwa Spika, ni vyema
kutambua kuwa ingawa uchaguzi umefanyika bado hali ya kisiasa ni tete. Hii ni
kwa sababu licha ya kuwa Muslim Brotherhood wameshinda kwa kuwa na Wabunge wengi
Bungeni na kushika Ikulu, bado Jeshi la Misri linaendelea kushika hatamu za
uongozi. Jeshi limevunja Bunge na ndilo linalofanya maamuzi
makubwa.
Mheshimiwa Spika, ni
matumaini yetu kwamba hali hiyo tete ya kisiasa itatengemaa na hali kuwa nzuri.
Tanzania itashirikiana na Serikali mpya ya Misri ili kuendeleza na kudumisha
mahusiano yetu ya kirafiki na ya kihistoria.
Libya
Mheshimiwa Spika, baada ya
aliyekuwa Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Qaddafi kuuawa na Serikali yake
kupinduliwa na wapinzani wa NTC, Libya ilikumbwa na matatizo ya usalama. Mauaji
ya Walibya weusi yaliendelea. Hakukuwa na Serikali madhubuti, hakukuwa na Bunge
na wala hakukuwa na taasisi za Kidemokrasia.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
tulilaani mauaji ya Kiongozi huyo na tulisema kuwa tungalitambua Serikali ya NTC
tu iwapo ingalikuwa na viongozi wa kuchaguliwa, Bunge, Mahakama na uundwaji wa
Serikali ya mpito ambayo itajumuisha wadau kutoka vyama vyote vya
siasa.
Mheshimiwa Spika, uchaguzi
wa kwanza wa Kidemokrasia ulifanyika Libya mwezi Julai, 2012 kuchagua Wabunge
200. Waombaji 3,000 walijitokeza kugombea nafasi hizo. Pamoja na matatizo yote
ya kiusalama, wananchi milioni moja na laki nane waliweza kuchagua Wabunge wao
200 na Bunge linategemewa kumchagua Rais na Waziri Mkuu katika kipindi cha siku
30 baada ya uchaguzi. Zoezi hilo limekamilika. Aidha, Bunge limechagua kutoka
miongoni mwao Wabunge 60 wa kuunda Baraza la kuandika Katiba mpya, na Baraza
hilo limepewa siku 120 kuwakilisha mapendekezo ya Katiba kwenye Bunge lao.
Mchakato huo umeanza.
Mheshimiwa Spika, uongozi
wa Serikali ya Libya umekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Kikwete mjini Addis Ababa tarehe 15 Julai, 2012 na ukaeleza nia yake
ya kutuma ujumbe Tanzania kuja kutoa taarifa ya hali ya usalama na kisiasa na
kufufua rasmi mahusiano ya Kibalozi na Tanzania. Tunausubiri ujumbe huo na sisi
sasa tumeridhika na mchakato wa kujenga demokrasia unaoendelea nchini Libya.
Tanategemea kuletewa hati za Balozi mpya hivi karibuni na tutazipokea ili tuweze
kurejesha huduma za Kibalozi kama ilivyokuwa
mwanzo.
Somalia
Mheshimiwa Spika, hali ya
kisiasa na kiusalama nchini Somalia kwa sasa inatia matumaini ya kupatikana kwa
amani kutokana na juhudi za Umoja wa Afrika pamoja na washirika wake katika
kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo. Serikali ya Mpito ya
Somalia inatarajiwa kumaliza muda wake mwezi huu Agosti, 2012 na tayari rasimu
ya Katiba kwa ajili ya Serikali mpya imeandaliwa na inatarajiwa kupitiwa na
Baraza la Katiba linalojumuisha Wazee kutoka Koo zote tarehe 20 Agosti 2012.
Kupatikana kwa Serikali mpya ambayo uhalali wake utatokana na wananchi wenyewe
inatazamiwa kutoa fursa kwa Wasomali kujenga mustakabali mpya wa taifa
lao.
Mheshimiwa Spika, hali ya
usalama katika mji wa Mogadishu sasa ni ya kuridhisha kutokana na jitihada za
majeshi ya AMISOM na yale ya Kenya kudhibiti maeneo na miji muhimu iliyokuwa
ngome ya Al-Shabaab. Pamoja na kuwa wamedhibitiwa, Al-Shabaab wameendelea
kufanya matukio machache nchini Kenya ikiwa ni njia ya kulipiza kisasi. Hali
hiyo imeleta hofu kwa watalii na wageni kutoka nje wanaotembelea ukanda wa
Afrika Mashariki. Serikali zetu zinashirikiana kwa karibu katika kuimarisha
usalama dhidi ya vitendo vya uharamia vya Al-Shabaab. Vivyo hivyo, hali ya
usalama katika pwani ya Bahari ya Hindi na Ghuba ya Aden nayo inazidi kuimarika
na matukio ya uharamia kupungua kutokana na operesheni inayoendelea kati ya nchi
za pwani ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya. Katika mwaka
2011/12 peke yake, Jeshi la Wananchi liliweza kudhibiti matukio 27 ya uharamia.
Tuungane kulipongeza jeshi letu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kulinda mipaka ya
nchi yetu. Tunachukua jitihada za makusudi kulisaidia jeshi letu kupata vifaa
madhubuti kwa ajili ya ulinzi wa pwani yetu ambayo ina utajiri mkubwa wa gesi
asilia dhidi ya maharamia hawa.
Ukanda wa Maziwa
Makuu
Mheshimiwa Spika, hali ya
usalama mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ukanda wa Maziwa Makuu
kwa ujumla nayo iko tete hata baada ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo ulimalizika na Rais Joseph Kabila kutangazwa mshindi dhidi
ya mpinzani wake mkuu Bw. Etienne Tshisekedi. Mapigano yameripotiwa kutokea
hivi karibuni tarehe 6 Julai, 2012 Kaskazini Mashariki mwa DRC. Kikundi cha
waasi kijulikanacho kama M23 kinachosemekana kinaongozwa na Jenerali Bosco
Ntaganda anayesakwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa tuhuma za uhalifu wa kivita
kujibu tuhuma mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kinadaiwa
kuhusika na mapigano hayo. Kikundi hicho kinasadikiwa kuyateka na kuyadhibiti
baadhi ya maeneo ya Mashariki ya DRC yakiwemo Rutshuru, Bunagana na Kivu.
Majeshi ya Umoja wa Mataifa yameingilia kati kwa kutoa ulinzi katika mji wa
Goma, na tarehe 25 Julai, 2012 yalilazimika kutumia silaha kuwasambaratisha M23
kutoka kwenye maeneo wanayoyashikilia.
Mheshimiwa Spika, Wakuu wa
Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, katika kikao chao tarehe 14 Julai, 2012
waliuomba Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi wa kulinda amani kwa lengo la
kudhibiti usalama wa mpaka kati ya DRC na Rwanda ili kurejesha hali ya
kuaminiana baina ya nchi hizi mbili. Vilevile, walikubaliana kufufua mpango wa
usuluhishi uliokuwa chini ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania
na Mheshimiwa Olesegum Obasanjo, Rais Mstaafu wa Nigeria. Serikali ya Tanzania
inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya kisiasa na kiusalama nchini DRC kwa
kuwa machafuko hayo yanatuathiri kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama. Ni
kutokana na hali hiyo, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete anahudhuria Mkutano
wa Wakuu wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu utakaofanyika Kampala nchini Uganda
kesho tarehe 7 Agosti, 2012.
MASUALA YA USHIRIKIANO WA
KIKANDA
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara imetekeleza jukumu la uratibu wa
masuala ya ushirikiano wa kikanda kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika
shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi
zinazopakana na Bahari ya Hindi (IOR-ARC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za
Kusini mwa Afrika (SADC). Kwa kuwa eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki
limeelezewa vizuri na Waziri husika kwenye hotuba ya bajeti yake, niruhusu
nidurusu masuala machache yafuatayo:
Uenyekiti wa Tanzania
katika Kamati ya Utatu ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya
SADC
Mheshimiwa Spika, mnamo
mwezi Agosti, 2011 Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa,
Ulinzi na Usalama ya SADC. Kutokana na uteuzi huo, Tanzania imeingia katika
Kamati hiyo ya Utatu (Troika) ambayo kwa sasa inaongozwa na nchi ya Afrika
Kusini. Ifikapo tarehe 17 Agosti, 2012 Tanzania itatwaa rasmi Uenyekiti wa
Asasi hiyo muhimu ya SADC ambayo itaipa jukumu la kusimamia, kufuatilia na
kushiriki kwa kina katika masuala yote ya siasa, ulinzi na usalama ya Nchi za
SADC, hususan katika nchi za Madagascar na Zimbabwe ambazo ziko kwenye agenda ya
SADC Troika kwa sasa.
UTEKELEZAJI WA SERA YA
DIPLOMASIA YA UCHUMI NA MPANGO WA MAENDELEO WA MIAKA MITANO 2011/2012 –
2015/2016
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeendelea kupata mgao kidogo sana wa bajeti isiyokidhi mahitaji katika
mwaka wa fedha 2011/2012. Katika kipindi tajwa, Wizara yangu ilipata asilimia 44
tu ya Bajeti iliyoombwa. Bajeti ndogo tunayopewa imekuwa changamoto kubwa
katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kiwango kinachostahiki. Hata hivyo,
pamoja na mapungufu hayo, Wizara yangu kwa nafasi yake kama kiungo muhimu cha
nchi yetu na nchi za nje imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara, Idara na
Taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na sekta binafsi kuhakikisha kwamba nchi
yetu inafaidika kwa kadri iwezekanavyo na fursa mbalimbali zenye manufaa kwa
nchi yetu katika sekta za uchumi na jamii. Juhudi zetu katika kutafuta fursa
hizo zilizingatia vipaumbele katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano
2011/12 - 2015/16. Niruhusu nitumie fursa hii kueleza kwa uchache mchango wa
Wizara yangu kwenye sekta mbalimbali katika kufanikisha utekelezaji wa Mpango
huo wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Sekta ya Nishati na
Madini
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa sekta ya nishati, Wizara yangu kupitia Ubalozi wetu nchini China
imeshirikiana bega kwa bega na Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya
Fedha kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata mkopo wa Dola za Marekani bilioni
1.2 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi
Dar es salaam. Kama ilivyokwishaelezwa na Waziri wa Fedha hapa Bungeni, tayari
mkataba wa kupata fedha hizo umekwisainiwa na Mheshimiwa Philip Marmo, Balozi
wetu nchini China kwa niaba ya Serikali. Uzinduzi wa ujenzi wa Bomba hilo
ulifanyika tarehe 21 Julai, 2012 Mkoani Mtwara. Ujenzi wa bomba hilo utaleta
mapinduzi makubwa sana katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi. Bomba la
zamani lilikuwa dogo na lisilokidhi mahitaji ya kusafirisha kiasi kikubwa cha
gesi kwenda Dar es Salaam. Pindi ujenzi wa bomba hilo utakapokamilika fursa
nyingi za uchumi zitafunguka na kuimarika hasa zile zote zinazotumia
gesi.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu pia ilikuwa mstari wa mbele katika kuishawishi Tume ya Uhifadhi Duniani
(World Heritage Commission-WHC) na jumuiya ya kimataifa kukubali kurekebisha
mpaka wa Hifadhi ya Selous ili kuruhusu uchimbaji wa madini ya urani kufanyika
kusini mwa hifadhi hiyo. Juhudi zetu zimezaa matunda ambapo mwezi Juni, 2012
WHC wameridhia hoja zetu, jambo ambalo huwa si rahisi kufanywa na Tume hiyo.
Ushindi huu ni kielelezo cha nguvu ya ushawishi wetu na kuaminika kwetu duniani.
Matarajio yetu ni kwamba Kampuni ya Uranium One kutoka Urusi itaanza kazi ya
utafiti na hatimaye uchimbaji muda si mrefu mara baada ya kukamilisha taratibu
zingine na Wizara husika za Maliasili na Utalii na Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua hofu za msingi juu ya usalama wa uchimbaji wa madini hayo, Wizara yangu
imetoa pia msukumo katika upatikanaji wa wataalam na mafunzo na hivi karibuni
Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini imekwenda Nchini Australia
na Namibia kujifunza namna ya kuendesha miradi ya urani. Tanzania itatumia
nafasi yake ya Ujumbe wa Bodi ya Shirika la Atomiki Duniani (IAEA) kupata kila
aina ya utaalamu na uzoefu kuhakikisha kuwa uchimbaji wa madini hayo unafuata
taratibu na viwango vya kiusalama vinavyotolewa na
IAEA.
Mheshimiwa Spika, jitihada
za Wizara yangu kuufufua mradi wa umeme wa Stieglers Gorge nazo zinaanza kuzaa
matumaini. Kufuatia jitihada za Wizara yangu, Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa
Waziri Mkuu walifanya Ziara nchini Brazil ambapo agenda ya mradi wa Stieglers
Gorge ilipewa kipaumbele kikuu. Kutokana na ziara hizo, Kampuni ya Brazil ya
ODEBRECHT na Shirika la RUBADA kwa upande wa Tanzania wameshasaini Makubaliano
ya Awali (MoU) kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa uzalishaji wa umeme ambao
unakadiriwa utazalisha zaidi ya megawati 2,100 za umeme wa uhakika na wa bei
nafuu. Wizara yangu itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha Wataalam wanaotakiwa
kuja tena nchini kwa ajili kufanya mapitio ya taarifa ya environmental impact
assessment (EIA) na upembuzi yakinifu wanafanya hivyo ili mradi huo uweze kuanza
mara moja.
Sekta ya
Kilimo
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa sekta ya kilimo, Wizara yangu imeshirikiana kwa karibu na Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika katika kufanikisha upatikanaji wa teknolojia ya
umwagiliaji kutoka nchini India chini ya makubaliano ya Mpango wa Maendeleo wa
India-Afrika. Makubaliano mahsusi haya ya ushirikiano baina ya nchi zetu mbili
yanayotokana na ziara ya Rais wa India hapa nchini mapema mwezi Februari 2012.
Vilevile, Wizara yangu ilishiriki na kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya
Awali kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Jain Irrigation ya India mbele
ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kutekeleza kwa pamoja miradi ya
umwagiliaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Wizara yangu pia imeendelea
kuishawishi Serikali ya India kutupatia mkopo kwa ajili ya awamu ya pili ya
mradi wa Matrekta. Matumaini yetu ni kwamba juhudi hizo zitazaa matunda katika
mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeshiriki katika kufanikisha ushiriki wa nchi yetu katika Mkutano wa nchi
Tajiri na zenye Viwanda vikubwa duniani zinazojulikana kama G8 uliyofanyika
nchini Marekani. Mkutano huo ulikuwa na mafanikio makubwa kwa sekta ya kilimo
nchini baada ya mataifa hayo kutoa ahadi ya Dola za Marekani milioni 890. Aidha,
makampuni binafsi ya nchi hizo yaliahidi kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani
bilioni 3 katika sekta ya kilimo. Katika mwaka huu wa fedha, Wizara yangu
itaelekeza nguvu zake kuvutia wawekezaji kutoka nchi za Japan, Korea Kusini na
China kuwekeza katika Ukanda wa Kusini wa SAGCOT na vilevile kuanzisha kanda
nyinginezo za kilimo magharibi, kaskazini na mashariki mwa nchi yetu.
Sekta ya
Miundombinu
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Sekta ya Miundombinu, Wizara yangu imeendelea kushirikiana na Wizara
ya Ujenzi katika kutafuta misaada na mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu.
Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Wizara yangu kupitia Ubalozi wetu Japan,
iliweza kuishawishi Serikali ya Japan kugharamia upanuzi wa barabara ya
Gerezani na Mwenge-Morocco. Hivi sasa tunaendelea na juhudi za kuwashawishi
ndugu zetu wa Japan watusaidie kujenga barabara za juu (Flyovers) maeneo ya
Tazara. Wameonesha utayari wao kutusaidia. Vilevile, Wizara yangu inaendelea
kushirikiana na Wizara ya Ujenzi kupata wawekezaji wa ujenzi wa barabara ya njia
sita ya kutoka Ubungo hadi Chalinze chini ya mpango wa ushirikiano wa sekta
binafsi na sekta ya umma (PPP). Matumaini yetu ni kwamba ujenzi wa barabara hizi
utasaidia kupunguza tatizo sugu la msongamano wa magari jijini, Dar es Salaam na
yale yanayokwenda mikoani na nje ya nchi na hatimaye kupunguza madhara ya
kiuchumi yatokanayo na msongamano mkubwa wa
magari.
Sekta ya
Maji
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa sekta ya maji, Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na
Wizara ya Fedha tumeweza kuishawishi Serikali ya India kutupatia mkopo wa Dola
za Marekani milioni 178.25 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji katika miji ya Dar
es salaam na Pwani. Hivi sasa mchakato wa kupata fedha hizo umefikia hatua za
mwisho na bila shaka inatarajiwa mapema mwezi ujao Mkataba utasainiwa na
utekelezaji wa mradi huo kuanza. Vilevile, Wizara yangu kwa kushirikiana na
Wizara ya Fedha, Ujenzi, Nishati na Maji za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imefanikisha upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni
50 kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Uchumi ya Korea kwa ajili ya mradi wa kilimo
cha umwagiliaji Zanzibar.
Sekta ya
Viwanda
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea na juhudi za kuchangia katika sekta ya ukuaji wa viwanda. Kilicho
dhahiri ni kuwa, kwa hali ya uchumi wetu kwa sasa, viwanda vinavyohitajika
haraka ni vile vya msingi ambavyo vinatumia rasilimali za ndani, vinaongeza
thamani na vinatoa ajira nyingi. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba
katika mwaka huu wa fedha tutapata wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza nyuzi
za nguo kutoka Japan na China. Uwekezaji huu mkubwa sio tu utatengeneza ajira
kwa wananchi wengi, bali pia utawahakikishia wakulima wetu wa pamba soko la
uhakika kwani viwanda vyote hivi vikianza kufanya kazi, vitahitaji kiasi cha
tani laki mbili za pamba. Hivi sasa nchi yetu inazalisha tani laki moja tu.
Hivyo basi, ipo fursa kwa nchi yetu kuzalisha pamba kwa wingi zaidi kutokana na
kuwepo kwa soko la uhakika nchini. Aidha, uko uwezekano mkubwa kwa Serikali ya
Marekani kuendelea na Mpango wake wa AGOA ambapo bidhaa za nguo kutoka Afrika
ikiwemo Tanzania, zitaendelea kupewa upendeleo
maalum.
Sekta ya
Ajira
Mheshimiwa Spika, katika
kuwatafutia ajira Watanzania nje, Wizara ikishirikiana na mamlaka husika za
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imekamilisha mchakato wa makubaliano ya kusaini mkataba wa ajira na nchi ya
Qatar. Kwa sasa, Wizara yangu inatarajia kupokea ujumbe kutoka Qatar kuja hapa
nchini kusaini mkataba huo ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hizo nyingi
za ajira wakati Qatar ikijiandaa kuandaa Kombe la Dunia la mwaka 2022.
Halikadhalika, jitihada za Wizara yangu katika kuvutia misaada na uwekezaji
katika sekta za miundominu, zimechangia kuchochea uzalishaji wa ajira nyingi
nchini. Tunatambua changamoto ya ajira bado ni kubwa lakini tunaendelea na
jitihada hizi kwa kushirikiana na Sekta nyingine kadiri uwezo wetu wa kibajeti
utakavyoruhusu.
Sekta ya Elimu
Mheshimiwa Spika, mbali na
kuendelea kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi, Wizara yangu kwa kushirikiana
na Bunge lako Tukufu ilisimama kidete kupigania urejeshwaji wa fedha za ziada
kiasi cha pauni za Uingereza milioni 29.5, zilizojumuisha kiasi tulicholanguliwa
na kile kilichotolewa mlungula wakati wa ununuzi wa rada kutoka kampuni ya
Kiingereza inayojihusisha na uuzaji wa silaha (BAE). Kama nilivyoahidi katika
Bunge lako wakati wa kuwasilisha Kauli ya Serikali na baadae wakati
nikiwasilisha Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2011/2012, fedha hizo zote
zimerejeshwa Serikalini na sio kwenye Asasi za Kijamii. Kwa pamoja, jitihada
zetu zimewezesha kuipatia sekta ya elimu shilingi bilioni 90 kama ambavyo Bunge
hili limejulishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, sitakuwa
nimetenda haki nisipomshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa msimamo wake thabiti
na Mheshimiwa Spika kwa kuiunga mkono Serikali na kuteua Kamati ya Wabunge
ambayo imefanya kazi ya kutukuka kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa Serikalini.
Naomba nitambue mchango mahsusi wa Waheshimiwa Wabunge wote. Aidha, niwashukuru
pia Mhe. Balozi Peter Kalaghe, timu yake na watumishi wa Wizara waliosimama
kidete pamoja nasi kwenye suala hili lenye maslahi kwa taifa. Nimejifunza kuwa
imo ndani yetu nguvu kubwa ya umoja pale tunapoweka kando maslahi yetu finyu ya
vyama na itikadi na kusimamia maslahi mapana ya Taifa. Hii ndio Tanzania
ninayoijua na kujivunia, Tanzania yenye umoja na Tanzania yenye kuthubutu.
Tumeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa nchi yetu na historia itatupa tuzo njema
na kulikumbuka Bunge hili kwa kazi hiyo nzuri.
MASUALA MTAMBUKA
YALIYOTEKELEZWA NA WIZARA
Mradi wa Kiswahili kwenye
Umoja wa Afrika
Mheshimiwa Spika, lugha ya
Kiswahili imekuwa ikitumika tangu mwaka 2004 katika shughuli za Umoja wa Afrika
na Serikali yetu imekuwa ikigharamia wakalimani wa Kiswahili hadi mwaka 2008
ambapo Kamisheni ya Umoja wa Afrika ilichukua jukumu hilo. Serikali yetu
inaendelea kushawishi nchi wanachama walau thelathini na sita ambayo ni theluthi
mbili kuridhia Itifaki ya Marekebisho ya Mkataba wa Kuanzisha Umoja wa Afrika
(Protocol on the Amendments to the Constitutive Act of the African Union).
Kuanza kutumika kwa Itifaki hiyo kutawezesha lugha ya Kiswahili kutumika katika
shughuli za kila siku za Umoja wa Afrika.
Mheshimiwa Spika, sambamba
na juhudi hizo, mwezi Januari, 2012 Umoja wa Afrika umeanza kufundisha lugha ya
Kiswahili katika Kituo cha kufundishia Lugha cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Tayari wamekwishajisajili wanafunzi 15 chini ya Wakufunzi wawili wa kujitolea
kutoka Tanzania. Naomba nitambue mchango wao wa dhati na kuwapongeza kwa
uzalendo wao. Mimi binafsi nilipata fursa ya kuwatembelea na kuwatia moyo mwezi
Januari, 2012 wakati nikihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja
wa Afrika mjini Addis Ababa. Changamoto kubwa inayotukabili ni upatikanaji wa
fedha za kuendesha Kituo hicho na walimu wa kutosha wa kufundisha. Mpango wa
Serikali ni kutafuta fedha kwa ajili ya kuanzisha Kituo cha Utamaduni cha
Kitanzania jijini Addis Ababa kwa lengo la kukuza utamaduni wetu na Lugha ya
Kiswahili miongoni mwa jamii ya Wanadiplomasia na Watumishi wa Umoja wa Afrika.
Tukifanikiwa katika hili tutakuwa tumetengeneza fursa za ajira kwa Wakufunzi wa
Kiswahili pamoja na kupanua wigo wa fursa kwa Watanzania kufanya kazi katika
Taasisi za Umoja wa Afrika.
Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC)
Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, umekamilika kwa Asilimia 95 na
tunategemea kukabidhiwa mwezi Septemba 2012. Kituo hiki cha kisasa kinaweza
kuhodhi Mikutano minne kwa mara moja, yenye idadi ya watu 1,600. Kituo hiki
kitakuwa na huduma nyingine muhimu kama vile huduma za benki, afya, ukalimani na
migahawa. Kituo kimejengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri wa Watu wa China.
Sanjari na Kituo hiki, pia Serikali hiyo imetoa msaada wa magari madogo na
mabasi yapatayo 75 ambayo tayari yapo nchini kwa ajili ya kutoa huduma katika
Kituo hicho. Kuanza kufanya kazi kwa Kituo hicho, kutachochea ajira nyingi zaidi
za moja kwa moja na nyingine zinatarajiwa kutengenezwa katika sekta za
huduma.
Kusimamia Mikataba na
Makubaliano ya Kimataifa
Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia wajibu huu, Wizara imeshiriki kwenye majadiliano mbalimbali
yaliyopelekea uwekaji saini Makubaliano ya Mikataba mbalimbali katika kipindi
cha mwaka 2011/2012 kama ifuatavyo:
Mkataba wa mpaka wa Bahari
kati ya Tanzania na Comoro, ambao uliosainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini
Maputo – Msumbiji. Mkataba huu utahakikisha kuimarika kwa usalama wa mpaka wa
Bahari baina ya nchi hizi mbili;
Mkataba wa mpaka wa Bahari
kati ya Tanzania na Msumbiji ambao ulisainiwa tarehe 05 Desemba, 2011 jijini
Maputo – Msumbiji. Kama ilivyo kwa Mkataba baina ya Tanzania na Visiwa vya
Comoro, Mkataba huu utahakikisha usalama wa mpaka wa bahari baina ya nchi hizi
mbili unaimarika;
Muhtasari wa Makubaliano ya
Mkutano wa Pili juu ya Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari (EEZ) kati ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Visiwa vya Comoro na Serikali ya
Ushelisheli, uliosainiwa tarehe 07 Septemba, 2011 huko Port Louis, Mauritius.
Utekelezaji wa makubaliano haya ni muhimu ili kuwezesha nchi zote husika
kunufaika na ukanda wa kiuchumi wa Bahari ya
Hindi;
Makubaliano kati ya Kituo
cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) na Beijing Construction Engineering
Group Co. Ltd (BCEG) kuhusu ujenzi wa Mount Kilimanjaro International Convention
Centre ambayo yalisainiwa mwezi Agosti, 2011 mjini Arusha. Mkataba huu unatoa
fursa ya kujengwa kwa Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Jijini Arusha ambao
utaiingizia Serikali mapato na pia kuendelea kuitangaza Arusha na Tanzania kwa
ujumla kupitia Diplomasia ya Mikutano; na mwisho
Makubaliano ya Pamoja (MoU)
kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na China Petroleum
Technology and Development Corporation (CPTDC) mwezi Machi, 2012 kufuatia ziara
ya Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Li Jinzao
hapa nchini ili kuendeleza eneo hilo.
Mradi wa kuongeza Eneo la
Bahari Nje ya Ukanda wa Kiuchumi (Exclusive Economic Zone -
EEZ)
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu kupitia Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa - New York,
imekuwa ikiratibu na kushiriki katika utekelezaji wa Mradi wa kuongeza eneo la
Tanzania la Bahari nje ya Ukanda wa Kiuchumi. Wizara ikishirikiana na Kamati
ilioundwa kushughulikia suala hilo, imeendelea kufanya mawasiliano na Taasisi za
Umoja wa Mataifa zenye jukumu la kupitia Maandiko ya Miradi kama hii ya nchi
zote zilizofanikiwa kuongeza eneo la Bahari. Andiko la Mradi la Tanzania
liliwasilishwa Umoja wa Mataifa mwezi Januari, 2012 na Mheshimiwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Aidha, mwezi Agosti, 2012 Timu ya
wataalamu inatarajiwa kwenda kutetea Andiko hilo mbele ya “Commission on the
Limits of the Continental Shelf” (CLCS), inayoendelea na mkutano wake ulioanza
tarehe 30 Julai, 2012 na unaotarajiwa kumalizika tarehe 10 Agosti, 2012 huko New
York. Wizara imeendelea kushiriki katika maandalizi ili kufanikisha utetezi
unaotarajiwa.
Tume za Pamoja za Kudumu za
Ushirikiano
Mheshimiwa Spika, Tume za
Pamoja za Kudumu za Ushirikiano (JPCs) ni nyenzo muhimu sana katika ufanikishaji
wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. Ni katika Tume hizi mikataba ya msingi
husainiwa ambayo huweka mazingira kwa sekta binafsi kuweza kupata unafuu na
fursa katika nchi ambazo tuna Mikataba nazo. Kwa mfano, soko la tumbaku nchini
China ni kubwa zaidi kuliko lile la Marekani lakini wakulima wa Tanzania
wanashindwa kupenya katika soko hilo kutokana na kukosekana kwa mikataba ya aina
hii baina ya nchi zetu mbili. Kutokana na ufinyu wa bajeti, tumeshindwa kutumia
nyenzo hii vizuri kufungua na kufufua fursa za ushirikiano. Kwa kutambua umuhimu
huo na kuzingatia ufinyu wa bajeti uliopo, tumedhamiria katika mwaka wa fedha
2012/2013 kufanya mikutano ya JPC walau na nchi tatu kwa kuzingatia vipaumbele
vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 -
2015/2016.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe
kuwa, asili ya miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa katika sekta nyingi
nchini kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo inatokana na Tume za
Pamoja za Kudumu za Ushirikiano. Katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wizara
ilifanikisha makubaliano kuhusu uanzishwaji wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya
Ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Jamhuri ya Afrika Kusini. Makubaliano hayo yalifikiwa mwezi Julai, 2011 jijini
Pretoria – Afrika Kusini. Lengo la Makubaliano haya ni kuzidi kuimarisha
uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizi mbili katika nyanja mbalimbali hasa
za uchumi.
Mheshimiwa Spika, haya
niliyoyataja ni maeneo machache tu ambayo Wizara yangu imeyafanya katika
kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika
sekta za uchumi. Yako mengine mengi ambayo tumewezesha kufanyika katika kila
sekta nchini lakini kwa ufinyu wa muda siwezi kuyasema yote kwa muda nilionao.
Itoshe tu kuongelea haya machache kwa leo. Ninaliahidi Bunge lako Tukufu kwamba
tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuwezesha utekelezaji wa Mpango wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ya kwanza. Zipo fursa nyingi za ushirikiano
huko nje ya nchi ambazo nchi yetu inaweza kunufaika nazo. Tumejidhatiti
kunufaika na fursa zitokanazo na China-Afrika Forum (FOCAC), TICAD V, EU-Africa,
EBA, AGOA, Turkey-Africa, SADC, NEPAD, Tume za Kudumu za Ushirikiano baina ya
nchi yetu na mataifa mengine. Tunachohitaji ni kuwezeshwa zaidi ili tufanye
kazi hiyo kwa ufanisi zaidi.
NAFASI YA TANZANIA KATIKA
JUMUIYA ZA KIMATAIFA NA KIKANDA
Mheshimiwa Spika, bendera
ya Tanzania imeendelea kupepea vyema katika medani za Kimataifa kutokana na
uongozi mahiri wa Waasisi wa Taifa hili na uongozi uliopo kufuatia kazi kubwa na
nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watanzania katika Mashirika ya
Kimataifa na Kikanda. Wizara yangu imeendelea kufanya jitihada za makusudi
kuhakikisha Watanzania wengi wanajiunga na kufanya kazi kwenye Mashirika ya
Kimataifa. Aidha, Tanzania imeendelea pia kugombania na kuchukuwa nafasi za
uongozi kwenye mashirika mbalimbali ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, wakati wa
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika
Perth, Australia mwezi Oktoba 2011. Tanzania ilichaguliwa kuingia kwenye Kikosi
Kazi cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Ministerial
Action Group - CMAG) kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2013. CMAG ndiyo
chombo chenye jukumu la kusimamia misingi, sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya
ya Madola. Kikundi Kazi hicho kinaundwa na jumla ya nchi tisa kati ya nchi 54 za
Jumuiya hiyo. Kuchaguliwa kwa Tanzania kuingia kwenye Kikundi Kazi hicho
kumezidi kudhihirisha imani ya Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi yetu. Mbali na
kuleta sifa kubwa kwa Taifa letu, nafasi hii inaipa nchi yetu nguvu kubwa ya
ushawishi ndani ya Jumuiya ya Madola na pia nafasi ya kuingiza na kusimamia
maslahi yake kwenye Jumuiya hiyo.
Mheshimiwa Spika, napenda
pia kumpongeza Dkt. Agness L. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali
ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika la
Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuanzia mwezi Juni, 2012 hadi mwaka 2015. Nafasi hii
ni muhimu kwani kati ya nchi 189 ambazo ni wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani, nchi 37 tu ndio wanaingia kwenye Baraza Kuu la Shirika hilo. Dkt.
Kijazi anakuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuteuliwa kuwa
mjumbe wa Baraza Kuu la Shirika hilo.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
kupitia raia wake Prof. Chris Maina Peter, ilichaguliwa kwa kishindo kuwa Mjumbe
kwa kipindi cha miaka mitano kwenye Kamisheni ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa
Mataifa katika uchaguzi wa wajumbe wa Kamisheni hiyo uliofanyika mwezi Novemba,
2011 Mjini New York, Marekani. Prof. Maina ni Mtanzania wa pili kuiwakilisha
Tanzania kwenye Kamisheni hiyo, baada ya Mheshimiwa Balozi James L. Kateka
ambaye alikuwa Mjumbe kwenye Kamisheni hiyo kwa vipindi viwili vya miaka mitano
mitano (1997 - 2006). Balozi Kateka sasa ni Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya
Sheria za Bahari.
Mheshimiwa Spika, Majaji
wawili Watanzania – Jaji William Hussein Sekule na Jaji Joseph E. Chiondo
Masanche nao walichaguliwa kuwa Majaji wa Mahakama inayorithi shughuli za
iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) katika
uchaguzi uliofanyika New York, Marekani mwezi Desemba
2011.
Mheshimiwa Spika, kupitia
azimio namba 66/408 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwezi Novemba, 2011
lilimthibitisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Tanzania, Bw.
Ludovic Utouh pamoja na Ofisi yake kuwa kwenye Bodi ya Wakaguzi ya Umoja wa
Mataifa kuanzia Julai, 2012 kwa kipindi cha miaka sita. Mafanikio haya
yanatokana na umakini wa Wizara yangu kwa kufanya kampeni za uhakika hadi
kufanikisha kuchaguliwa.
Mheshimiwa Spika, kuanzia
mwezi Septemba, 2011 Tanzania imekuwa mjumbe katika Bodi ya Magavana ya Shirika
la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kwa kipindi cha 2011/2012. Kuwemo kwenye
Bodi hiyo, kunaipa nchi fursa ya kushiriki kwenye masuala nyeti na muhimu kama
vile kwenye majadiliano kuhusu mipango ya nyuklia ya baadhi ya nchi. Bodi hiyo
ina jukumu la kutathmini maombi ya nchi zinazoomba uanachama na kuthibitisha
viwango vya usalama. Aidha, Bodi ndiyo inayomteua Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ambaye
huthibitishwa na Mkutano Mkuu wa IAEA. Hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu hasa
ikizingatiwa kwamba Tanzania inayo malighafi ya urani.
Mheshimiwa Spika, niruhusu
nilitaarifu rasmi Bunge lako Tukufu kwamba Mtanzania mwenzetu, Dkt. Asha-Rose
Migiro, amemaliza kipindi chake kama Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kwa
hakika Dkt. Migiro amefanya kazi nzuri na kubwa iliyotukuka katika Umoja wa
Mataifa. Ameiletea sifa nchi yetu na Bara la Afrika kwa ujumla kutokana na
kumsaidia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban ki Moon. Kwa niaba ya
Watanzania wote, ninamshukuru kwa kutuwakilisha vizuri na ninampongeza sana na
kumkaribisha tena nyumbani ili aendelee kushirikiana na wananchi wenzake katika
ujenzi wa Taifa letu. Aidha, napenda pia, kupitia Bunge lako Tukufu kumpongeza
Dkt. Migiro kwa kuteuliwa tena kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika
masuala ya Ugonjwa wa UKIMWI Barani Afrika.
Mheshimiwa Spika, vile
vile, nchi yetu ilijipatia sifa kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa
Balozi Liberata Mulamula akiwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa Jumuiya ya Nchi
Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Mkuu. Balozi Mulamula aliratibu, aliisimamia na
kuongoza Jumuiya hiyo kwa mafanikio makubwa pamoja na changamoto nyingi
zilizokuwepo katika Ukanda wa Maziwa Makuu. Kutokana na kazi yake nzuri, ndio
maana Mheshimiwa Rais amemteua sasa kuwa Msaidizi wake Mwandamizi wa Masuala ya
Kidiplomasia.
MSIMAMO WA TANZANIA KATIKA
MASUALA MBALIMBALI
Mheshimiwa Spika, tumekuwa
tukishuhudia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii duniani kote
ambayo wakati mwingine yanahitaji nchi kuonesha msimamo wake kwa baadhi ya
masuala hayo. Moja ya sifa kubwa ambayo Mwasisi wa Taifa hili Hayati Mwalimu
Nyerere aliyotuachia ni kuweka misimamo kwenye misingi tunayoiamini kama Taifa.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania kama nchi huru imeweza kuwa na misimamo yake
kuhusiana na masuala hayo kama yanavyoelezewa hapa chini.
Suala la Mpaka Kati ya
Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa
Mheshimiwa Spika, lipo
tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka
kwenye Ziwa Nyasa. Tatizo lenyewe ni kwamba Malawi wanadai kuwa Ziwa lote
Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba
wa Heligoland uliowekwa saini tarehe 1 Julai
1890.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
kwa upande wetu tunasema kuwa mpaka wa kweli kati yetu na Malawi unapita
katikati ya Ziwa hivyo kufanya eneo lote la kaskazini mashariki ya Ziwa kati ya
Latitude digree 9° na digree 11° kuwa mali ya Tanzania kwa mujibu wa Mkataba huo
huo wa Heligoland (Ango-German Agreement) wa mwaka 1890 ambao ulikubali kuwa kwa
vile kuna maeneo ya mpaka ambayo hayana mantiki, pande zinazohusika zikutane na
kurekebisha kwa kuunda “Border Commissions”. Aidha, tunazo ramani ambazo
Waingereza wenyewe (ambao wakati huo walikuwa wakitawala Nyasaland na
Tanganyika) walikubaliana kurekebisha na hivyo kusogeza mpaka katikati kama
ulivyo mpaka kati ya Malawi na Msumbiji.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na tatizo hili, mwaka 2005 Marehemu Rais Bingu wa Mutharika, alimwandikia Rais
wa awamu ya tatu Mheshimiwa Mkapa akimtaka waunde Kamati ya kuliangalia tatizo
hilo na kulipatia ufumbuzi. Awamu ya Nne ikaendeleza kwa kuunda Kamati ya
Mawaziri wa Mambo ya Nje kuliangalia tatizo na kulitolea mapendekezo. Kama
zilivyokutana mwaka 2010, mwaka 2012 zilikutana tena ili kuendeleza mazungumzo
ya mwaka 2010 na pia kujadili matukio ya kuonekana kwa ndege ndogo ndogo za
utafiti wa mafuta na gesi kwenye Ziwa Nyasa zikitafiti hadi pwani ya Ziwa hilo
upande wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, baada ya
majadiliano makubwa kati yetu na Malawi, Serikali yetu iliwataka wenzetu wa
Serikali ya Malawi pamoja na kampuni za utafiti au uchimbaji kusitisha mara moja
shughuli zote za utafiti hadi majadiliano yatakapokamilika. Ni matumaini yetu
kuwa wenzetu wa Malawi wametuelewa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa
mgogoro huu mbele ya safari kutatuliwa na Msuluhishi badala ya sisi
wenyewe.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya
pili ya mgogoro bado iko mezani kwa majadiliano. Kufuatia maelekezo ya Marais
wa pande mbili, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wataalamu wetu wa masuala ya mipaka,
ulinzi na usalama tulikutana Dar es Salaam tarehe 27 Julai, 2012 kujadili kwa
kina mgogoro na kuupatia suluhu ya kudumu. Majadiliano yanaendelea vizuri na
tumekubaliana kuwa wakati tukiendelea na mazungumzo, nchi zote zijiepushe na
shughuli zozote kwenye Ziwa Nyasa ambazo zinaweza kutafsiriwa kuathiri maslahi
ya nchi mojawapo. Kwa makubaliano haya, naomba niwatoe hofu wananchi wa mikoa ya
Mbeya na Ruvuma kuhusu hali ya usalama mpakani mwa nchi yetu na Malawi. Chini ya
uongozi wa Serikali ya CCM, wananchi wa Tanzania daima watakuwa salama dhidi ya
tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama. Tumefanya hivyo tokea uhuru
na hatutachelea kufanya vinginevyo wakati wote tukiwa madarakani. Hili
limeelezewa katika Ibara ya Nane, aya ya 191 na 192 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM
ya mwaka 2010 - 2015.
Mgogoro wa Morocco na
Sahara Magharibi
Mheshimiwa Spika, Tanzania
ina uhusiano mkubwa na wa kihistoria na Jamhuri ya Sahara Magharibi.
Itakumbukwa kuwa nchi ya Sahara Magharibi inapakana na Morocco, Mauritania na
Algeria ilikuwa ni koloni la Hispania. Wakoloni hao waliondoka Sahara Magharibi
mwaka 1975 na wakati wananchi wanajiandaa kujitawala, ghafla nchi yao ikavamiwa
na nchi jirani za Mauritania na Morocco. Mauritania iliondoka na Morocco
ikaendelea kuikalia Sahara Magharibi tangu wakati huo yaani 1975 hadi sasa.
Wananchi wa Sahara Magharibi walianza kazi upya ya kudai uhuru wao kutoka kwa
jirani yao na Mwanachama wa OAU, Morocco. Mwaka 1976 Umoja wa Afrika uliamua
kuitambua Sahara Magharibi kama mwanachama wa OAU. Morocco ikajitoa kwenye
Umoja huo. Kwa kuwa Tanzania ilikuwa ndiyo Makao Makuu ya vyama vya Ukombozi
Barani Afrika, kuanzia mwaka 1963, ukombozi wa Sahara Magharibi ulikuwa ni moja
ya agenda yetu kuanzia wakati huo hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, msimamo
wa Tanzania kuhusu Sahara ya Magharibi, haujabadilika na upo pale pale.
Tunataka wananchi wa Sahara Magharibi waachwe waamue kupitia kura ya maoni
(referundum) iwapo wanataka kujitawala (independence) wenyewe au wanataka kuwa
chini ya Himaya ya utawala wa Morocco. Huo pia ndio msimamo wa AU na Umoja wa
Mataifa tangu mwaka 1992. Serikali ya Morocco imekataa kura ya maoni
(referendum) na badala yake wanataka Sahara Magharibi iwe sehemu ya Himaya ya
Morocco. Wamekataa kwa sababu wanajua kuwa wakikubali kura ya maoni kufanyika,
wananchi wa Sahara Magharibi watataka
kujitawala.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
inauomba Umoja wa Mataifa kuendelea na jitihada zake za usuluhishi na tunaitaka
Serikali ya Morocco kubadilika. Tupo tayari kuwa na mahusiano na Morocco bila
ya kuathiri msimamo wetu na Sahara Magharibi. Tunafanya hivyo kwa Israel na
Palestina.
Ziara za Viongozi
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeendelea kuratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nje ya nchi. Ziara
hizo zimekuwa na mafanikio na faida kubwa kwa nchi yetu, hasa katika kulinda na
kuendeleza maslahi ya kitaifa ya kiuchumi na kijamii, kukuza mahusiano ya
kidiplomasia na nchi mbali mbali, Mashirika ya Kimataifa na Kikanda, Kampuni za
Kimataifa na hata watu binafsi.
Mheshimiwa Spika, ili
kuhakikisha kwamba ziara hizo zinaendelea kuwa na tija pamoja na kupunguza
gharama katika mazingira ya kiuchumi tuliyonayo, kama alivyoelekeza Mheshimiwa
Rais, Wizara yangu imeanza kuchukua hatua mbalimbali kupunguza utegemezi wa
ziara hizo pekee katika kupata mafanikio mbalimbali, hususan ya kiuchumi.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni:
Kupunguza ukubwa wa ujumbe
katika misafara ya Viongozi Wakuu;
Kuwatumia Wawakilishi,
hususan Mawaziri katika safari mbalimbali hatua ambayo inapunguza gharama kwani
anaposafiri Waziri huongozana na wajumbe wachache
sana;
Kuelekeza nguvu katika
kuziimarisha Balozi zetu ikiwa ni pamoja na kufungua Balozi Ndogo katika maeneo
yenye maslahi ya kiuchumi kwa Taifa; na
Kutoa kipaumbele katika
kufungua Ofisi za Wawakilishi wa Heshima katika maeneo muhimu ambayo Tanzania
haina Uwakilishi.
Mheshimiwa Spika, katika
kudumisha mahusiano na nchi nyingine, nchi yetu imeendelea kutembelewa na wageni
mbalimbali katika ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri na Viongozi
wengine wa Kimataifa. Katika diplomasia, kutembelewa na wageni ni daraja muhimu
la kukuza mahusiano na pia ni kielelezo cha sera za nchi yako kukubalika na
Mataifa mengine yakiwemo Mashirika ya Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha uliopita wa 2011/2012 tulitembelewa na Marais kutoka Ivory Coast,
Somalia, Uganda, Liberia na Malawi. Vilevile, tulitembelewa na Makamu wa Rais
kutoka Burundi, Kenya, Zambia, Iran na Afrika ya Kusini. Wageni wengine
mashuhuri waliotembelea nchini ni pamoja na Prince Charles wa Uingereza na mkewe
Duchess of Cornwall Camilla Parker, Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia na Rais wa
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dkt. Donald Kaberuka na wengineo.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
imepokea idadi kubwa ya mawaziri kutoka nchi mbalimbali duniani kama vile China,
Uingereza, Japan, Sweden, Finland, Afrika ya Kusini, Korea ya Kusini, Korea ya
Kaskazini, Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu. Wizara inaendelea kutekeleza
mwongozo unaowataka viongozi wanaofanya ziara nchini Tanzania pia kutembelea
Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka fedha wa 2011/2012, Viongozi wafuatao walitembelea Zanzibar: Mwana wa
Malkia wa Uingereza, Prince Charles na Mkewe Camilla; Mfalme wa Ashanti wa
Ghana; Waziri wa Uingereza wa Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Finland wa
Maendeleo ya Afrika; Waziri wa Afya wa Finland; Waziri wa Afya wa Marekani; na
Waziri wa Afya wa Norway.
CHANGAMOTO MBALIMBALI
ZINAZOIKABILI WIZARA NA HATUA ZILIZOCHUKULIWA
Mheshimiwa Spika, kama
ilivyo kwa Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali, Wizara yangu imekumbwa
na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan kwa mwaka
wa fedha 2011/2012. Changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na
kuendelea kupungua kwa bajeti ya Wizara kila mwaka. Aidha, kuendelea kushuka
kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ambayo hutumiwa na Balozi
zetu nje nako kunasababisha bajeti kuendelea kutokukidhi mahitaji. Ufinyu wa
bajeti umesababisha Wizara na Balozi zetu kushindwa kutekeleza kwa vitendo
diplomasia ya uchumi. Kuendelea kupewa bajeti ndogo kumesababisha, pamoja na
matatizo mengine, madeni makubwa, wafanyakazi kutolipwa stahili zao na uchakavu
wa magari na majengo. Aidha, ufinyu wa bajeti umechangia kwa kiasi kikubwa kwa
Wizara kushindwa kuwarejesha nyumbani watumishi waliomaliza muda wao Balozini na
kuwapeleka wengine kutoka Makao Makuu. Kama nilivyosema hapo awali, Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalam (NUU) imetembelea Balozi zetu
mbalimbali na kujionea hali halisi. Ninaamini Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hiyo
watakuwa wasemaji wazuri wa matatizo yanayozikabili Balozi zetu kutokana na
ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha changamoto hizo zinapungua, Wizara yangu imepanga kuwa na majengo ya
vitega uchumi katika baadhi ya Balozi zetu ili kusaidia kuongeza mapato na
kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia pango katika maeneo hayo. Katika hatua
nyingine, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kuhusu uwezekano wa
kutumia utaratibu wa mikopo ya nyumba (Mortgage Financing) katika Balozi zetu
badala ya utaratibu wa sasa ambao una gharama kubwa kwa Serikali. Vile vile,
Wizara yangu katika mwaka huu wa fedha imepanga kuwasiliana na Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ili kuwaomba waruhusu Balozi zetu zitumie
utaratibu wa “hire and purchase” kununua vifaa mbalimbali kama vile magari ya
uwakilishi na hivyo, kupunguza gharama.
Mheshimiwa Spika, ninayo
kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Wizara yangu walioko Wizarani na
Ubalozini kwa uvumilivu na kujitolea kwa moyo wao wote katika mazingira haya
magumu. Wafanyakazi wameendelea kutekeleza wajibu wao kwa uaminifu na uadilifu
mkubwa sana. Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
tumekuwa tukiihusisha kwa karibu kuhusu changamoto hizi na wameshuhudia hali hii
kila walipopata fursa ya kutembelea Balozi zetu. Tunawashukuru kwa kuielewa hali
yetu halisi na kushirikiana nasi katika kushauri namna bora ya kuondokana na
changamoto hizo. Nasi tunauchukulia ushauri wao na ule wa Kambi ya Upinzani kwa
umakini mkubwa sana.
UTAWALA NA MAENDELEO YA
WATUMISHI WIZARANI NA KWENYE BALOZI ZETU
Mheshimiwa Spika, napenda
kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteua Mabalozi – kuiwakilisha nchi yetu huko
Kenya, Misri, Msumbiji, Uganda, Oman, Zambia, Italia, Ubelgiji na China. Vile
vile, aliwateua Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa na Naibu wake
pamoja na Wakurugenzi tisa katika Wizara yangu ambao wana hadhi ya Balozi.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa
Wizara yangu ina jumla ya watumishi 430 ambapo kati yao 249 wapo Makao Makuu ya
Wizara, 18 wapo ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar na 163 wapo kwenye Balozi zetu.
Kwa kipindi cha Julai, 2011 hadi Juni, 2012 jumla ya watumishi 50 walihudhuria
mafunzo ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, 17 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu
na watumishi 33 wamehudhuria mafunzo ya muda
mfupi.
Mheshimiwa Spika, kwa
kipindi hicho hicho, jumla ya watumishi 58 walipandishwa cheo baada ya
kutekeleza majukumu yao vizuri pamoja na kutimiza masharti ya Miundo ya Utumishi
inayosimamia kada zao. Vile vile, watumishi 51 walithibitishwa kazini baada ya
kumaliza muda wa mwaka mmoja wa majaribio baada ya kuajiriwa, na watumishi wanne
walibadilishwa vyeo baada ya kujiendeleza na kupata sifa za kada husika.
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu imeweka mkakati wa kuongeza idadi ya watumishi kutoka Zanzibar katika kada
ya Maafisa Mambo ya Nje kwa kuwapatia fursa Wanafunzi 18 kutoka Tanzania
Visiwani kuingia kwenye Chuo chetu cha Diplomasia. Dhamira ya Wizara ni kuona
kwamba, pindi watakapomaliza na kufaulu masomo hayo waweze kuajiriwa kwenye
Wizara yangu kulingana na nafasi za ajira mpya tutakazokuwa nazo.
TAASISI ZILIZO CHINI YA
WIZARA
Chuo Cha
Diplomasia
Mheshimiwa Spika, Wizara
imeendelea kukisaidia Chuo ili kiweze kutekeleza majukumu yake kama yalivyo
kwenye nia na madhumuni ya uanzishwaji wake. Lengo ni kukiwezesha Chuo kuendelea
kutoa mafunzo na kufanya utafiti katika masuala ya diplomasia, uhusiano wa
kimataifa, stratejia, usuluhishi wa migogoro, ujenzi wa amani, kutoa ushauri na
kuendesha mafunzo ya muda mfupi. Lengo tarajiwa ni kukifanya Chuo kuwa taasisi
bingwa ya elimu ya juu na ushauri katika nyanja hizo pamoja na kushirikiana na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika masuala ya utekelezaji
wa shughuli zake.
Mheshimiwa Spika, tatizo la
umiliki wa ardhi limemalizika baada ya Chuo kupatiwa Hati ya Umiliki wa eneo
lake. Kwa kuwa Chuo kinaendelea kupanuka ni wazi kuwa eneo la sasa kwa Chuo
haliwezi kukidhi mahitaji hayo. Hivyo, Serikali kupitia Wizara yangu imeendelea
kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo. Hadi sasa eneo la ekari 1,000 limeshapatikana.
Vile vile, tathmini ya kulipa fidia ya ardhi imekwishafanyika ambapo Serikali
inapaswa kulipa shilingi bilioni 2.5 kwa wananchi wa eneo la Buma lililopo
Wilayani Bagamoyo na Wizara inaendelea kufuatilia upatikanaji wa fedha hizo
kutoka kwa mamlaka husika.
Kituo Cha Kimataifa Cha
Mikutano Cha Arusha (AICC)
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Kituo kimeweza kukaribisha wastani wa
mikutano 64 kwa mwaka. Kati ya mikutano hii asilimia 30 ya mikutano ni ya
kimataifa na asilimia 70 ni ya kitaifa. Idadi hiyo ya mikutano imeweza kuleta
Arusha wageni wanaokadiriwa kufikia 44,578 kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha
ulioishia Juni, 2011 Kituo kiliweza kuwa mwenyeji wa mikutano ya kimataifa 15 na
ya kitaifa 47 iliyoingiza nchini wageni wanaokadiriwa kufikia
35,000.
Mheshimiwa Spika, naomba
kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea
kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa
kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni 2011. Kituo kilipata faida ghafi ya shilingi
milioni mia tano thelathini na moja, elfu mia sita na tano mia tatu na ishirini
(531,605,320/=) na kinaendelea kufanya shughuli zake kwa ufanisi na bila kuwa
tegemezi kwa Serikali Kuu. Katika kipindi cha mwaka 2012/2013, Kituo kimepanga
kuingiza mapato ya shilingi bilioni tisa, milioni mia sita arobaini na tano,
elfu mia tatu hamsini na tisa na mia saba (9,645,359,700/=) kutokana na vyanzo
vyake mbalimbali vya mapato na baada ya kutoa gharama za uendeshaji, Kituo
kinategemea kupata ziada ghafi ya shilingi milioni miatano ishirini na tano,
elfu mia moja hamsini na tisa, mia sita sitini na nne
(525,159,664./=).
Mheshimiwa Spika, Wizara
yangu inaendelea kufuatilia kuhusiana na kujengwa kwa Kituo kipya cha mikutano
mjini Arusha kitakachoitwa Mt. Kilimanjaro International Convention Centre
(MK-ICC). Mradi huu ni moja ya miradi itakayofadhiliwa na Serikali ya Watu wa
China kupitia benki yao ya Exim. Napenda kuipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa
Kituo, Menejimenti na wafanyakazi wote wa AICC na pia kuwatakia mafanikio mema
katika kazi zilizo mbele yao.
Mpango wa Kujitathmini kwa
Utawala Bora
Barani Afrika
(APRM)
Mheshimiwa Spika, kazi ya
tathmini ya utawala bora hapa nchini imeendelea kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Kwa kuwa Taarifa ya tathmini iliyokuwa imetayarishwa mwaka 2009 haikufanyiwa
uhakiki kama ilivyotarajiwa. taarifa hiyo ilihuishwa ili kurekebisha takwimu
mbalimbali zilizokuwa zimepitwa na wakati lakini pia kuakisi mabadiliko ya
kisiasa yaliyokuwa yametokea baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. APRM Tanzania
kwa kushauriana na Sekretarieti ya Afrika Kusini na Wizara, iliandaa pia Taarifa
mahsusi ya Zanzibar. Hatua hii ilitokana na maoni ya mara kwa mara ya wadau wa
Zanzibar hasa Makatibu Wakuu na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa ingawa
suala la APRM ni la Muungano, ingekuwa ni busara ikaandaliwa taarifa mahsusi ya
Zanzibar kwa nia ya kurahisisha utekelezaji wa changamoto zitakazobainishwa.
Taarifa hiyo nayo ilikamilishwa na kuwa sehemu ya Taarifa ya nchi iliyokuja
kufanyiwa tathmini na uhakiki na Timu ya Wataalamu wa kutoka nchi za Afrika
tarehe 2 hadi 23 Machi 2012.
Mheshimiwa Spika, wataalam
wa Country Review Mission wapatao 20 waliwasili nchini mwezi Machi 2012. Wakiwa
nchini walikutana na Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Serikali ya Muungano,
Makamu wa Kwanza wa Rais (SMZ), Makamu wa Pili wa Rais (SMZ), Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar, Makatibu
Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wawakilishi wa Serikali,
Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa, Wabunge, Viongozi wa Vyama vya
Siasa, Jumuiya ya Wafanya Biashara, Washirika wa Maendeleo pamoja na Asasi
zisizo za Kiserikali ili kupata maoni yao. Aidha, Wataalam hao, waligawanyika
katika makundi mawili tofauti walitembelea mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini
Pemba, Mtwara, Mbeya, Dodoma, Arusha, Kagera, Ruvuma na
Kigoma.
Mheshimiwa Spika, katika
mikutano mbalimbali iliyofanyika masuala yafuatayo yalijitokeza ambapo pamoja na
kuwepo kwa amani na utulivu, maeneo mengine yaliyoonekana kuwa ni tunu na
yanayopaswa kuenziwa ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, utaratibu wa
kurithishana madaraka kwa amani kila baada ya uchaguzi mkuu, Muafaka wa kisiasa
Zanzibar na kazi nzuri inayofanywa kwa uhuru na uwazi na Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Tanzania
inatarajia kufanyiwa tahmini kwenye Kikao cha nchi wenza zinazoshiriki katika
mchakato Januari, 2013 badala ya Julai, 2012 kutokana na Timu hiyo ya APRM
kutokuweza kukamilisha taarifa yao katika muda ambao ungetoa nafasi kwa Serikali
yetu kutoa majibu na kuyawasilisha kwenye Kikao cha APRM cha Tathmini cha Wakuu
wa Nchi kilichofanyika Julai, 2012 mjini Addis Ababa. Ninaipongeza Bodi ya
Uendeshaji ya APRM kwa kazi nzuri walioifanyia nchi yetu.
MAPATO NA MATUMIZI YA
WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2011/2012
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha wa 2011/2012 Wizara yangu ilipangiwa kutumia kiasi cha shilingi
bilioni mia moja ishirini na tano, mia moja na mbili milioni na mia nane sabini
na tano elfu (125,102,875,000/=). Kati ya fedha hizo shilingi bilioni themanini,
mia sita na mbili milioni na mia nane sabini na tano elfu (80,602,875,000/=) ni
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni arobaini na nne na milioni
mia tano (44,500,000,000/=) ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Aidha, katika
bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara (Recurrent Budget), shilingi bilioni
sabini na sita, mia tatu themanini na saba milioni na mia moja themanini na saba
elfu (76,387,187,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (OC) na bilioni
nne, mia mbili kumi na tano milioni na mia sita themanini na nane elfu
(4,215,688,000/=) ni kwa ajili ya mishahara.
Mheshimiwa Spika, Wizara
kupitia Balozi zake ilitegemea kukusanya kiasi cha shilingi bilioni kumi na nne,
mia nane sabini na mbili milioni na mia nne tisini na mbili elfu
(14,872,492,000/=). Hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2012 kiasi cha shilingi
bilioni kumi na tatu, mia nane hamsini na tatu milioni, mia nne arobaini na tisa
elfu na mia tano hamsini na tisa (13,853,449,559/=) ikiwa ni makusanyo ya
maduhuli balozini na Makao Makuu. Kiasi hiki cha fedha ni sawa na asilimia 93 ya
makusanyo ya fedha zote za maduhuli zilizokadiriwa kukusanywa balozini na Makao
Makuu kwa mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, hadi
kufikia tarehe 30 Juni, 2012 Wizara ilikuwa imepokea kutoka HAZINA jumla ya
shilingi bilioni mia moja na ishirini na tatu, milioni mia nane themanini na nne
elfu mia saba sabini na nane na mia saba themanini na saba (123,884,778,787/=)
ikiwa ni pungufu ya asilimia 0.97 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida, Mishahara,
pamoja na bajeti ya Maendeleo. Kiasi cha shilingi bilioni tisini na saba,
milioni mia mbili arobaini na moja elfu mia mbili thelathini na tisa, mia saba
themanini na saba (97,241,239,787/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida pamoja
na Mishahara ikionyesha ongezeko la asilimia 20.64 ya bajeti ya Wizara kwa
mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, ongezeko
hili limechangiwa na kuibuka kwa majukumu mbalimbali ya kitaifa ambayo awali
hayakupangiwa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti kama vile; Ujio wa Timu ya
Ukaguzi kuhusu Mpango wa Kujitathmini Wenyewe kuhusu Utawala Bora (APRM) kutoka
Makao Makuu ya Taasisi hiyo, Mchakato wa maandalizi pamoja na uzinduzi wa
Majadiliano ya Ubia Nadhifu (Smart Partnership Dialogue), Ujumbe na ushiriki wa
Tanzania katika Kikosi Kazi cha Kamati ya Mawaziri ya Jumuiya ya Madola
(CommonWealth Ministerial Action Group – CMAG), Mchakato wa ujumbe wa Tanzania
katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za kusini mwa
Afrika pamoja na Ujumbe wa Tanzania katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja
wa Afrika.
Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa bajeti ya Maendeleo, Wizara hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2012 imepokea
kutoka Hazina shilingi bilioni ishirini na sita, mia sita arobaini na tatu
milioni na mia tano thelathini na tisa elfu (26,643,539,000/=). Kiasi hiki ni
sawa na asilimia 59.87 ya bajeti yote ya Maendeleo iliyotengwa kwa Wizara kwa
mwaka wa fedha 2011/2012. Ikumbukwe kuwa Bajeti ya Maendeleo ya Wizara
ilipunguzwa kwa kiasi cha shilingi 16,898,098,757/= kutokana na hali ya mapato
ilivyodhihirika.
MALENGO YA WIZARA KATIKA
MWAKA WA FEDHA WA 2012/2013
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2012/2013, Wizara itaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi
kama yalivyoainishwa katika hotuba hii. Aidha, Wizara itaendelea kutekeleza
malengo yake iliyojiwekea kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka
2010-2015. Msisitizo utakuwa ushiriki wa Wizara katika utekelezaji wa Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano 2011/2012 – 2015/2016. Naomba kusisitiza na kukumbusha
Wizara nyingne kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara
mtambuka na hivyo inahusika na ufanikishaji wa miradi mingi inayotekelezwa na
Wizara, Idara na Taasisi nyingine mbalimbali za Serikali. Kama nilivyoeleza hapo
awali, Wizara yangu ina nafasi kubwa katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo
ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, kama
sehemu ya kuendeleza na kuhimiza njia mbadala za kukabiliana na changamoto
zinazotokana na bajeti inayoendelea kupungua kila mwaka, pamoja na mambo
mengine, Wizara inatarajia kufaya mambo
yafuatayo:
Kufungua Balozi Ndogo
katika miji ya Uturuki, Loss Angeles (LA), California, Lubumbashi na Guangzhou;
ambazo sanjari na kuendeshwa kwa gharama nafuu zinaweza kukusanya maduhuli mengi
kupitia utoaji wa viza na tozo, hivyo kuongeza idadi ya watalii na kukuza
biashara nje ya zile nchi tulizozoea (traditional allies) zilizoko Ulaya ambazo
uchumi wake unayumba kwa sasa;
Tume za Kudumu za Pamoja za
Ushirikiano (JPC) -Wizara inatarajia kuitisha mikutano ya Tume za Kudumu za
Pamoja za Ushirikiano angalau kwenye nchi tatu kwa lengo la kuzifufua tume hizo
na kupanua fursa za ushirikiano, hususan masoko ya bidhaa zinazozalishwa
nchini;
Watanzania Waishio
Ughaibuni (Diaspora) - Nafurahi kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa kufuatia
Mheshimiwa Rais kuteua Mkurugenzi wa Idara ya Diaspora mapema Mei, 2012 Wizara
yangu sasa ipo katika mchakato wa kuandaa Sera na Mpango wa Kitaifa kuhusu
masuala ya Diaspora ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwahusisha Watanzania
hao katika kuchangia maendeleo ya nchi yao. Hatua hii muhimu itasaidia kuainisha
wigo wa kisera, ushiriki wa wadau na majukumu ya Wizara, Idara na Taasisi
nyingine katika kufanikisha ushirikishwaji wa Watanzania waishio ughaibuni
kuchangia katika maendeleo ya taifa. Ni azma ya Wizara yangu kuona kuwa mchakato
huu unakamilika mapema ili kutoa mwongozo kwa wadau na kurahisisha uelewa wa
pamoja kuhusu mikakati bora ya kuwatambua na kuwashirikisha diaspora katika
kuchangia maendeleo ya nchi yao;
Majukumu ya Kimataifa -
Wizara imejipanga kutumia kikamilifu nafasi za Tanzania kimataifa katika kipindi
hiki zikiwemo uenyekiti wa asasi ya SADC organ Troika na ujumbe wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Afrika kukuza taswira ya nchi yetu nje na kukuza
ushirikiano wa Tanzania na nchi zilizoendelea ambazo ndizo zinafanya vizuri
kiuchumi kwa sasa;
Utatuzi wa Migogoro na
Uimarishaji wa Amani - Tanzania imeendelea kuwa nchi ya kutumainiwa katika
ulinzi na ujenzi amani Barani Afrika. Kumejitokeza haja kubwa ya uzoefu wetu
kutakiwa na nchi nyingine katika utatuzi wa migogoro na ujenzi wa amani katika
nchi zinazotoka katika migogoro. Serikali imeamua kujikita katika kutumia uzoefu
wetu na sifa hii katika kupanua maslahi ya nchi yetu kwa kuitikia fursa hizo.
Tunajipanga kutumia Wanadiplomasia wetu wastaafu na waliopo katika kutafuta
suluhu ya migogoro. Lengo ni baadae kuanzisha taasisi ya usuluhishi wa migogoro
katika Chuo chetu cha Diplomasia. Uwepo wa Taasisi hiyo nchini Tanzania itavuna
mikutano mingi na hivyo kuingizia nchi fedha za kigeni, kupanua sekta ya utalii
na kutoa fursa ya kujenga urafiki na kupanua maslahi yetu kwa nchi nyingi zaidi.
Tutatumia fursa zetu za kuwa Mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika na
Uenyekiti wa Asasi ya SADC kufanikisha azma hiyo;
na
Ulinzi wa Amani - sambamba
na mkakati huo, eneo la ulinzi wa amani (peacekeeping operations) ni eneo jipya
tunalotaka kulipa kipaumbele. Azma hiyo inakwenda sambamba na uanzishwaji wa
Chuo cha Ulinzi wa Amani (Peacekeeping School) nchini kwa ushirikiano wa Jeshi
la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Canada. Napenda kulifahamisha Bunge lako
Tukufu kuwa tayari Hati ya Awali ya Makubaliano (MoU) imesainiwa mwaka huu.
Kuanza kwa Chuo hicho kutatoa fursa kwa vijana wetu kujenga uwezo wa kushiriki
katika operesheni za Ulinzi wa Amani, vijana wetu wa jeshi kupata uzoefu na
mbinu mpya za kivita nje ya nchi, kuwezesha Watanzania wa fani mbalimbali kupata
ujuzi na utaalamu na kuweza kushiriki kwenye operesheni za AU na UN (Civilian
Peacekeeping Mission) ambako kwa sasa ushiriki wetu ni mdogo kutokana na kukosa
stadi za aina hii.
MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI KWA MWAKA 2012/2013
Mheshimiwa Spika, ili
kuweza kutekeleza kikamilifu kazi zilizotajwa hapo juu, Wizara yangu imepangiwa
kiasi cha shilingi bilioni tisini na nane, mia tatu thelathini na tisa milioni
na mia saba na saba elfu (98,339,707,000/=) kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kati
ya fedha hizo, shilingi bilioni themanini na moja, milioni mia sita themanini na
sita, mia tano na tatu elfu (81,686,503,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya
Kawaida, shilingi bilioni kumi na sita, mia sita hamsini na tatu milioni na mia
mbili na nne elfu (16,653,204,000/) ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo. Aidha,
jumla ya shilingi bilioni sabini na sita, mia tano arobaini milioni na mia tano
ishirini na moja elfu (76,540,521,000/=) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na
bilioni tano, mia moja arobaini na tano milioni na mia tisa themanini na mbili
elfu (5,145,982,000/=) ni kwa ajili ya Mishahara.
Mheshimiwa Spika, katika
bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara; shilingi bilioni moja, mia tano
arobaini na tisa milioni na mia tisa ishirini na tano elfu (1,549,925,000/=) ni
kwa ajili ya mchakato wa APRM, shilingi bilioni moja, mia tano na nne milioni,
mia tano sabini na nne elfu na mia nne sabini na nane (1,504,574,478/=) ni kwa
ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na shilingi bilioni
mbili, mia tano ishirini na sita milioni, mia tisa sabini na tatu elfu na mia
nne sitini na mbili (2,526,973,462/=) ni kwa ajili ya fedha za Mshahara na
Matumizi ya Kawaida ya Chuo cha Diplomasia.
Mheshimiwa Spika, aidha,
Wizara yangu, kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi
bilioni kumi na sita, milioni mia nane themanini na mbili elfu mia mbili
thelathini na moja, mia tatu na thelathini (16,882,231,330/=) kama maduhuli ya
Serikali. Kwa maana ya utekelezaji wa Bajeti, kiasi hiki cha maduhuli tayari
kimehesabiwa kama sehemu ya Matumizi ya Kawaida ya Bajeti ya Wizara
yangu.
Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment