Wednesday, August 1, 2012

RC Magalula asikitishwa na halmashauri za wilaya Mkoani Kagera kumfichia Mkaguzi nyaraka


Na Theonestina Juma, Karagwe
KAIMU Mkuu wa Mkoa Kagera, Bw. Magalula Said ameonesha kukerwa na tabia ya halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuficha nyaraka muhimu  na za malipo wakati Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa hesabu za serikali anapoenda kuwakagua na pindi wanapotakiwa kujibu hoja nyaraka hizo hupatikana.
Hayo yalibainika jana katika kikao cha kawaida cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo iliofanyika mjini Kayanga na kuhudhuriwa na Kaimu Mkuu wa Mkoa Kagera, Bw. Said ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita.
Alisema “kitendo cha kuficha nyaraka muhumu na  za malipo, pindi  Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali anapoenda kuwakagua, ni ugonjwa ambao unaonekana kushamiri kwa kasi katika halmashauri za wilaya za Mkoa Kagera ambapo wakitakiwa kujibu hoja nyaraka hizo hupatikana  baadae ni za kupikwa”
“Haiwezekani wakati mnakaguliwa nyaraka zikihitajika ili mdhibiti mkuu wa mahesabu ya serikali aweze kujidhihirisha na matumizi hayo ya fedha, hazionekani… lakini mkitakiwa kujibu hoja zinapatikana… zinatoka wapi.. hizi ndizo nyaraka tunazosema ni za kubuni… za kupikwa lazima muwe makini katika utunzaji wa nyaraka” alisema Bw. Said
Alisema uongozi wa halmashauri husika unatakiwa kuwachukulia hatua kali za kisheria watendaji wao wazembe wanaosababisha hasara na upotevu wa nyaraka ambazo ni mali ya umma.
Mkuu huyo alisema katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali, imebaini kuwepo kwa usimamizi mbovu wa nyaraka za malipo ya mishahara kwa watumishi.
Alisema kutokana na hali hiyo kila Mkuu wa idara kuhakikisha kuwa kabla ya mishahara kulipwa lazima apitie orodha ya watumishi wa kitengo chake ili kuepuka kulipa watumishi hewa wasistahili kulipwa.
Alisema katika taarifa ya CAG inaonesha kuwa mwaka 2010/2011 halmashauri za mkoa wa Kagera ulikuwa na hoja ya kutorejesha hazina mishahara isiyolipwa sh. milioni 46,420,054, ambapo pia ilibainika sh.milioni 123 zilitumilika mishahara watumishi wafu, waliofariki dunia, watoro na walioachiwa kazi.  
Hata hivyo, kwa upande wa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Bw. Bosko Nduguru alikiri  kuwepo kwa tatizo la uzembe wa utunzaji wa nyaraka muhimu na malipo na kuahidi kulifanyia kazi.
Aidha kwa upande wa Makamu Mwenyekiti wa Halmshauri hiyo, Bw. Wales Mashanda ambaye pia ni diwani wa Kata ya Nyaishozi alisema halmashauri hiyo inayo mpango wa kutenga jingo maalum kwa ajili ya kutunza nyaraka muhumu na kuweka utawala wake lengo kuondoa tatizo la upotevu wa nyaraka muhumu na malipo.
Alisema hatua hiyo wameiridhia baada ya kubaini kuwepo kwa upotevu wa nyaraka muhumu ambao uko ndani ya uwezo wao kuudhibiti.
Alisema kutakuwepo  na utaratibu wa kutumia ‘dispatch’ ya kuonesha taarifa ya  fulani imepelekwa kwa wapi na kupokelewa na nani lengo kuu likiwa ni kudhibiti unzaji mbovu wa nyaraka za halmashauri hiyo.
Kwa upande wa Kaimu Mkaguzi Mkazi wa Mkoa Kagera, Bw. Gerald Machumu aliridhia mpango wa halmashauri hiyo kutenga jengo maalum kwa ajili ya kutunza nyaraka muhumu na kuwahimiza jambo hilo litakuwa jema kama litatekelezwa kama baraza lilivyoazimia.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment