Mkuu wa Mkoa wa
Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe afunga rasmi maonesho ya NANE NANE
2012 Mkoani Kagera yaliyofanyika katika viwanja vya Kyakailabwa nje kidogo ya
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba yaliyoanza tarehe 1-8/08/2012.
Katika kufunga
maonesho hayo yaliyofana sana na kushirikisha wakulima mbalimbali kutoka katika
Halmashauri za Wilaya na Manispaa katika mkoa wa Kagera Mhe. Massawe aliyekuwa mgeni
rasmi alitembelea mabanda mabalimbali ya wakulima na biashara na kujionea
shughuli mbalimbali za wajasiliamali na kilimo.
Akiongea na wakulima
na wananchi waliohudhuria katika siku ya kilele cha NANE NANE 2012 mkoani
Kagera Mhe. Massawe alisistiza sana miradi ya kilimo kumilikiwa na wananchi
wenyewe pamoja na Halmashauri za Wilaya, aidha kushiriki katika vikao vya
kuibua miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
Ufugaji wa nyuki,
Mhe. Massawe alitoa wito kwa wakulima kuanza
ufugaji wa nyuki ili kujipatia kipato kutokana na kuuza asali. “Asali ya
mkoa wa Kagera ni asali bora duniani ambayo ina kiwango cha hali ya juu, pia
kimeanzishwa kiwanda cha kusindika asali mkoani Pwani, fugeni nyuki ina soko
kubwa duniani kote.” Aliwasistiza wakulima Mhe. Massawe.
Maagizo; Aidha Mhe.
Massawe alitoa agizo kwa Halmashauri za Wilaya kuhakikisha maonyesho yajayo ya
mwaka 2013 wanaletwa wakulima wengi ili waweze kujifunza kuliko kuwaleta
wachache wakati wakulima wengi wangependa kujifunza teknolojia na kilimo cha
kisasa chenye tija.
Pia Mhe. Massawe
aliiagiza kamati ya maandalizi ya NANE NANE 2012 Mkoa wa Kagera kuanzisha
maonyesho ya mifugo (wanyama) ili na sekta ya mifugo iweze kupata hamasa ya
kutoa elimu kwa wafugaji kujifunza kufuga kisasa kuondokana na ufugaji wa
kienyeji usiokuwa na tija.
Aidha katika
kumaliza hotuba yake Mhe. Massawe aliwasistiza wananchi kujiandaa na kuwa
tayari kuhesabiwa katika sensa itakayofanyika Agosti 26, 2012 na kuwaomba wale
wote wanaopotosha na kuhamasisha wananchi kutohesabiwa kuacha mara moja kwani zoezi hilo la sensa ni la kusaidia
serikali kupanga mipango ya maendeleo ya wananchi wake.
Maonesho ya NANE
NANE 2012 Mkoani Kagera yaliandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Kagera na Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi ilichukua kikombe kwa kuchukua nafasi
ya kwanza kiujumla kwenye maonyesho hayo.
Pia Mwenykiti
wa maonesho hayo Bw. Kagombora
alibainisha kuwa pamoja na maonesho hayo kufana lakini bado kuna changamoto
zinazoukabili uwanja wa Kyakailabwa ambazo ni
miundombinu ya Maji na Umeme ambazo bado zinatafutiwa ufumbuzi.
Imetolewa na:
Sylvester
Raphael
Afisa
Habari Mkoa,
Kagera
@2012
No comments:
Post a Comment