EFE. 5:25-26, 28-31 “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.
 Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.
 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”
Ni ukweli usiopingika kuwa mwanamke anapaswa kumtii mume wake. Wanawake wamekuwa wakifundishwa kila siku kuhusu utii kwa mume, tangia wakiwa wasichana. 

Wanawake wengi kwenye ndoa wanapata taabu sana maana waume zao wanashindwa kabisa kuwaonyesha upendo wakati mwingine kwa kutokujua au kwa makusudi. Hali hii imewafanya waonyeshee utii kwa kujilazimisha na kwa hali ngumu lakini kama mume angefahamu kuwa mke anastawi kwa kuonyeshwa upendo na akamuonyesha upendo ndoa nyingi sana zingepona na kuona furaha ya ndoa.
Biblia iko wazi sana kuhusu jambo hili na imelinganisha upendo wa mume kwa mkewe kama upendo wa Kristo na kanisa, na mume anapaswa ampende mkewe kama mwili wake mwenyewe.
Mume unawezaje kumpiga mke wako? Hivi kweli mtu unaweza kuupiga mwili wako mwenyewe? Unawezaje kumpuuza mke wako? Unafanya mambo bila kumshirikisha, hautambui mchango wake katika maendeleo na ustawi wa familia? Unawezaje kumtelekeza mke wako? Kumsimanga na hela ya matumizi? Kumuonyesha mke upendo sio udhaifu, sio kutawaliwa wala sio kujishusha bali ni kuonyesha jinsi gani wewe unasimama na neno la Mungu.

Mke ni msaidizi, mke ni ubavu wako, mke ni sehemu yako, mke ni mwili mmoja na wewe hivyo basi usimuone kama adui yako, mshindani wako, mtumwa wako wala mtu wa kukutumikia bali awe rafiki yako, mshauri wako, mtu wako wa karibu na sifa yako.