Saturday, March 8, 2014

Namna ya kupanga bajeti katika familia


Mwisho wa maelezo haya nitaweka fomu ya bajeti ambayo unaweza kui-download na kuiprint kwa matumizi yako ya nyumbani. Kuna hatua chache za kuweka bajeti, hapa kuna hizi tatu
Hatua ya Kwanza
Andika matumizi yote ya familia ya mwezi. Andika kwa mafungu maana bajeti itakuwa kwa mafungu na sio kitu kimoja kimoja maana tayari tuna orodha ya manunuzi (Kama bado hujaipata ipate hapa: HOUSEHOLD SHOPPING ). Andika fedha unayoipanga kuitumia kwa kila kipengele na uwe makini usije bajeti hela nyingi au kidogo kuliko kinachohitajika. Matumizi hayo yanaweza kuwa kama haya
a) Matumizi yasiyobadilika
  • Fungu la kumi
  • Kodi ya nyumba
  • Umeme
  • Maji
  • Mlinzi
  • Msaidizi wa kazi
b) Matumizi yanayobadilika
  • Chakula Ofisini
  • Mahitaji ya nyumbani
  • Matibabu
  • Akiba
  • Mahitaji binafsi
  • Nauli, mafuta ya gari
  • Mahitaji mengine
Hatua ya Pili
Ainisha mapato yote kwa mwezi katika familia yako. Andika mapato yote yanayoingia katika familia yako kwa mwezi (wewe na mume wako), mfano mishahara, faida za biashara, zawadi, ‘allowances’ n.k. Kwa mshahara weka kiasi unachopokea baada ya makato yote ili bajeti yako iwe halisia. Yajumlishe yote ili upate jumla ya mapato ya familia kwa mwezi.
Hatua ya Tatu
Linganisha mapato na matumizi. Kama mapato yote yanazidi matumizi basi bajeti hiyo uliyoiweka inakufaa bali kama matumizi yamezidi mapato kaa chini uangalie lipi sio la muhimu uondoe au upunguze fedha ulizozipanga. Ili uweze kuwa na bajeti yenye manufaa jaribu kuweka mgawanyo wa fedha kufuatana na umuhimu wa jambo husika. Kwa mfano:
Fungu la kumi 10% (kuna wanaotoa zaidi!)
Kodi ya nyumba 20%
Matumizi ya nyumbani  30%
Gharama za ofisini   15%
Binafsi   4%
Mavazi  3%
Burudani  3%
Matibabu  5%
Tahadhari  5%
Bajeti ya mavazi sio lazima itumike kila mwezi bali unaweza kuweka na kuitumia kila baada ya muda fulani. Fedha za matibabu tenga kila mwezi iwapo hazitatumika usitumie kwa shughuli nyingine bali endelea kuziweka. Akiba ni kwa ajili ya mipango ya baadaye na dharura kubwa, na ya tahadhari ni kwa ajili ya dharura ndogo yoyote.
Mithali 6:6-8 Ewe mvivu, mwendee mchwa,
zitafakari njia zake ukapate hekima!
Kwa maana yeye hana msimamizi,
wala mwangalizi, au mtawala,
lakini hujiwekea akiba wakati wa kiangazi
na hukusanya chakula chake wakati wa
mavuno.
Fomu Inapatikana hapa:: HOUSEHOLD MONTHLY BUDGET ::

No comments:

Post a Comment