Saturday, March 8, 2014

Umuhimu wa kuongeza mvuto kwenye chumba cha kulala


Chumba cha kulala ni mahali ambapo unapatumia wakati ukiwa umechoka na unahitaji utulivu na pumziko. Ni mahali ambapo unahitaji kuondoa ‘stress’ zote na kutuliza mwili na akili, vilevile ni mahali ambapo kwa wewe uliyeolewa unapata faragha ya kutosha kuwa na mume wako. Kutokana na umuhimu wa chumba cha kulala basi ni vyema kikawa na mvuto utakaokufanya ujisikie vyema kuwa ndani yake namuonekano wake uchangie katika kukuondolea uchovu na stress.
Haipendezi kuona chumba kikiwa kimejaa makaratasi, magazeti na vitabu kila mahali bila mpangilio mzuri. Weka vitabu na makaratasi yote mahali pamoja na kama unaweza kupata kabati na ukaviweka humo ili chumba kionekane nadhifu na sio kiwe kama maktaba. Nguo ziwe zimepangwa vizuri kabatini au sandukuni na zile chafu zikae mahali pake kwenye kapu la nguo chafu. Usiache nguo zinaning’inia kila mahali kwenye milango, madirisha, besele n.k maana inafanya chumba kiwe kimejaa na kuondoa mvuto.
Chumba cha kulala sio stoo hivyo haipendezi kuhifadhi vitu vya zamani chumbani kama viatu visivyovaliwa, nguo za watoto zisizovaliwa, miavuli, makoti ya mvua, toys za watoto n.k kama kuna ulazima wa kuhifadhi vitu hivi chumbani basi tafuta sanduku la bati na uviweke na kuhifadhi juu ya kabati au mvunguni ili kuondoa mlundikano wa vitu chumbani. Kipambe chumba chako kwa maua na mapazia ya kuvutia. usipambe tu sebule na jikoni na kusahau chumba cha kulala. Chumba kinaongezeka mvuto pale unapokipamba kwa maua na vessel nzuri, fremu za picha, mapazia mazuri na pia kapeti zuri la kuvutia. Unaweza weka picha yenu mkiwa honeymoon kwenye fremu na kuiweka mezani au ukutani na ikawa pambo zuri sana la chumbani kwenu.
Wekeza kenye mashuka mazuri na yenye kuvutia. Mashuka mazuri yanakufanya ujisikie vizuri unapokuwa chumbani na vilevile unapokuwa umelala. Hakikisha unayafanyia usafi mara kwa mara na kuyabadilisha badilisha sio kila siku mashuka  hayo hayo (kauka nikuvae). Wewe pia ni pambo mojawapo la chumba, hakikisha unakuwa na nguo nzuri za kulalia zenye kuvutia na kukufanya ujisikie vizuri na mwenye kuvutia. Hasa kwa wale walioolewa ni vyema kuzingatia hili na kuepuka kuvaa ma-tsheti ya zamani na madela kila siku unapoenda kulala au unapokuwa umejipumzisha chumbani.
Ubarikiwe

No comments:

Post a Comment