Ndugu zangu; Wanahabari;
Naomba
nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia
uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo. Vile vile, napenda kutoa
shukrani zangu za dhati kwa kukubali kuhudhuria mkutano huu ambao
kupitia kwenu nitapata fursa ya kuongea na wananchi kuhusu Maadhimisho
ya Siku ya Wanawake Duniani, tunayo adhimisha tarehe 8 Machi ya kila
mwaka. Kwa mwaka huu kama ilivyo kawaida yetu Watanzania tunaungana na
nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hii
Jumamosi tarehe 8 Machi, 2014.
CHIMBUKO LA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Ndugu wanahabari,
Vuguvugu la Siku ya Wanawake
lilianza mwanzoni mwa miaka ya 1900 kupitia kwa wanawake wafanyakazi wa
sekta ya viwanda nchini Marekani walioandamana kupinga mazingira duni ya
kazi zao, walilalamikia ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa
vitendo vya unyanyasaji katika ajira. Kutokana na hali hiyo, nchi ya
Marekani ilikubali kuwa na siku ya maadhimisho ya kitaifa ili kutafakari
masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wa wanawake.
Hatimaye Umoja wa Mataifa
ulipoanzishwa mwaka 1945; tarehe 8 Machi iliridhiwa kuwa Siku ya
Kimataifa ya Wanawake Duniani. Uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa ulitokana
na kukubali kwake kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake
yalihitaji msukumo maalumu na wa pekee.
MADHUMUNI YA MAADHIMISHO
Ndugu Wanahabari,
Madhumuni ya kuadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani ni kuwezesha jamii kupima utekelezaji wa maazimio,
matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa/ kikanda na
kitaifa zinazohusu masuala ya maendeleo ya jinsia na wanawake katika
kuhakikisha haki za wanawake kiuchumi, kijamii, na kisiasa zinapatikana
na zinalidwa.
Aidha, madhumuni mahususi ya
kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani ni kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu
wa kutambua na kuthamini uwezo na mchango mkubwa wa wanawake katika
kuleta maendeleo, kuelezea jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali
na wadau wengine katika kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kijamii ili
waweze kushiriki kikamilifu kujiletea maendeleo yao, familia zao na
Taifa kwa ujumla.
UTARATIBU WA MAADHIMISHO
Ndugu Wanahabari,
Tanzania ilianza kuadhimisha Siku
ya Wanawake Duniani mwaka 1996, maadhimisho yamekuwa yakiandaliwa
Kitaifa na katika ngazi ya mkoa. Aidha, nikumbushe kwamba katika
maadhimisho ya mwaka 2005 Serikali iliweka utaratibu wa kuandaa
Maadhimisho ya Kitaifa kila baada ya miaka minne; ili kutoa fursa maalum
kwa mikoa, wilaya na wadau wengine kupima mafanikio yaliyofikiwa katika
kumwendeleza mwanamke katika ngazi hizo kwa miaka hiyo na ifikapo mwaka
wa tano maadhimisho yafanyike kitaifa kwa kutoa taarifa ya utekelezaji
kwa nchi nzima.
Hivyo maadhimisho ya mwaka huu
2014 yanafanyika katika ngazi ya mkoa, na kila Mkoa umeandaa utaratibu
wa maadhimisho haya kwa kusisitiza Kaulimbiu ya kimataifa ambayo ni:
”CHOCHEA MABADILIKO KULETA USAWA WA KIJINSIA”. Ujumbe huu unasisitiza na
kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya jinsia katika
kupanga na kutekeleza mikakati na mipango ya maendeleo kwa kuzingatia
ushirikishwaji na ushiriki stahiki wa wanawake na wanaume katika
kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
JITIHADA ZA KULETA USAWA WA KIJINSIA KATIKA MAENEO YA KIPAUMBELE
Ndugu Wanahabari
Katika kuhakikisha kuwa kunakuwepo
na usawa wa kijinsia hapa nchini Serikali imekuwa ikichukua hatua za
utekelezaji katika maeneo yafuatayo:
Kuwapa wanawake uwezo wa kisheria
Ndugu Wanahabari,
Katika kuhakikisha kuwa wanawake
wanajengewa uwezo wa kisheria na kupata haki zao, sheria kadhaa
zimetungwa na nyingine kufanyiwa marekebisho ikiwemo Sheria ya Makosa ya
Kujamiiana yaani (SOSPA) ya mwaka 1998, ambayo imefanyiwa marekebisho
na kuhuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu; Sheria ya Ajira na
Mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo imetoa fursa sawa katika
ajira na likizo ya Uzazi pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009.
Kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi
Ndugu Wanahabari,
Kumekuwepo na ongezeko la ushiriki
wa wanawake katika ngazi mbalimbali za maamuzi. Marekebisho ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1995 yalifanywa na kuongeza
viti maalum kwa wanawake vilivyoongezwa kuwa asilimia 15 ya viti vyote
na kwa Zanzibar idadi ya nafasi za uwakilishi wa wanawake iliongezeka
hadi asilimia 20 mwaka 2000. Mabadiliko mengine ya Katiba ya mwaka 2005
yalifanya wabunge hao kufikia asilimia 30. Aidha, kwa mujibu wa Katiba
hiyo, Mheshimiwa Rais amepewa mamlaka kuteua wabunge 10. Kati ya hao,
wabunge watano ni lazima wawe wanawake. Kufuatia marekebisho hayo idadi
ya Wabunge wanawake kwa sasa ni asilimia 36.
Kuwawezesha wanawake kiuchumi
Ndugu Wanahabari,
Katika kuwawezesha wanawake
kiuchumi Serikali imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake unaotoa
mikopo ya kuanzisha biashara na shughuli nyingine za kiuchumi. Vilevile,
Serikali imeandaa Sera ya Mitaji midogo midogo ya Mwaka 2000, ambayo
imeweka mazingira mazuri kwa taasisi binafsi za kifedha ambazo nazo
hutoa mikopo kwa wanawake. Kwa mfano, Benki ya Wanawake Tanzania (TWB)
kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba, 2013 ilitoa mikopo kwa
wanawake 7395 yenye thamani ya shilingi bilioni 9.163 na pia walipatiwa
mafunzo ya ujasiriamali. Wanawake hao ni sawa na asilimia 79 ya wateja
wote waliopewa mikopo. Taasisi nyingine zinazotoa mikopo kwa wanawake ni
pamoja na PRIDE, FINCA, GATSBY-TANZANIA, SELF na kadhalika.
Kuwapa wanawake nafasi katika elimu na mafunzo
Ndugu Wanahabari,
Elimu ya Msingi: Haki ya kupata
elimu ni haki ya kibinadamu na yenye maana kubwa kwa mtu binafsi pamoja
na maendeleo ya kiuchumi. Katika eneo hili la elimu kumekuwepo na
mafanikio makubwa. Takwimu zinaonesha kuwapo na uwiano sawa (kwa tofauti
ya 0.99) kwa wasichana na wavulana wanaojiunga na elimu ya msingi, kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya kwa mwaka 2012. Ufundi . wenye umri kati ya miaka 7-13, kutoka asilimia 88.7 (mwaka 2006) hadi kufikia asilimia 89.6 (mwaka 2010).
Elimu ya Sekondari: Kwa upande wa
elimu ya sekondari idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule hizi
iliongezeka kutoka wanafunzi 675,672 mwaka 2006 hadi wanafunzi
1,638,699 mwaka 2010. Kwa mwaka 2006 wavulana walikuwa 358,128 sawa na
asilimia 53 na wasichana walikuwa 3317,544 sawa na asilimia 47. Mwaka
2010 kulikuwa na ongezeko ambapo wavulana walikuwa 910,171 sawa na
asilimia 56 na wasichana walikuwa 728,528 sawa na asilimia 44. Kwa
kiwango kikubwa uamuzi wa Serikali wa kuanziasha shule za sekondari za
kata na uhamasishaji ulisaidia kuongeza idadi ya wasichana na wavulana
waliojiunga na elimu ya sekondari.
Masomo ya Chuo Kikuu: Udahili wa
wanafunzi katika vyuo vikuu vya Serikali na Binafsi. Jumla ya wanafunzi
118,951, walidahiliwa mwaka 2009/2010. Kati yao wavulana walikuwa
76,935 sawa na asilimia 67.8 na wasichana 42,016 sawa na asilimia 32.2.
Aidha, Vyuo Vikuu vya binafsi vilidahili wasichana asilimia 40.5 na vile
vya Serikali vilidahili wasichana asilimia 33.4. Uanzishwaji wa shule
za sekondari za Kata kumewezesha wasichana wengi kuendelea na masomo ya
sekondari, hivyo kupunguza tatizo la kuolewa na kupata ujauzito katika
umri mdogo.
Ajira
Sera ya Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Ajira ya mwaka 2002 inabainisha haki sawa za ajira kwa wanawake
na wanaume. Aidha, sheria ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2002,
(ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2007) imetoa fursa sawa za ajira kati
ya wanawake na wanaume. Inapotokea kuwa mwanaume na mwanamke wanapata
alama sawa wakati wa usaili, mwanamke anapewa kipaumbele kupata nafasi
hiyo. Halikadhalika, Sheria ya Kazi na Mahusiano Kazini (2004) imetoa
fursa sawa kati ya wanawake na wanaume kuhusu haki zao za ajira, ikiwa
ni pamoja na kuwepo kwa likizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume.
Kupiga vita ukatili wa kijinsia.
Ndugu Wanahabari,
Katika kukabiliana na kuonekana
kwa tatizo la muda mrefu la unyanyasaji dhidi ya wanawake kutokana na
mila na desturi potofu hapa nchini, Serikali imeandaa, sera na mikakati
mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sera ya Maendeleo ya Jinsia na Wanawake
(2000) , Mkakati wa Kukabiliana na Ukatili wa Kijinsia (2001 – 2015)
2000) na Sheria ya Kujamiiana (SOSPA). Pia kwa kushirikiana na wadau
kampeni mbalimbali za kupiga vita ukatili wa kijinsia zimeendeshwa kwa
lengo la kuhamasisha jamii kuacha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana
na uhamasishaji huu unafanyika kwa ushirikiano wa karibu sana na vyombo
vya habari.
Mafunzo yanayohusu kuzuia ukatili
dhidi ya wanawake yanaendelea kutolewa kwa wasimamizi wa sheria,
wakiwamo askari polisi, Mahakimu wa Wilaya, Viongozi wa Vijiji na
Kamati za Ulinzi na usalama. Jeshi la Polisi limeanzisha madawati ya
Jinsia zaidi ya 417 na yanatoa huduma kwa wanaofanyiwa ukatili wa
kijinsia.
Serikali pia imeunda Kamati ya
kitaifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupata kutoa
ushauri kuhusu njia stahiki za kuzuia ukatili wa kijinsia katika ngazi
mbalimbali. Aidha Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa asasi
zisizokuwa za kiserikali kushiriki katika kupiga vita ukatili wa
kijinsia. Taasisi hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa elimu,
ushauri wa kisheria na matunzo kwa waathirika wa ukatili.Tunazishukuru
sana taasisi hizo na tutaendelea kushirikiana nazo kwa karibu.
Kuanzishwa kwa madawati ya jinsia
katika Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea, Wakala,
Sekretariati za Mikoa na Halmashauri kunasaidia sana katika kuingiza
masuala ya jinsia katika sekta husika. Aidha, baadhi ya Wizara na
Taasisi nyingine zimeunda kamati za jinsia ndani ya Sekta zao ili
kuharakisha uingizwaji wa masuala ya jinsia katika mipango ya kisekta,
pamoja na upatikanaji wa takwimu zilizoainishwa kijinsia.
Kwa umuhimu wa pekee kabisa naomba
nitoe shukrani za dhati kwa ninyi wanahabari kwa kazi kubwa mnayoifanya
ya kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya vitendo vya ukatili na
unyanyasaji wa watoto na wanawake kupitia vyombo vyenu. Ukisoma magazeti
au kusikiliza taarifa za habari na matukio kwa miaka hii hutakosa
kusikia taarifa za ukatili na hatua zinazochukuliwa na wadau ikiwemo
Serikali, NGOs na hata wananchi katika kukemea na kufikisha shauri
katika vyombo vya sheria.
Tunajua tatizo bado ni kubwa na
nawaomba wananchi wote na kupitia kwenu tungeze juhudi kifichua, kubaini
na kuchukua hatua kukomesha ukatili na kunyimwa haki kwa wanawake kwani
wanaofanyiwa hivi ni dada zetu, watoto wetu, mama zetu na wengine ni
bibi zetu. Serkali pekee haiwezi kushinda vita hii, kila mmoja ashiriki
kikamilifu na ndipo tutashinda.
HITIMISHO
Mwisho, napenda kurudia kuwaomba
wanahabari wote nchini kushirikiana na Serikali na wadau wengine
kutangaza na kuelimisha jamii mifano bora inayoonyesha jinsi gani
mwanamke na msichana akipewa fursa na kuwezeshwa na kuwekeza kwa mtoto
wa kike; hutoa mchango mkubwa sana kwa familia yake na taifa kwa ujumla.
Hili ndilo lengo kuu la kuadhimisha siku hii. Wanawake wapo zaidi ya
asilimia hamsini (50) ya watanzania wote kwa hiyo wakipata fursa na
kushirikishirikishwa ipasavyo katika shughuli za maendeleo mchango wao
utakuwa na manufaa makubwa katika Taifa letu.
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Wanawake Duniani hapo kesho kutwa tarehe 8 Machi, 2014
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment