Friday, January 4, 2013

TAARIFA YA MKUU WA MKOA WA KAGERA KWA UMMA KUHUSU MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE MKOANI KAGERA 2005 - 2012


Mkoa wa Kagera unaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo za serikali ya awamu ya nne chini ya Mhe. Dkt. Rais Jakaya Kikwete.  Mkoa umepata mafanikio mbalimbali katika sekta za uzalishaji, miundombinu, huduma za kiuchumi, uwezeshaji wananchi kiuchumi na huduma za jamii. Aidha, kuhakikisha shughuli za maendeleo kwa wananchi mkoa umekuwa unakabiliana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitafutiwa ufumbuzi ili kuinua hali ya kiuchumi na kijamii ya wananchi wa mkoa wa Kagera.
  Aidha, ifuatayo ni taarifa inayoonesha mafanikio yaliyokwisha patikana katika sekta zilizoainishwa hapo juu kwa kipindi cha miaka 2005 – 2012 kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 - 2015
 1.    KILIMO
Ili kuhakikisha sekta ya Kilimo inafanikiwa na kupiga hatua zaidi mkoa uliandaa mwongozo wake wa mapinduzi ya Kilimo ulioandaliwa Mei, 2007, na kuweka mikakati ya kutekeleza azimio la Kilimo Kwanza iliyokubalika kwenye mkutano wa wadau wa Kilimo Desemba, 2009.
Mafanikio:
·         Bajeti ya maendeleo ya Sekta ya Kilimo Mkoani Kagera imeongezeka kutoka sh. 1,590,724,374/= mwaka 2005 hadi sh. 8,648,435,000/= mwaka 2012; sawa na ongezeko la asilimia 443.7.
·         Eneo linalolimwa mazao ya biashara limeongezeka kutoka hekta 41,325 mwaka 2005 hadi hekta 68,201 mwaka 2012.  Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 65. 
·         Uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula umeongezeka kutoka tani 1,946,938 mwaka 2005 hadi tani 3,339,410 mwaka 2012; sawa na ongezeko la asilimia 71.5.
·         Uzalishaji wa mazao mbalimbali ya biashara umeongezeka kutoka tani 58,120 Mwaka 2005 hadi tani 660,110 mwaka 2012; sawa na ongezeko la asilimia 1,035.
·         Tija ya uzalishaji wa mazao mbalimbali imeongezeka kama ifuatavyo:
ü  Kahawa: kutoka tani 0.9 kwa hekta hadi tani 1.2 kwa hekta mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la aslimia 33.
 Pamba mbegu: kutoka tani 0.6 kwa hekta mwaka 2005 hadi tani 0.71 mwaka 2011/2012; sawa na ongezeko la asilimia 18.
ü  Muhogo: kutoka tani 3.7 kwa hekta hadi tani 4.1 kwa hekta mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la aslimia 11.
ü  Ndizi: kutoka tani 7.02 kwa hekta hadi tani 9.59 kwa hekta mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la aslimia 37.
ü  Mahindi: kutoka tani 1.3 kwa hekta hadi tani 2.7 kwa hekta mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la aslimia 200.
·         Matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 1,078 kwa mwaka 2005 hadi tani 4,766 mwaka 2012, sawa na ongezeko la asilimia 342.
·         Mbolea ya ruzuku imeongezeka kutoka tani 200 mwaka 2005 hadi tani 2,500* mwaka 2012 sawa na asilimia 1250.
·         Matumizi ya wanyamakazi maksai katika kilimo yameongezeka kutoka jozi 3,370 mwaka 2005 hadi jozi 5,578 mwaka 2012.
·         Matumizi ya mbegu bora yameongezeka kutoka tani 153 mwaka 2005 hadi tani 2,423 mwaka 2012.
·         Matumizi ya matrekta madogo (Power Tillers) yameongezeka kutoka 8 mwaka 2005 hadi 73 mwaka 2012.  Yanategemea kufika 272 ifikapo 2015.
·         Matumizi ya Matrekta makubwa yameongezeka kutoka 23 mwaka 2005 hadi 71 mwaka 2012.  Yanategemea kufika 103 ifikapo 2015.
·         Kilimo cha umwagiliaji kimeongezeka kutoka hekta 8,458 mwaka 2005 hadi hekta 19,014 mwaka 2012; ongezeko la asilimia 124.8. 
2.    MIFUGO
Mkoa unatekeleza Ibara ya 32 ya Ilani ya Uchaguzi ambayo ina mkakati wa kuongeza mchango wa mifugo katika Uchumi wa taifa na kipato kwa Wafugaji, msisitizo ukiwa ni ubora wa mifugo kuliko wingi.
Mafanikio – 2005 hadi 2012
·         Majosho yanayofanya kazi yameongezeka kutoka 18 mwaka 2005 hadi 64 mwaka 2012.
·         Wataalam wa uhamilishaji (Artificial Insemination) wameongezeka kutoka 10 mwaka 2005 hadi 36 mwaka 2012.
·         Madume bora yameongezeka kutoka 1,300 mwaka 2005 hadi 5,326 mwa 2012
·         Idadi ya ng’ombe waliohamilishwa imeongezeka kutoka 4,198 mwaka 2005 hadi 6,303 mwaka 2012.
·         Dawa za kuogesha mifugo zenye ruzuku ya Serikali zimeongezeka kutoka lita 0 mwaka 2005 hadi lita 31,444 mwaka 2012.
·         Elimu kupitia mashamba darasa ya ufugaji imeongezeka kutoka 37 mwaka 2005 hadi 310 mwaka 2012.
·         Wafugaji 10,068 wamepata mafunzo ya ufugaji bora.
·         Malambo ya maji yakunywesha mifugo yameongezeka kutoka 7 mwaka 2005 hadi 19 mwaka 2012
·         Ng’ombe wa maziwa wameongezeka kutoka 18,200 mwaka 2005 hadi 20,115 mwaka 2012.
·         Vifo vya ndama kabla ya kufikia mwaka mmoja kutokana na magonjwa yaenezwayo na kupe vimepungua kutoka asilimia 35 mwaka 2005 hadi asilimia 10 mwaka 2012.
·         Maeneo 77 yenye ukubwa wa Hekta 180,414.80 yametengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo.
3.    UVUVI
Serikali ya mkoa inahakikisha wananchi wa Kagera wanazitumia maliasili zilizomo katika maziwa na mito ili wavuvi watuimie fursa hizo kuinua hali zao na maisha.
Mafanikio:
·         Matumizi ya zana bora za uvuvi yameongezeka kutoka injini 1,077 mwaka 2005 hadi kufikia injini 1,942 mwaka 2012.
·         Uhamasishaji wa ufugaji wa samaki katika mabwawa  unaendelea kutolewa kwa wakulima na jumla ya mabwawa 202 yameanzishwa na kupandikizwa vifaranga 37,423 hadi kufikia mwezi Agosti, 2012.
·         Hatua zinachukuliwa kupambana na uvuvi haramu ni:-
Kuendesha doria mbalimbali zilizopelekea wavuvi haramu 324 kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.  Kutokana na doria hizo zana haramu zifuatazo zilikamatwa na kuteketezwa: kokoro 317, timba 469, makila 6,089, nyavu za dagaa 146, katuli 6, kwa ujumla zina thamani ya Tshs. 611,395,000/=.
·          Mafanikio yake ni kama ifuatavyo:-
Zoezi la uelimishaji wananchi limesaidia kusalimishwa kwa hiari zana haramu za uvuvi zifuatazo; kokoro 336, timba 642, makila 1,273, nyavu za dagaa 5, katuli 67, kwa ujumla zina thamani ya Tshs. 316,905,500/=.
4.    USHIRIKA / SACCOS
Sekta ya ushirika imetekeleza yafuatayo katika kuhakikisha wananchi mkoani kagera wanajiunga na ushirika na pia kunufaika nao;
Mafanikio:-
·         Idadi ya vyama vya Ushirika vya Akiba na mikopo (SACCOS) vimeongezeka kutoka vyama 232 mwaka 2005 hadi 330 Mwaka 2012.
·         Mtaji nao umeongezeka kutoka shilingi 2,136,220,690 mwaka 2005 hadi kufikia shilingi 9,633, 800,000 mwaka 2012; sawa na ongezeko la asilimia 351.
·         Katika kipindi hiki SACCOS zimepata jumla ya mikopo yenye thamani ya shilingi 13,977,000,000 hadi tarehe 30 Septemba, 2012.  Asilimia 82 ya mikopo imerejeshwa.
5.    MAZINGIRA
Juhudi za kuyatunza mazingira zimekuwepo ili kuhakikisha wananchi wa mkoa wa Kagera wanepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na uchafuzi au uharibifu wa mazingira. Aidha, Mkuu wa Mkoa amekuwa kiongozi katika kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kulindwa.
Mafanikio:-
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imekuwa mshindi wa tatu katika ngazi ya Halmashauri zote Tanzania na kupokea Tuzo hiyo Siku ya Mazingira Duniani tarehe 05 Juni, 2012 mjini Moshi
·         Uhifadhi wa vyanzo vya maji umeongezeka kutoka asilimia 54.2 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 68 mwaka 2012, sawa na asilimia 13.8
·         Matumizi ya mizinga ya kisasa yameongezeka kutoka mizinga 151,860 mwaka 2005 hadi mizinga 222,603 mwaka 2012.
·         Uzalishaji wa Asali umeongezeka toka kilogram 1,539,984 za 2005/2006 hadi kilogram 1,847980 mwaka 2011/2012, sawa na ongezeko la asilimia 20.
·         Mipaka ya vijiji 590 kati ya vijiji vyote 600 imepimwa.  Vijiji 52 vimekamilisha maandalizi bora ya ardhi.
·         Upandaji na Utunzaji miti umeongezeka toka miti 10,084,607 (91%) iliyopandwa na miti iliyostawi 9,712,535 (86%) kwa lengo la miti 11,000,000 kwa mwaka hadi mwaka 2011/2012 upandaji wa Miti, jumla ya miti 13,100,875 (105%) imepandwa na miti 11,220,328 (89.7%) kuota kati ya 12,500,000 ya lengo.  Hii ni sawa na ongezeko la 19% upandaji pamoja na ongezeko la 3.7% ya utunzaji wa miti hiyo.
·         Upimaji wa mipaka ya misitu unaendelea kufanyika na kwa sasa mwaka 2013 katika Msitu wa Hifadhi wa Taifa RUIGA uliopo katika Wilaya ya Muleba baada ya kukamilika kwa Msitu wa Hifadhi wa Taifa wa Biharamulo (hekta 134,000) na Nyantakara (hekta 25,000) mwaka 2011/2012 na upimaji wa Msitu wa Hifadhi wa Minziro (25,000) katika Wilaya ya Missenyi mwaka 2010/2011.
·         Kuanzia mwezi Julai, 2011 hadi Agosti, 2012 tumeendesha operationi, na doria za mara kwa mara ikiwa ni jitihada za kudhibiti uvamizi wa Hifadhi za wanyapori kama vile wahamiaji haramu kutoka ndani na nje ya nchi na kufanikiwa kukamata wafugaji mia tisini na sita (196) na ng’ombe wapato kumi na tano elfu mia nne na sitini na tano (15,465) wamekamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kukusanya fedha za adhabu shilingi 250,420,000/=.  Aidha, wafugaji wawili (2) wamefikishwa mahakamani na kuhukumiwa kulipa faini shilingi 400,000/= kila mmoja.
·         Vilevile, kuanzia mwezi Julai, 2011 hadi Agosti, 2012 operesheni na doria shirikishi (viongozi Serikali za vijiji, kata na askari polisi) zimefanyiak katika maeneo ya Hifadhi za Misitu na maeneo ya wazi ambapo technique ya Mobile Court imetumika na kutia hatiani watuhumiwa kumi na saba (17) kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili kwa mkosa mbalimbali kama ilivyoelekezwa na sheria ya misitu Na. 14 ya mwaka 2002.  Aidha, jumla ya shilingi 187,815,00/= zimekusanya kutokana na tozo na faini za kuvunja masharti ya sheria hiyo.

·         Kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2012 hadi tarhe 20 Novemba, 2012 Mkoa umefanya operationi maalum katika Wilaya za Karagwe, Muleba na Biharamulo na kukusanya fedha jumla ya shilingi 125,595,000/= kukamata silaha tatu aina ya Gobole pamoja na risasi tisa (9).


6.    ELIMU

Ibara ya 57 hadi 62 ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 inaelekeza maendeleo ya elimu bora katika ngazi zote na mkoa wa Kagera umeweza kupata mafanikio yafuatayo katiak sekta ya elimu

(i)            Elimu ya Awali:

·         Madarasa ya elimu ya awali yameongezeka kutoka 692 mwaka 2005 hadi 1,004 Mwaka 2012.

(ii)          Elimu ya Msingi:-

·         Asilimia ya uandikishaji darasa la kwanza imeongezeka kutoka asilimia 103 mwaka 2005 hadi asilimia 110 mwaka 2012

·         Idadi ya Wanafunzi darasa la I – VII imeongezeka kutoka 446,674 Mwaka 2005 hadi 535,280 mwaka 2012;

·         Idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 967 mwaka 2005 hadi 1,055 mwaka 2012.  Kati ya hizo shule za binafsi ni 49;

·         Idadi ya walimu imeongezeka kutoka 7,950 mwaka 2005 hadi 10,624 mwaka 2012;

·         Idadi ya nyumba za walimu imeongezeka kutoka 1,322 mwaka 2005 hadi 1,809 mwaka 2012.

·         Uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi (BPR) umeshuka kutoka 1:7 mwaka 2005 hadi 1:3 mwaka 2012;

·         Idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza imeongezeka kutoka asilimia 59.56 mwaka 2005 hadi asilimia 99.48 Mwaka 2010. Aidha, idadi ya wanafunzi waliofaulu 2012 ni asilimia 71.43 na asilimia 87.1 ya waliofaaulu wamechanguliwa kujiunga na kidato cha kwanza 2013.


(iii)         Elimu ya Sekondari:-

·         Idadi ya shule za serikali imeongezeka kutoka 66 mwaka 2005 hadi 240 mwaka 2012.

·         Idadi ya shule zisizo za serikali imeongezeka kutoka 21 mwaka 2005 hadi 47 mwaka 2012;

·         Shule za Sekondari za Serikali zenye “A Level” zimeongezeka kutoka 5 mwaka 2005 hadi 15 mwaka 2012.

·         Shule za Sekondari zisizo za Serikali zenye “A Level” zimeongezeka kutoka 7 mwaka 2005 hadi 13 mwaka 2012

·         Idadi ya walimu imeongezeka kutoka 750 mwaka 2005 hadi 1,972 mwaka 2012 sawa na asilimia 52 ya walimu wanaohitajika.  Kuna upungufu wa walimu 1,848 sawa na asilimia 48 ya mahitaji.

(iv)         Elimu ya Ualimu:-

·         Idadi ya vyuo vya ualimu imeongezeka kutoka 1 mwaka 2005 hadi 5 mwaka 2012.  Kati ya hivyo kimoja ni cha serikali, kimoja cha mtu binafsi na vitatu vinamilikiwa na madhehebu ya dini.

(v)          Elimu ya Ufundi:-

·         Kuna vyuo vya ufundi thelathini (30) mwaka 2012.  Kati ya hivyo saba (7) ni vya serikali, viwili ni vya Jumuia na ishirini na moja (21) ni vya Mashirika au Watu binafsi.

(vi)         Elimu ya Juu

Vyuo vikuu vimeongezeka kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kimoja (1) mwaka 2005 hadi vitatu (3) mwaka 2012. Mkoa unaendea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye elimu ya juu.



7.    AFYA

Mkoa umekuwa ukiweka juhudi kubwa za kuhakikisha unaboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kagera. Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya ni kama ifuatavyo;-

·      Zahanati zimeongezeka kutoka 206 mwaka 2005 hadi 268 mwaka 2011 kati ya hizo 31 ni za mashirika ya dini na 16 ni za watu binafsi;

·      Vituo vya afya vimeongezeka kutoka 21 mwaka 2005 hadi 30 mwaka 2011 ambapo 5 ni vya mashirika ya dini na sekta binafsi;

·      Hospitali zimeongezeka kutoka 13 mwaka 2005 hadi 15 mwaka 2011 kati ya hizo 12 ni za mashirika ya dini na sekta binafsi;

·      Kiwango cha akina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuhudumiwa na wahudumu wenye mafunzo kimeongezeka kutoka asilimia 52.1 mwaka 2005 hadi asilimia 71.9 mwaka 2011;

·      Vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua vimepungua kutoka 194/100,000 mwaka 2005 mpaka 89/100,000 mwaka 2011;

·            Chanjo ya watoto chini ya mwaka mmoja ni kama ifuatavyo:-
-    Polio (kutoka 97% mwaka 2005 hadi 89% mwaka 2011).
-    BCG (kutoka 97 % mwaka 2005 hadi 99% mwaka 2011).
-    DPT HB (kutoka 94% mwaka 2005 hadi 88.6% mwaka 2011)
-    MEASLE ( kutoka 93% mwaka 2005 hadi 89.7% mwaka 2011).
 -   Pepopunda kwa wajawazito kutoka 90.9% mwaka 2005 hadi 73% mwaka 2011)

·            Vifo vya watoto wachanga (IMR) chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka 110/1000 mwaka 2005 hadi 8/1000 mwaka 2011;

·            Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 182/1000 mwaka 2005 hadi 9/1000 mwaka 2011.

·            Jumla ya vyandarua 737,695 vimegawiwa kwa wananchi katika Mkoa wa Kagera.

·            Idadi ya watumishi wa afya.

Jedwali linaloonesha watumishi wa afya waliopo ikilinganishwa na mahitaji


Serikali
Mashirika ya Dini
Mashirika ya Umma
Binafsi
Jumla
Waliopo
1,007
474
25
42
1,548
Mahitaji
1,770
784
42
113
2,709
Upungufu
763
310
17
71
1,161
Asilimia ya upungufu
43
40
40
62
43%




8.         UKIMWI:
Serikali ya mkoa wa Kagera imeendelea na jitihada kubwa kuhakikisha inapunguza kiwango cha maambukizi kwa kuoa elimu mbalimbali zinazohusu ugonjwa wa UKIMWI pia kuhasisha wananchi kupima ili kujua hali zao.

·         Wagonjwa wanaopata matibabu ya dawa za “ARV” wameongezeka kutoka 598 mwaka 2005 hadi 11,256 mwaka 2012.

·         Aidha, wastani halisi wa maambukizi kimkoa kwa ujumla ni asilimia 3.4, hii inaonesha kwamba maambukizi yamepungua kutoka asilimia 3.7 mwaka 2009 hadi asilimia 3.4 mwaka 2010.

9.0  MAJI
Katika sekta ya maji serikali imekuwa ikitekeleza miradi mbalilmbali ya maji kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kwa kipindi cha kuanzia 2005 hadi 2012.

·         Idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama vijijini imeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 55.3 mwaka 2012.

·         Idadi ya Watu wanaopata huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Bukoba imeongezeka kutoka asilimia 63.4 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 76.5 mwaka 2012.

·         Idadi ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama katika miji ya Makao makuu ya Wilaya za Muleba, Biharamulo, Karagwe na Ngara imepanda kutoka asilimia 54.9 mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 65.8 mwaka 2012.
·         Mkoa ulipokea shilingi 11,325,051,892 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji tangu mwaka 2005, fedha hizo ni shilingi 7,978,061,655 kutoka programu ya maendeleo ya sekta ya maji, na shilingi 5,397,320,040 kutoka kwa wafadhili wengine wanaopeleka fedha moja kwa moja kwenye Halmashauri za Wilaya kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.  Aidha, wananchi walichangia shilingi 142,378,500 katika miradi hiyo ya maji.

·         Fedha hizo ziliwezesha vituo 1,806 vya kuchotea maji kutekelezwa na watu wapato 503,882 wamenufaika na huduma ya maji safi na salama kutokana na fedha zilizotolewa kwa kipindi hicho hadi kufikia Disemba, 2012.

Aidha, kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi kufikia 2012 miradi iliyotekelezwa ni kama ifuatavyo:-

·         Mwaka 2005 visima vifupi vilikuwa 1,119 kufikia 2012 vilikuwa 1,391 ongezeko la asilimia 28.8.

·         Visima virefu mwaka 2005 vilikuwa 257 kufikia 2012 vilifika 281 ongezeko la asilimia 40.5.

·         Miradi ya maji ya bomba mwaka 2005 ilikuwa 106 na kufikia 2012 ilikuwa 127 ongezeko la asilimia 19.9.

·         Aidha, vyanzo vya maji viliboreshwa kutoka vyanzo 804 mwaka 2005 hadi 942 mwaka 2012 ambalo ni ongezeko la asilimia 17.2.

·         Matenki ya kuvuna maji ya mvua mwaka 2005 yalikuwa 548 mwaka 2012 yalikuwa 777 ongezeko la asilimia 41.8.

·         Mwaka 2005 Mkoa ulikuwa na malambo/mabwawa 11 kufikia mwaka 2012 Mkoa ulikuwa na malambo/mabwawa 35 ongezeko la asilimia 218.2.

Serikali inaendelea na juhudi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya vijiji kumi (10) kwa kila Halmashauri ya wilaya Mkoani Kagera. Utekelezaji wa miradi hii uko kwenye hatua ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwenye vijiji 12 vya awali.  


10. MIUNDOMBINU

Mkoa wa Kagera mwaka 2005 ulikuwa na mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 4,200 kati ya hizo kilometa 1,841 zilikuwa zinasimamiwa na Wizara ya Miundombinu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) na kilometa 2,359 zikihudumiwa na Halmashauri za Wilaya na Manispaa.

Mkoa ndani ya miaka saba uliweza kuongeza kilometa 428.78 za lami kutoka km 353.45 hadi km 639.11, Changarawe kilometa 908.57 kutoka kilometa 1,737.5 hadi kilometa 2,646.07 na barabara za udongo zilizoongezeka ni kilometa 212.74 kutoka kilometa 1,842.05 hadi kilometa 2,054.7
Utekelezaji wa miradi mipya ya ujenzi wa barabara
Barabara ya Kyaka - Bugene (km 59.01m). Kazi ya ujenzi imekamilika kwa asilimia 20. Barabara ya Kagoma - Lusahunga (km 154) hadi sasa Km 142 za lami zimekamilika sawa na asilimia 92. Barabara ya Ushirombo – Lusahunga (Km 110) ujenzi wa Km 58 kwa kiwango cha lami umekamilika sawa na asilimia 55.

Aidha, kazi ya ujenzi wa daraja la Rusumo na ‘one stop boarder post ‘ eneo la Rusumo unaendelea ambapo kwa sasa Mkandarasi yupo kwenye hatua za upelekaji wa mitambo na vifaa na ujenzi wa jingo la one stop boarder post katika eneo la Mtukula umefikia hatua ya lipu.


11. NISHATI YA UMEME:

Wilaya zote saba (7) za mkoa wa Kagera zimepatiwa umeme.  Wilaya ya Missenyi, Bukoba, Muleba na Karagwe zinapata umeme wa megawati 5 kati ya megawati 9 kutoka nchini Uganda. Aidha, wilaya za Biharamulo na Ngara zinapata umeme wa jenereta zenye uwezo wa kilowati 450 kwa kila wilaya. Hata hivyo wilaya mpya ya Kyerwa bado haijapata huduma ya umeme.  Watapatiwa umeme baada ya mradi wa Murongo kukamilika.

·         Idadi ya vijiji 15 katika wilaya za Muleba, Karagwe na Bukoba vipo katika mpango wa kupatiwa umeme na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa gharama ya shilingi 1,097 milioni. Aidha, mradi wa umeme wa Murongo/ Kikagati wenye uwezo wa kutoa umeme wa megawati 16 umefikia katika hatua nzuri ya ujenzi baada ya kumpata mwekezaji. Mradi wa umeme wa Rusumo bado upo katika hatua ya upembuzi yakinifu (feasibility study) na inatarajiwa kuwa zitapatikana megawati 93 ambazo zitagawanywa kwa usawa kati ya nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

12.       WASTANI WA PATO LA MWANANCHI NA MKOA

Wastani wa pato la mkazi wa mkoa wa Kagera mwaka 2005 lilikuwa ni shilingi 291,644 na mwaka 2011 lilipanda mpaka shilingi 559,070. Aidha, pato la mkoa mwaka 2005 lilikuwa shilingi 643,605 na kufikia mwaka 2011 limepanda mpaka shilingi 1,488,061.


12. UKUSANYAJI WA MAPATO

 Mapato ya Ndani

Mwaka 2005/2006 Halmashauri za mkoa wa Kagera zilikusanya jumla ya shilingi 1,908,525,584 na mwaka 2010/2011 Halmashauri zilikusanya jumla ya shilingi 5,284,819,613.61 hivyo kufanya ongezeko la shilingi 3,376,294,029 ambazo ni sawa na asilimia 116.43. Aidha, katika mwaka wa fedha wa  2011/2012 Halmashauri zilijiwekea lengo la kukusanya shilingi 14,599,860,000, hadi Juni, 2012 fedha iliyokusanywa ni shilingi 8,518,089,764.44 sawa na asilimia 58.3 ya lengo. Kiwango hiki ni sawa na ongezeko la asilimia 346.3% ukilinganisha na makusanyo ya mwaka 2005/2006. 

Changamoto zinazokabili Mkoa na Halmashauri za Mkoa wa Kagera katika ukusanyaji wa Mapato ya Ndani

1.    Kuwapo kwa vyanzo vingi vikubwa vinavyokusanywa na Serikali Kuu.

2.    Baadhi ya mawakala wa kukusanya mapato wasio waaminifu hivyo kuzifanya Halmashauri kushindwa kukusanya mapato kulingana na masharti ya mikataba.

3.    Kuwepo kwa vyanzo vya mapato ambavyo kwa kiasi kikubwa msimu na hali ya hewa hivyo endapo hali ikibadilika malengo yaliyowekwa hayatimii.

4.    Serikali Kuu kuleta fedha pungufu ya bajeti kwenye fidia ya vyanzo vilivyofutwa.

5.    Serikali Kuu kutokuwa na takwimu halisi za vyanzo vilivyofutwa kwa ajili ya fidia.

6.    Watendaji wa Halmashauri kutokuwa na ubunifu wa vyanzo vipya.

7.    Baadhi ya Sheria Ndogo za ukusanyaji kutopitishwa kwa wakati ngazi ya Wizara.

8.    Baadhi ya Halmashauri kukosa takwimu sahihi na kamili za walipa kodi, ushuru na tozo mbalimbali za mapato.  Aidha, kutofanya tathmini ya vyanzo vya mapato.

9.    Ulegevu na uwezo mdogo wa watendaji katika kuwajibika, kusimamia na kukusanya mapato ya Halmashauri.

Bajeti inayotengwa na Serikali Kuu isiyokidhi mahitaji hivyo kukwamisha usimamizi na ufuatiliaji katika Halmashauri

·         Jinsi ya kuzikabili Changamoto

Ø  Kuhakikisha Halmashauri zinasimamia ipasavyo ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuendelea kubuni na kubaini vyanzo vipya vya mapato.

Ø  Kuhakikisha Halmashauri zinaimarisha Mipango ya Bajeti shirikishi.

Ø  Kuhakikisha Halmashauri zinakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu majukumu yao kwa wananchi.

Ø  Kuhakikisha Halmashauri zinasimamia mikataba inayofanyika kati ya Halmashauri na mamlaka na ukusanyaji mapato.  Aidha pale inapotokea ukusanyaji wa mikataba kuhakikisha mikataba hivyo inavunjwa.

Ø  Kuhakikisha Halmashauri zinachukua hatua stahiki za udhibiti wa matumizi mabaya ya rasilimali ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watumishi wanaojihusisha na ubadhilifu.

Ø  Kuhakikisha zoezi la ukaguzi wa miradi linaimarishwa katika Halmashauri ili miradi inayotekelezwa iwe na “value for money.

13. CHANGAMOTO ZINAZOUKABILI MKOA WA KAGERA
Mkoa wa Kagera unakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo:
1.    Kuwepo kwa biashara ya magendo ya kahawa katika maeneo ya mipaka ya Wilaya ya Karagwe na Missenyi na Nchi jirani ya Uganda kunasababisha Halmashauri kutokusanya ushuru wa zao hilo kwa kiwango ambacho kingestahili kukusanywa.  Pamoja na kufanyika kwa operesheni za kudhibiti biashara ya magendo kwa kipindi chote cha mavuno, bado kahawa inavushwa na hivyo kuathiri ukusanyaji wa ushuru wa zao hilo.

2.    Kufutwa kwa baadhi ya vyanzo vya mapato vya Halmashauri kwa ajili ya uwianishaji wa mapato ili kuondoa vyanzo ambavyo ni kero kwa wananchi. Hali hii imeendelea kuwa kikwazo pamoja na Serikali kutoa ruzuku ya fidia ya vyanzo vilivyofutwa bado kiwango kinachotolewa hakitoshelezi mahitaji, hivyo kuathiri ukusanyaji wa Halmashauri ikiwa ni pamoja na utoaji wa baadhi ya huduma.

3.    Kuchelewa kupitishwa kwa Sheria ndogo za Halmashauri za kukusanya mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani kumesababisha Halmashauri kuendelea kukusanya mapato yake kwa kiwango cha chini na maeneo mengine ya vyanzo vipya kutokusanywa.

4.    Kushuka kwa ushuru wa kahawa kutoka asilimia 5 hadi 3 kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011 bila Serikali kuongeza fidia ya vyanzo vilivyofutwa.

5.    Uhaba wa watumishi  wenye sifa na ujuzi hasa katika Sekta za Elimu, Afya, Kilimo na Mifugo.

6.    Uhaba wa vitendea kazi kama vile ofisi, nyumba za watumishi, magari na pikipiki unaosababisha utendaji wa shughuli za maendeleo pamoja na uratibu wa miradi ya maendeleo kuwa mgumu. Hadi sasa idara za Kilimo, Mifugo na Ushirika; na Uchumi, Mipango na Biashara pamoja na idara ya Maliasili na Mazingira hazina magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli mbalimbali Wilayani.

7.    Mwitikio mdogo wa jamii katika kuchangia miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa vituo vya Afya, Ujenzi na ukarabati wa majosho ya kuogeshea mifugo pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni.

8.    Kuongezeka kwa matukio ya mimba za utotoni hasa kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari.

9.    Kutokuwa na vyanzo vya maji  vya uhakika kwa ajili ya kuhudumia wakazi waliopo na matarajio ya ongezeko la ukuaji hasa katika maeneo ya Miji Midogo.

10. Mapato duni ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri

11. Uchelewashaji wa fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo toka Serikali
      kuu unaochangia miradi mingi kutokamilika kwa wakati

12. Bajeti ndogo inayotengwa katika shughuli za Maendeleo

13. Kilimo kisicho na tija kwa jamii hasa kutegemea kilimo cha mvua na jembe la Mkono. Tatizo hili pia limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa bei ndogo ya mazao.

14. Upungufu wa dawa na vifaa vya tiba vituoni na kutokuwa na huduma za
kutosha na kukua kwa kiwango cha UKIMWI katika baadhi ya maeneo hasa  maeneo ya uvuvi/visiwani

15. Gharama kubwa za matengenezo ya barabara kutokana na hali ya
kijiografia,mvua nyingi ,ukosefu wa mitambo imara ya kuimarisha barabara   na gharama kubwa ya kukodisha mitambo.

16. Uharibifu wa mazingira na uvamizi wa wafugaji katika maeneo ya misitu huko Burigi, Kimwani na Kasindaga.

17. Baadhi ya walipa kodi kukataa kulipa kodi na kusababishia Halmashauri kutokusanya mapato ya kutosheleza mahitaji (mfano; ushuru wa hotel na nyumba za kulala wageni, vibanda sokoni pamoja na ushuru wa samaki katika mwalo wa Goziba).

18. Kasi ndogo ya matumizi ya zana bora za kilimo pamoja na kuuza mazao yasiyosindikwa.

19. Milipuko ya magonjwa ya mazao na mifugo.  Ugonjwa wa Mnyauko Bakteria kwa zao la Migomba; Mnyauko Fuzari kwa zao la Kahawa na Magonjwa ya Batobato kali na Michirizi Kahawia kwa zao la Muhogo, pia ugonjwa wa miguu na midomo kwa ng’ombe na  ugonjwa wa mafua makali ya ndege.

20. Vijana kutoshiriki  kikamilifu katika shughuli za maendeleo Vijana wengi hawajihusishi na shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na ushirika. Wamekuwa wakipenda kufanya shughuli zinazoaminika kuwa zinawapatia kipato cha haraka na wakati mwingine zikiwa sio halali. Baadhi wamekuwa wakijihusisha na starehe wakati wa kazi hivyo kutokuwa wazalishaji.
UTATUZI WA CHANGAMOTO ZILIZOPO.
Mkoa unafanya jitihada mbalimbali za kutatua changamoto zilizopo kama ifuatavyo:
1.    Kuendelea kuimarisha doria na operesheni za kudhibiti biashara ya magendo ya kahawa kwenye maeneo ya mipaka na sehemu zote zinazotumiwa kuvushia kahawa.

2.    Kuendelea kuiomba Serikali Kuu kutoa fidia ya vyanzo vya mapato vilivyofutwa kwa kiwango kinacholingana na hali halisi ya ukusanyaji kama vyanzo hivyo vingekuwa vinaendelea kukusanywa.

3.    Serikali kutoa fedha za miradi kulingana na mpango Kazi na kwa wakati ili kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa inatekelezwa kwa wakati ili kuepuka ongezeko la gharama

4.    Mkoa kuendeleza mawasiliano na Serikali Kuu juu ya upatikanaji wa watumishi wenye sifa na ujuzi, pia kuweka utaratibu wa jinsi ya kuwawezesha kuendelea na utumishi katika mazingira ya Wilaya zilizoko pembezoni.

5.    Halmashauri zinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari kutokana na mapato ya vyanzo vya ndani pamoja na kuiomba Serikali Kuu kuruhusu ununuzi wa vyombo vya usafiri kutokana na fedha za usimamizi na uratibu wa miradi ya maendeleo Wilayani.

6.    Halmashauri zinaendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Madiwani.

7.    Halmashauri zinaendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kuboresha vile vilivyopo ili kuongeza vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri, vilevile sheria ndogo zimetungwa ili kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.

8.    Mkoa umeandaa mkakati wa utekelezaji wa kaulimbiu ya kilimo kwanza pamoja na kuwaelimisha wakulima juu ya mbinu bora za kilimo kama vile, matumizi sahihi ya mbolea, mbegu bora na kanuni za kilimo kwa ujumla ili kuleta mapinduzi ya kijani katika kilimo.

9.    Elimu ya utunzaji mazingira inaendelea kutolewa kwa jamii ili kuhifadhi mazingira pamoja na usambazaji wa sheria ndogo za uhifadhi wa mazingira sambamba na kuundwa kwa mabaraza ya mazingira kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Wilaya.

10. Kuendelea kutenga fedha na kutangaza zabuni za miradi mbalimbali katika vyombo vya habari ili kupata wazabuni wenye uwezo wa kutosha katika kutekeleza miradi.

11. Kuendelea kuelimisha jamii kuhusu kujikinga na maambukizi ya UKIMWI na kusaidia makundi tete hasa waishio katika visiwa.

12. Mkoa unashirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Maruku kukabiliana na magonjwa mbalimbali ya mimea na kuanzisha kilimo cha Kahawa na migomba aina ya Phia yenye kuzaa kwa wingi na muda mfupi.

13. Kuanzisha vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) vya Wavuvi ili kupata mikopo kwa urahisi na kuongeza kipato kwa Wavuvi.
14. Halmashauri zinashirikiana na jamii ili kuhakikisha sheria ndogo  za nguvu kazi zinafanya kazi kuwahamaisha vijana kujiunga na kuwekeza katika shughuli za uzalishaji.

15. Halmshauri kwa kushirikiana na Bodi ya kahawa wameendelea kuwahamasisha wanunuzi binafsi kuomba leseni na kununua kahawa ili kuongeza ushindani kwa vyama vya ushirika vya msingi.  Kwa upande wa wakulima wa miwa wameendelea kushirikiana na bodi ya sukari kuona jinsi ambavyo wanaweza kuongeza ushawishi kwa kiwanda kuongeza bei.


HALI YA ULINZI NA USALAMA:

Mkoa wa Kagera unapakana na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi. Kufuatia machafuko yaliyotokea katika nchi jirani za Rwanda na Burundi na mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994, mkoa ulipokea maelfu ya wakimbizi kutoka katika nchi hizo. Wakimbizi hao waliokuwa wanakadiriwa kufika 750,000 walipokelewa na kuishi katika kambi za wakimbizi katika wilaya za Karagwe, Ngara na Biharamulo.

Wakimbizi hao walichangia sana katika uharibifu wa mazingira hususan ukataji miti ovyo, uchomaji mkaa, kulima kwenye vyanzo vya maji na kuua wanyamapori.  Aidha, mifugo yao inapata malisho kwenye mapori ya akiba na hivyo kuharibu mazingira.  Hali ya ulinzi na usalama ilikuwa tete hadi wakimbizi hao waliporudi katika nchi zao.
Hivi sasa mkoa unao wakimbizi 35,000.

Kwa wastani hali ya ulinzi na usalama ni nzuri; inaendelea kuimarika kutokana na ushirikiano ulipo kati ya vyombo vya dola na wananchi hasa kupitia sera ya ulinzi shirikishi.
Katika maeneo mbalimbali hapa mkoani wananchi wameelimishwa njia za utoaji taarifa za uhalifu na hali hii imeleta mafanikio makubwa katika kudhibiti uhalifu.

Mikutano ya ujirani mwema ya mara kwa mara na nchi jirani zinazotuzunguka nayo imesaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao. Doria zinazofanyika mipakani nazo zimesaidia kuimarisha hali ya amani na utulivu.

Mkoa wa Kagera unapakana na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.  Mpaka kati ya Tanzania na nchi hizo una urefu wa km. 552.6 na ni “porous”.  Udhibiti wake ni mgumu.

 Kutokana na hali hiyo, yapo matatizo ya wahamiaji haramu hasa katika wilaya za Ngara, Karagwe na Missenyi.  Baadhi yao hujihusisha na vitendo vya uhalifu.



No comments:

Post a Comment