Monday, January 7, 2013

DC Kanyasu awapa siku 30 wafugaji haramu kuondoka katika wilaya yake

Na Ashura Jumapili, Kagera
 SERIKALI wilayani Ngara, Kagera imewapa siku 30 wafugaji wenye asili ya Rwanda kuondoka na ng’ombe wao kabla hatua za kuwasaka na kutaifisha mifugo yao hazijachukuliwa.
Kauli hiyo iliyolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu pamoja na kupiga marufuku viongozi wa vijiji wilayani humo kuwapatia ardhi wahamiaji wenye mifugo kutoka ndani na nje.
Akizungumza na wafugaji wakubwa na wadogo wa Kata za Kasulo na Rusumo pamoja na viongozi wa kata hizo, Mkuu huyo wa wilaya alisema tamko hilo limetolewa baada ya kuwepo baadhi ya wafugaji wenye asili ya Kinyarwanda na wengine kutoka wilaya za mikoa ya hapa nchini wanaoingia wilayani hapa na ng’ombe wengi na kuwanyanyasa wazalendo wenye ng’ombe wachache.
Kanyasu alisema ili kuhakikisha amani na utulivu vinapatikana ndani ya siku 30, viongozi wa vijiji kwa kata zote wilayani Ngara wafanye usajili upya wa kuwatambua wafugaji wageni toka nje ya vijiji vyao na mifugo waliyo nayo na kubaini walioingia kihalali na walioingia kinyume, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Alisema serikali inafanya kazi ya kulinda na kutetea haki za wananchi na sio kutetea kundi dogo lenye uwezo wa kifedha na kuwanyanyasa wachache, kwani kufanya hivyo ni kukiuka haki za binadamu.

No comments:

Post a Comment