Thursday, January 10, 2013

Ati hii ndiyo elimu ya bure wakati kumsajili mtoto Bukoba kuanza darasa la kwanza lazima mzazi alipe sh. 20,000

 

MWAKA wa masomo umeanza, wazazi wanapishana kila kona kuwanunulia watoto wao vifaa vya shule..
Ndiyo kwa shule za umma inajulikana kuwa elimu inatolewa bure…. Bureeeee… ahh nani kakuambia?
Aniambie nani si serikali ilishatangaza kuwa elimu ya shule ya msingi ni Bureeee… mhh…
Jamani si utani na si kweli kuwa serikali  inatoa elimu ya shule ya msingi bure…. Kimtazamo wangu…
Bora hata  miaka ya 1987…1990 ilijulikana kabisa kuwa watoto wanalipa ada.
Lakini hii ya sasa mtoto wa darasa la kwanza kuandikishwa lazima mzazi ateme 20,000 nimeshuhudia mimi.
Katika Manispaa ya Bukoba kumsajili mtoto lazima mzazi ateme sh.20,000 kama huna pisha waliokamilika wangie ndani ya ofisi ya Mkuu wa shule amsajili mwanae….. haya nimeyasikia kwa masikio yangu!
Ndiyo, katika baadhi ya shule za msingi, kuna michango kibao sawa na kulipa ada!.....
Kuna michango kama sweta la shule sh.10,000, fulana sh.6,000, ulinzi wa shule  sh.3,000.Katika hili sijui wanalinda nini hawa walinzi labda kama ni miti, kwani mimi huwa siwaoni hao walinzi hao, muhuri wa shule sh.500  hapa kweli yule  mtu masikini atamudu hali hii?.... sijui… labda Rais wangu anajua.
Chakushangaza katika michango hiyo, hawatoi risiti, wewe mzazi unatema fedha mwalimu yeye anazikunja tu mkononi tena mkali kama nini….!
Siku ya jumatatu masomo yalipoanza, nilifika katika shule mojawapo mjini Bukoba, nilikutana wazazi walioleta watoto wao kuanza darasa la kwanza wakilumbana na Mkuu wa shule na baadhi ya walimu jambo lililonilazimu nitulie kidogo niulizie kulikoni?
Ahhh … huwezi amini, kumbe fulana, masweta ni biashara ya walimu bwana!
Kwani kulikuwa na sehemu kama mbili za kuuza masweta  hayo, sehemu ya kwanza ni ndani ya ofisi ya Mkuu wa shule ambapo masweta yaliuzwa sh. 10,000 na hapa mzazi unatema hizo, mtoto anavalishwa papo hapo!
Sehemu ya pili ilikuwa ni nje  ambapo walimu wengi walikuwa wamekaa wakigawana vitabu kuukuu hivi!
Kwa hao walimu kuna mwalimu wa kike ambaye inasemekana kuwa kila mwaka huwa anapewa zabuni ya kuleta masweta, yeye alikuwa anawauzia wazazi kwa sh.8,000!
Cha ajabu kule penye unafuuuuuu ndiko walikimbilia wazazi wengi, kumbe ulimchukiza mwalimu wa kiume ambaye naye alipata hako ka zabuni kwa mwaka huu…. Matokeo yake watoto waliovaa masweta ya bei nafuu walikuwa wakifukuzwa kwa madai kuwa masweta hayo hayatambuliwi hapo shuleni wakati yako sawa na yale yanayouzwa ndani ya ofisi ya Mkuu wa shule…. Mmhhh!
Baada ya kunyaka hayo machache ilinibidi niondoke niendelee na shughuli zangu za kutafuta mkate wa kila siku sijui mwishowe walimalizana vipi!
Hata hivyo kwa sasa katika manispaa ya Bukoba sare za shule bei haishikiki, sketi zilizoshonwa maarufu kama korija sh.5,000 shati  la korija 5,000 ukiingia soko kuu mitaani ni sh. 3,500 lakini ndugu yangu yalivyoshonwa mtoto akishiba tumbo liko nje tu vishikizo havifungi! Ndiyo hayo maisha bora kwa kila Mtanzania.

No comments:

Post a Comment