Friday, January 18, 2013

Jamani mapenzi... mume atenganisha kichwa na kiwili wili cha mkewe naye ajimaliza kwa kujitia kitanzi... kisa wivu


Na Theonestina Juma, Kagera

MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha Kikuku kata Kagoma wilayani Muleba, Bi. Bilivu Festo (40) ameuawa kikatili kwa kucharangwa mapanga na kisha kutenganishwa kichwa na kiwili wili chake na mume Bw. Festo Kibenderena (56) na kisha kujinyonga kwa kile kinachodaiwa kuwa ni  kutokana na wivu wa mapenzi.
Tukio hilo la aina yake ambalo limethibitishwa na Kamanda wa polisi Mkoa Kagera, Pillip Kalangi limetokea Januari 16, mwaka huu saa 12 jioni katika kijiji cha Kikuku kata ya Kagoma wilayani Muleba.
Chanzo cha mauji hayo ya kikatili kimeelezwa kuwa ni kutokana na wivu wa mapenzi ambapo, Bw. Festo alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa anasaliti ndoa yao kwa anatembea nje na wanaume wengine.
Wanandoa hao ambao wameacha watoto wanne, siku ya tukio, baba yao aliwatoa nyumbani kwenda kupalilia njugu shambani ambapo kumbe alikuwa na lengo lake la kutaka kumuua mkewe.
Katika tukiko hilo ambalo wakati likitokea, mtu wa kwanza kutoa taarifa  ya mauaji hayo ni mtoto mdogo wa miaka mitatu ambaye ni mwanaye Bw. Godwin Kasebano anayemwita Bw. Festo kuwa baba mdogo wake.
Imeelezwa kuwa siku hiyo ya tukio, mtoto huyo ambaye jina lake halijapatikana alienda kwa baba yake na kumwelezea jambo kwa ishara ambapo Bw. Godwin alienda kwa baba yake mdogo huyo na kukuta Bi.Bilivu akiwa ameuawa kwa kucharangwa mapanga sehemu mbali mbali za mwili na kutenganishwa kichwa na kiwiwili huku baba yake mdogo huyo akiwa ametoweka nyumbani hapo.
Hata hivyo, baada ya mauaji hayo, watu walianza kumsaka Bw. Festo bila mafaniko hadi  kesho yake Januari 17, mwaka huu  saa 7 mchana baada ya maziko ya mkewe ndipo aligundulika kuwa amejinyonga.
Mwili wa Bw. Festo  ulikutwa juu ya mti wa mwembe ukiwa unaning’inia akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba aina ya manila  ng’ambo wa pili na watu waliokuwa wakipelekea nguruwe chakula.
Mwili wa Bw. Festo pia ulizikwa siku hiyo ambayo alizikwa mkewe Bi. Bilivu.

No comments:

Post a Comment