Wednesday, January 16, 2013

Majambazi matatu wauawa Muleba katika majibizano ya risasi na polisi



Na Mwandishi wetu
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa na jeshi la polisi mkoani Kagera katika majimbizano ya risasi wakati wakiwa katika harakati  za  kutaka kuvamia kituo cha mafuta  wilayani Muleba.
Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Phillip Kalangi alisema tukio hilo limetokea Januari 14, mwaka huu saa 2 usiku katika kituo cha mafuta cha BP Wilayani Muleba.
Katika tukio hilo kundi la watu wapatao watano walitakiwa kusimama na askari lakini walikataa kutii agizo hilo na hivyo kuanza kuwarushia polisi risasi za moto na polisi kujibu mapigo yao ambapo polisi walifanikiwa kuwauawa watu watatu papo hapo.
Katika jaribio hilo Jeshi la polisi lilifanikiwa kuwapokonya majambazi  bomu moja la kutupwa kwa mkono,  magobore  mawili , bunduki moja aina ya SMG yenye namba 08462289 na risasi  25.
Aidha kamanda Kalangi alisema miongoni mwa watu hao watano watu wawili walifanikiwa kutoroka kusiko julikana.
 Alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wilayani humo  waliopanga kuvamia kituo cha mafuta cha BP na hivyo jeshi hilo kuweka mitego yake.
Alisema kati ya watu hao waliouawa ni mtu mmoja tu ndiye ameweza kutambuliwa kwa jina  Jafety Mwigabo  raia Kirundo nchini  Burundi kulingana na kitambulisho alichokutwa nacho.
Kamanda Kalangi alisema majambazi hao waliouawa  ni miongoni wanaounda mtandao wa majambazi  wanaopora wavuvi mali zao katika ziwa Victoria na kwamba walikuwa wakitafutwa kwa kipindi kirefu na jeshi hilo.
Miili ya majambazi hayo yamehifadhiwa katika kituo cha afya cha Kaigara wilayani Muleba yakisubiri ndugu na jamaa kutambua.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment