Friday, January 31, 2014

Wafanyabiashara Bukoba wakerwa na kodi wanazotozwa na Jeshi la Zima moto



Na Theonestina Juma
 BAADHI ya Wafanyabiashara wa mjini Bukoba wameitaka serikali kufuta kodi wanaozotozwa na Jeshi la Zimamoto kutokana na wao huduma wanazotoa ni kama majeshi mengine nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wakizungumza na Naibu Waziri wa fedha,  Adam Malima katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Kagera mjini Bukoba.
“Unakuta kila mwezi Jeshi la zima moto linazunguka katika maeneo ya biashara zetu kukusanya kodi ambazo hatuzijui ni kwa ajili ya nini, wao hawana tofauti na majeshi mengine zaidi ya sita wanazotoa huduma kwetu bure, mbona Jeshi la polisi wanatulinda na mali zetu bila kututoza kodi”alisema mfanyabiashara, Jemsi Mwanga.
 Mwanga alienda  mbali zaidi kwa  kwa kuhoji kuwa huenda Jeshi la Wananchi (JWT) ambao wanajukumu kubwa la kulinda mipaka yetu wakianza kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara hali itakuwaje kwao?
Kuhusu mashine ya EFD wafanyabiashara hao waliitaka Serikali kuwaacha wajinunulie mashine yao kokote wanakojua na mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)wawauzie kadi (line) kama ilivyo kwa upande wa simu za kiganjani.
“Tunaomba serikali iwache wafanyabiashara wanunue mashine za EFD wenyewe halafu TRA wawauzie line kama ilivyo kwenye simu, na si kuwalazimisha wafanyabiashara wanunue mashine hizo ambazo bei yake ni ghali”alisema Remigius maafuru mjini hapa kwa jina la Dkt. Remmy.
Hata hivyo, kwa upande wa Naibu Waziri, Malima akizungumzia juu ya kodi za Jeshi la Zima moto, alisema wao wana ‘theory’ yake ambayo wao wameiweka lakini hata wao katika baraza la Mawaziri wamekuwa wakihoji hilo ambapo hata hivyo utoaji huduma zao kwa jamii iko tofauti na majeshi mengingine.
Alisema”Nawambieni wazi hili la asuala la Jeshi la ZimaMoto hata sisi kwenye baraza la Mawaziri tulihoji, hii kodi  ni ya nini? Inakwenda wapi? Mpaka sasa hata bado tunasubiri majibu lakini kaeni mkijua kuwa kila Jeshi lina utaratibu wake”
Alisema hata yeye binafsi suala hilo la zimamoto linamsumbua, kwani hajui tozo hizo  ni kwa ajili ya nini kwani hata kwa wakulima, wafanyabishara wadogo  na  wa wakati wote wanalalamikia hilo tozo.
Hata hivyo, Naibu huyo aligeuka kuwa mbogo baada ya Remigius kutoa pendekezo la serikali kuondoa tozo za kusafirisha fedha nje ya nchi pindi  mfanyabiashara kwenda kununua bidhaa nje ya nchi kwani ni miongoni mwa sababu ya bidhaa kupanda bei na hivyo kumuumiza mlaji.
Alisema kamwe haiwezekani na wala serikali haiweze kuondoa tozo hilo na wasije wakafikiria kuwa iko siku serikali itaondoa tozo hiyo.
“Hivi kuna nchi yoyote ambayo inasafisha fedha zake kwenda nchi nyingine bila kutoza ushuru, haiwezekani”alisema.
Awali  Kamishina wa TRA Taifa,Patrick  Kasera akizungumzia umuhimu wa mashine ya EFD alisema kuwa ni kumwezesha mfanyabiashara kutunza kumbukumbu za mauzo na biashara zake, ambapo asilimia kubwa ya wafanyabiashara wengi ambao hawasimamii katika biashara zao wamekuwa wakiibiwa pasipokujua ni kiasi gani wanachoibiwa.
Halikadhalika alisema tatizo kubwa kwa Watanzania ni kumbu kumbu  ambapo hasara yake ni kukadiriwa  kipato chake kutokana na biashara yake  na matokeo yake huona kuwa anaonewa na TRA bila kuwa na uthibitisho.
Alisema “Kazi ya mashine hizo ni kutunza kumbukumbu vizuri na kukuwezesha kulipa kodi stahili na anayeona anaonewa hata ona hilo tena, kwani watu wengine wanafilisika bila kujua kama wao wenyewe hawasimamii biashara zao, lakini kwa kupitia TFD huweza kubaini hata kama hatakuwepo kwenye biashara zake”alisema.    
Alisema mashine za EFD zinamwezesha kila mtu kulipa kodi vizuri  bila kufilisika kwani atapewa makadirio ambayo  anaweza kuyamudu tofauti na hapo aawali ambapo mtu alikadiriwa tu kodi kumbe kiasi hicho kilikuwa ni kikubwa tofauti  na uwezo wake.
Mwisho.

   


No comments:

Post a Comment