Saturday, February 1, 2014

JAMBO BUKOBA YAWAJENGEA UWEZO WATOTO WA KIKE KUJIAMINI NA KUSHIRIKIANA NA WENZAO KATIKA ELIMU PAMOJA NA MICHEZO



Jambo Bukoba ni Shirika lisilokuwa la Serikali linalofanya kazi mkoani Kagera kwa kushirikiana na serikali ya mkoa. Mwanzilishi wa Jambo Bukoba  anaitwa Bw. Clemence Mlokozi ambaye asili yake ni mkoani Kagera katika Wilaya ya Missenyi Kijiji Ishozi na anaishi nchini Ujerumani.
Jambo Bukoba ilianzishwa mkoani Kagera kwa kusaidia watoto hasa wanafunzi wa shule za msingi kuanzia miaka 5 hadi 19 kujenga afya zao kimichezo ili kujikinga na maabukizi ya UKIMWI, kuweka haki sawa katika elimu kupitia michezo kwa wasichana na wavulana.
Shirika hili chini ya mwanzilishi wake Bw. Mulokozi tangu kuanzishwa kwake mkoani Kagera  limekuwa likiwafunza watoto  katika shule za msingi  kila wilaya michezo midogo midogo ya kujenga ushirikiano wa pamoja hasa watoto wa kike kujiamini na  kushirikiana zaidi na wenzao wa kiume.
Jambo Bukoba katika kuhakikisha inapunguza unyanyapaa wa kuwatenga watoto wa kike katika jamii imeweza kueneza elimu kupitia michezo kwa watoto wote kushirikiana kwa pamoja bila kujali jinsia za watoto iwe katika masomo , michezo au katika shughuli nyingine za kijamii.
Ili kuleta umoja katika mkoa kwa watoto wa kiume na kike Jambo Bukoba kuanzia mwaka 2012 ilianzisha bonanza la michezo kila mwisho wa mwaka la kuwaunganisha watoto kutoka shule mbalimbali mkoani Kagera ili waweze kushirikiana pamoja kimichezo na kujenga kujiamini kwa pamoja.
Bonanza la michezo la Jambo Bukoba mwaka 2013 limefanyika mwaka huu 31 Januari, 2014 na kushirikisha Wilaya zote za mkoa wa Kagera  pamoja na mwanzilishi wa Jambo Bukoba akiambatana na wenzake kutoka nchini Ujerumani.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Kanali Mstaafu Massawe alikuwa mgeni rasmi ambapo katika hotuba yake ya ufunguzi aliwashukuru Jambo Bukoba kuanziasha bonanza la michezo ili kuwajenga watoto kiakili na kujiamini  aidha  aliwahimiza wazazi  kuwaruhusu watoto wao kucheza kwani michezo nayo ni ajira.
Jambo Bukoba hutoa vifaa vya michezo kama vile fulana na bukta za michezo, viatu na mipira  katika shule mbalimbali mkoani Kagera. Vilevile ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu nzuri Jambo Bukoba imeanza kukarabati miundombinu mbalimbali ya baadhi ya shule za msingi mkoani hapa.
Miundombinu hiyo ni pamoja na madarasa ambayo yameharibika na kuhitaji ukarabati, kujenga matundu ya vyoo mapya pamoja na kukarabati ofisi za walimu ambazo ziko katika hali mbaya ili kuwarahisishia walimu kutekeleza majukumu yao vizuri ya ufundishaji.
Bw. Mulokozi anasema lengo lake kubwa kuanzisha Bukoba ni kupunguza kasi ya watoto wa kike kuanzisha mahusiano ya kimapenzi wakiwa wadogo, pia  kupunguza unyanyapaa wa wtoto wa kiume kwa wasichana ambapo Jambo Bukoba imepunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa mkoani Kagera.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2014

No comments:

Post a Comment