Na
Theonestina Juma, Bukoba
WANAFUNZI 14
kati ya 175 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu katika shule
ya sekondari ya Kaigara Wilayani Muleba ndiyo wamesharipoti shuleni, tangu
shule zifunguliwe Januari 13, mwaka huu.
Hayo yamebainishwa
jana na Mkuu wa shule hiyo, Bw. Sadru Majid wakati akizungumza kwenye mkutano wa wazazi uliofanyika shuleni
hapo.
Alisema
chanzo cha wanafunzi hao wachache kuripoti ni
kutokana na baadhi ya wazazi wao kutokuwa na fedha za kuwalipia mahitaji
mbali mbali yanayohitajika shuleni hapo kama vifaa vya shule.
Alisema “wazazi
wengi wanalalamika kuwa hawana fedha kwa ajili ya kuwalipia watoto wao mahitaji
mbali mbali za shule hivyo, hadi tunaanza mwaka wa masomo ni watoto 14 tu ndiyo
wamesharipoti kati ya watoto 175 waliopangiwa katika shule hii”
Hata hivyo,
baadhi ya wazazi wakizungumza katika mkutano huo walidai kuwa wameshindwa
kuwapeleka watoto wao shuleni kutokana na kuwepo kwa michango mingi
inayohitajiwa shuleni hapo.
Pia walidai
kuwa kushindwa kwa mitihani ya kidato cha pili kwa baadhi ya wanafunzi ni
miongoni mwa chanzo cha watoto kuacha shule na kunawakatisha tamaa kwa kuhofia
kuharibu fedha zao huku watoto nao wakijiingiza katika shughuli zingine kama
usafirishaji wa abiria kwa kutumia baiskeli na uvuvi.
Hata hivyo
kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya MUleba, Bw. Lembris Kipuyo amewataka wazazi na
walezi wa watoto wao kuwapeleka watoto shuleni mara moja hata kama hawana fedha
za kuwalipia ada na vifaa vinavyohitajika shuleni hapo.
“Alisema
Wazazi na walezi wa watoto ambao hawajariporiti shuleni, wahakikishe watoto wao
wanaripoti shuleni mara moja, kwani huko watapewa maelekezo namna ya kuwalipia
watoto wao vifaa vya shule, hata kama hawana fedha kwa wakati huu”alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Halikadhalika amewataka Madiwani na watendaji wa
kata husika kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia agizo hilo ili kuwabaini
wazazi na walezi watakaobainika kukiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za
kisheria
No comments:
Post a Comment