Hivi
karibuni kumekuwa na taarifa za kutisha katika Wilaya ya Butiama mkoa
wa Mara ambapo imearifiwa baadhi ya wanawake kuuawa kikatili kwa kukatwa
vichwa. Sababu ambazo hazijathibitishwa zinaeleza kuwa chanzo cha
mauaji hayo ni pamoja na imani za kishirikina, uchu wa kumiliki mali, kulipiza visasi na kuendekeza hulka ya ukatili kwa kudhani kuwa mhusika anapata heshima yoyote katika jamii.
Wizara
ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto imepokea kwa masikitiko makubwa
taarifa za kuwepo kwa mauaji hayo ya kikatili na inawataka wananchi
kutoa ushirikiano thabiti ili kuhakikisha kuwa matukio hayo ya udhalimu
YANAKOMA MARA MOJA.
Wizara
inalaani vikali mauaji ya wanawake waliokatishwa maisha yao kutokana na
kuuawa na watu wenye fikra potofu dhidi ya wanawake. Wizara inasisitiza
kwamba wanawake
wanayo haki ya kuishi kama inavyosisitizwa katika Ibara ya 14 ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 inayotamka kuwa ‘Kila
mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya
maisha yake kwa Mujibu wa Sheria.’
Wakati
mwingine wanawake wamekuwa wakikandamizwa katika jamii kutokana na
tofauti za kimaumbile na hivyo kusababisha ukatili au mauaji. Wizara
inaitaka jamii itambue kuwa wanawake wana haki ya kuthaminiwa utu wao na
kushiriki haki zote za msingi bila ubaguzi wowote ambao unaweza
kuhatarisha haki zao ikiwemo haki ya kuishi ambayo ndio haki kuu kuliko
haki zote.
Vitendo
vya mauaji ya kikatili wanavyofanyiwa wanawake wa wilaya ya Butiama ni
jambo ambalo linasababisha hofu kubwa miongoni mwa wanawake. Mauaji hayo
yana wakosesha amani na utulivu na hivyo kuzorotesha ari yao katika
shughuli za uzalishaji mali kwa wanawake wa wilaya ya Butiama na Taifa
kwa ujumla. Mwananchi ambaye anawindwa kama mnyama kamwe hawezi
akashiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi kwa kuogopa
kuwa, maisha yake yako hatarini.
Kwa
kutambua hili Wizara inaagiza wadau wote kuiunga mkono Serikali katika
kuhakikisha kwamba uhai wa wanawake wa Butiama na kote nchini
unalindwa. Wananchi watambue kuwa tukio la mauaji dhidi ya mtu yeyote
ni kinyume na haki za binadamu na ni kosa la jinai.
Katika
kipindi hiki cha majonzi, Wizara inatoa pole kwa familia ambazo
zimeguswa na mauaji ya ndugu zao waliopoteza maisha, Wizara inahimiza
wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha watuhumiwa wa mauaji
wanafichuliwa na kuchukuliwa hatua ili kukomesha tabia hiyo.
Mwisho, Wizara inapenda
kuikumbusha jamii kuwa, mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake
yanapingana na jitihada kubwa za Taifa katika kutekeleza sheria za nchi
na Mikataba ya Kimataifa na Kikanda kuhusu haki na usawa wa kijinsia,
Aidha ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanaishi katika hali ya usalama, amani na utulivu.
Sophia M. Simba (Mb)
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto
23 Januari, 2014
No comments:
Post a Comment