Wednesday, January 1, 2014

Salaam za Rais Kikwete mwaka mpya 2014


SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2013




UtanguliziNdugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu wengi ambao hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia mbele ya haki. Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.

Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi; 
Tunaumaliza mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora zaidi mwaka 2014 na daima dumu.

Hali ya usalama wa ndani ya nchi nayo ni nzuri. Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu haipo. Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo mbaya amepita tuombe atokomee kabisa.

Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo, umoja, kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui na mifarakano. Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. “Mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi”. Tuchague kuijenga nchi yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.

Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea kupambana na vitendo vya uhalifu. Mafanikio ya kutia moyo yameendelea kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014 na miaka ijayo.

Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Kati ya Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na kilo 89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631wametiwa mbaroni. Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.

Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya. Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa kufanya zaidi.

Ujambazi
Ndugu wananchi;
Jeshi la Polisi limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio yameendelea kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013 ukilinganisha na mwaka 2012. Takwimu zifuatazo zinathibitisha ukweli huo. Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409. Mwezi Julai mwaka huu, niliamua kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka Ngara kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi Kakonko. Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee.

Ndugu Wananchi;
Uamuzi wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na mafanikio ya kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa. Silaha nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo. Aidha, watu 31,203waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi makwao. Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa wakati wa Operesheni. 

No comments:

Post a Comment