Friday, August 2, 2013

Kumpinga Meya wa Bukoba ni kanuni za halmashauri-CCM BUKOBA



Na Theonestina Juma,Bukoba
CHAMA cha Mapinduzi [CCM] katika  Manispaa ya Bukoba kimesema mambo yanayotokea kwa sasa kati ya madiwani 15 wanaompinga Meya wa Manispaa hiyo, Dkt.Anatory Amani yanakwenda kulingana na kanuni za halmashauri  nchini.
Aidha Uongozi wa CCM mjini hapa,umesema wanakubaliana na maneno aliyoyaongea, Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na migogoro iliopo kati ya Meya na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini ambaye pia  Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ya kutaka wakae chini  na kumaliza tofauti zao.
Akizungumza na gazeti hili mjili hapa, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Bw. Yusuph Ngaiza alisema kwa sasa yale yote ambayo Rais Kikwete  aliyasema tayari wameanza kuyatekeleza, bila kufafanua ni mambo yapi ambayo wameanza kutayetekeleza hadi hivi sasa.
“CCM wilaya imeanza  kutekeleza yale yote ambayo Rais alituasa akiwa mkoani hapa, lakini yanayotokea kwa sasa ndani ya Manispaa ya Bukoba kati ya madiwani 15 ya kumpinga Meya yanakwenda kulingana na kanuni za halmashauri hivyo kauli kuwa ‘madiwani wa CCm wamgeuka Kikwete’ sio kweli”alisema
Alisema maneno aliyoyasema Rais Kikwete ni kwa ajili ya kujenga chama pamoja na manispaa ya Bukoba.
Katika mkutano wa hadhara wa Rais Kikwete katika uwanja wa Kaitaba alimtaka Mstahiki meya wa Mansipaa ya Bukoba , Dkt. Amani na Bw. Kagasheki kukaa chini na kumaliza tofauti zao kwani hakuna kitu kisichokuwa na mwisho.
Halikadhalika aliuagiza uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuhakikisha inawalipa watu wanaodai viwanja 800 bila masharti yoyote kwani tangu mwaka 2003 ni kipindi kirefu.
Pia alitaka  uongozi wa manispaa hiyo kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa soko kuu la kisasa, lakini kabla ya kuanza zoezi hilo watafute sehemu pa kuhamishia wafanyabiashara walioko ndani ya soko hilo kwani hapo ndiko wanakopata riziki yao.
Hata hivyo, katika uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa pamoja na maneno ya Rais Kikwete kwa  CCM mjini hapa, aliponyanyua miguu yake tu kesho yake jumanne wiki hii, madiwani wanne wa CCM waliwasilisha barua kwa mkurugenzi ya kutaka uitishwe baraza la madiwani kwa lengo la kutaka kupiga kura ya kutokuwa imani Meya wa manispaa hiyo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment