Thursday, August 15, 2013

Wabunge wa kamati ya kudumu ya bunge Miundombinu wanusurika kifo



 Na Theonestina Juma

WABUNGE zaidi ya 11 wa kamati ya kudumu ya Bunge ya miundo mbinu jana wamenusurika kifo baada ya gari waliokuwa wamepanda kuwaka moto ghafla wakati wakienda Wilayani Missenyi mkoani Kagera.



Tukio hilo lilitokea jana katika eneo la mwanzo mgumu mpaka wa wilaya ya Missenyi na halmashauri ya wilaya ya Bukoba katika barabara kuu iendayo  nchi jirani ya Uganda wakati wabunge hao wakiwa wanelekea katika eneo la Omukajunguti wilayani Missenyi  sehemu ambayo inatarajiwa kujengwa uwanja wa kisasa cha kimataifa.



Katika tukio hilo ambalo lilizua taharuki miongoni mwa Wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Bw.Peter Serukamba  ambaye ni Mbunge Kigoma Mjini ilimlazimu kila mmoja kutafuta njia yake ya kupitia kutoka ndani ya gari hilo.

Kamati hiyo waliokuwa wamepanda gari aina ya costa yenye namba ya usajili T 570 BYU ambayo liliandaliwa na uongozi wa mkoa lilipata hitilafu baada ya kuanza kutoa moshi mwingi kwa upande wa nyuma wakati likiwa kwenye mwendo mkali na kuleta hofu kubwa kwa abiria walikuwemo ndani ya gari hilo.



Hata hivyo, dereva wa costa aliyegundua gari linataka kuungua alifanikiwa kulisimamisha gari hilo na kuwataarifu wabunge hao ambapo yeye alifanikiwa kurukia dirishani na kuwaacha wabunge hao wakihaha.

“Wabunge waliweza kubanana mlangoni huku wengine wakirukia dirishani kweli ilikuwa ni pata shika nguo kuchanika” alisema shuhuda mmoja

Kwa mujibu wa wabunge walikuwemo kwenye gari hilo walisimulia kuwa baada ya kuambiwa kuwa gari linaungua kila mmoja alifanya juhudi za kujiokoa yeye mwenyewe ambapo mmoja wao alipita dirishani na wengine walifanikiwa kusukuma mlango na ukafunguka na kutoka salama.

Hata hivyo, katika tukio hilo hakuna mbunge aliyeumia isipokuwa mbunge wa viti maalum bi. Elizabeth Batenga  aliumia mkono kidogo baada ya kubanana mlangoni.

Aidha imeelezwa kuwa sehemu ya injini ya gari hilo liliungua vibaya ambapo hata hivyo, wabunge hao waliendeela na safari zao baada ya kupanda magari madogo yaliokuwepo katika msafara huo.

Wabunge waliokuwemo katika gari hilo ni pamoja na  Bi.Rebbecca Mngondo (Arusha Viti Maalumu), Bi.Rita Kabati (Iringa Viti Maalumu), Bi.Mariam Msabaha (Zanzibar Viti Maalumu), Bi.Elizabeth Batenga (Kagera Viti Maalumu), Bi. Madabida (Dar es Salaam Viti Maalum) na  Bi. Clara Mwatuka (Mtwara  Viti Maalumu).

Wengine ni Bw.Mzee Hussein (Zanzibar), Bw.Mussa Haji Kombo (Pemba Zanzibar),Bw. Abdul Mteketa (Jimbo la Kilombelo) na Bw. Mutula Mutula (Jimbo la Tunduru Kusini).

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati  hiyo Bw.Serukamba Hakuwemo katika gari hilo lilotaka kuungua ambapo kamati hiyo ilikuwa katika zira ya siku moja mkoani hapa ya  kukagua miundombinu ya badandari ya mkoani pamoa na pamoja na viwanja vya ndege.

No comments:

Post a Comment