Tuesday, August 20, 2013

wabambwa na bunduki mbili na risasi 78 wakiwa wamezifukia ardhini



Na Mwandishi Wetu
JESHI la polisi mkoani Kagera limefanikiwa kukamata bunduki mbili zilizokuwa zikitumika katika matukio mbalimbali ya ujambazi ,ikiwemo utekaji na ujangili pamoja na risasi 78 zinazotumika katika bundukia aina ya SMG/SAR.
 Kamanda wa polisi mkoani hapa, Philip Kalangi alisema kuwa silaha hizo zimepatikana kutokana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo ambapo bado unaendelea katika wilaya zote za mkoa huu ili kuwabaini na kuwakamata wale wanaojihusisha na vitendo vya uharifu.
 Kamanda Kalangi alizitaja silaha hizo kuwa ni SMG yenye namba za usajili KO 17753 na Gobole moja  pamoja na risasi 78 na magazine tatu tupu zikiwa zimefukiwa ndani ya mashimo mawili tofauti nje ya nyumba.
 Alisema Agosti 11 mwaka huu saa 4.25 usiku katika kijiji cha Sasa Maharage, kata ya Lusahunga Wilayani Biharamulo polisi waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata, Kazuba Misigwa  (41) ambaye alikuwa akimiliki SMG ambapo alikiri baada ya kukamatwa na kuwapeleka polisi na kuwaonyesha shimo ambalo walifukua na kukuta silaha hiyo na risasi 78 na magazine tatu tupu zikiwa zimefungwa  kwenye kiroba.
 Alisema baada ya kumhoji zaidi alimtaja mwenzake mwingine aitwaye ,Alex Emmanuel (35)mkazi wa kitongoji chaNyangamagulu eneo la Nyakahula Mizani Wilayani Biharamulo ambaye pia alikamatwa na kuhojiwa alikiri na kuonyesha silaha nyingine aina ya gobole iliyotengenezwa kienyeji.
 Waliendelea kuhojiwa ndipo wakakiri kuwa silaha hizo wamekuwa wakizitumia kwa pamoja katika matukio mbalimbali ya kiuhalifu na ujangili yaliyokuwa yakitokea katika maene mbalimbali ya mkoa huu na mikoa mingine.
 Alisema kutokana na kauli hizo za watuhumiwa hao jeshi hilo linaendelea kuwahoji kwa kina ili kuyabaini matukio hayo waliyoyafanya, wahusika wengine na maeneo ili waweze kufanya ufuatiliaji zaidi.
 Hata hivyo,  zaidi ya silaha 45 zimeweza kusalimishwa na wananchi mbali mbali wiki tatu zilizopita hadi  Agosti 19 mwaka huu.
  Hatua hiyo ni kutokana na agizo la Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa katika ziara ya kikazi mkoani Kagera la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuzisalimisha kabla hawajakumbwa na msako mkali unaotarajiwa kuanza muda wowote.
Alisema hadi sasa jumla ya wahamiai haramu 10,035 wameondoka nchini kwa hiari yaohadi kufikia jana.

No comments:

Post a Comment