Tuesday, August 13, 2013

Wahamiaji haramu 7814 waondoka Kagera, Wanyarwanda 166 watimkia Uganda na mifugo yao



Na Theonestina Juma

JUMLA ya wahamiaji haramu 7814 waliokuwa wakiishi mkoani  Kagera  wameripotiwa kuondoka nchini kupitia mipaka zaidi ya  10 zilizoko mkoani hapa kufuatia agizo  la Rais Jakaya Kikwete  la kuwataka kuondoka ndani ya siku 14 alizotoa kwao.

  Akizungumza na Mwandishi habari wa gazeti  hili ofisini kwake jana , Naibu Kamishna wa uhamiaji ambaye ni Kaimu afisa uhamiaji Mkoa  wa Kagera,Bw. Elizeus Mushongi alisema idadi hiyo ya wahamiaji haramu walioripoti katika vituo mbalimbali vya uhamiaji vilivyopo mkoani hapa ni ndogo ikilinganishwa na wahamiaji wanaondoka kupitia njia za panya ambao ni wengi.

 Aliswema kituo kinachoongoza kupitisha wahamiaji haramu wengi ni cha Rusumo  ambacho kimewapitisha jumla ya wahamiaji  haramu 4748 wakielekea nchini Rwanda.

 Mushongi alisema katika makundi hayo ya wahamiaji haramu ambao wanatoka katika nchi tatu ambazo ni Uganda,Burundi na Rwanda kuna wahamiaji wengine ambao hawataki kururudi kwao na idadi kubwa ya wasiotaka kurudi kwao ni Wanyarwanda  wanaojiorodhesha katika vituo wakielekea Burundi na Uganda.

 Halikadhalika wengi wao wameeonekana wakipita njia za panya wakielekea nchi hizo pia.

 Alisema  katika  vituo  vya  Murusagamba walipita wanayarwanda 35 wakielekea Burundi,Mutukula 13 wakielekea Uganda,Bugango 22wakielekea Uganda,Kanyigo saba wakielekea Uganda.

 Halikadhalika kituo cha Kabanga Warundi  522  wamepita kurudi nchini mwao na 10 kupitia kituo cha Murongo kuelekea Uganda katika kituo hicho Wanyarwanda 166 walipitia hapo kuelekea nchini Uganda.

  Alisema kituo cha Murongo kimepitisha jumla ya wahamiaji 332,Murusagamba 78 na Mutukula 31 na eneo la Mgoma ambalo hakuna vituo vya idara ya uhamiaji walijisalimisha wahamiaji haramu 1734  katika ofisi za vijiji.

 Alisema  idadi ya ng’ombe walioondoka hadi kufikia jana walioripotiwa ni 1996 kupitia kituo cha Rusumo hata hivyo alisema kuwa ng’ombe wengi wanaelekea Uganda  kwa sababu Rwanda hawataki idadi kubwa ya Ng’ombe.

 Alisema kwa mujibu wa takwimu za wahamaiji haramu  walioondoka kwa hiari Wanyarwanda asilimia 64,warundi asilimia 34 na waganda,asilimia mbili.

 Alisema msako maalum haujaanza na unatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa  na wameishaanza maandalizi.

 Hata hivyo aliwataka wahamiaji hao haramu waendelee kuondoka kwa hiari kabla hwajafikishwa kwenye mkono wa sharia.

 Aidha  alisema Idara ya uhamiaji Mkoa wa Kagera imesitisha utoaji wa vibali kwa muda wakisubiri maelekezo kutoka juu.

 Mkuu wa Mkoa wa Kagera kanali mstaafu Fabian  Massawe  amewatahadharisha wananchi kuwa makini wakati wa msako huo wa wahamiaji haramu sambamba na kuwafichua waliojificha.

 Massawe  alisema serikali haitasita kuwachukulia hatua kwa mujibu wa  sheria  watu watakaobainika wakiwa ficha na kuwawekea vifua  wahamaiji haramu.

 Alisema msako huo utaanza muda wowote kuanzia sasa  na hawezi kutaja  siku rasmi  kwa sababu za kiusalama.

 Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera  Philip  Kalangi alisema jumla ya silaha 42 zimewasilishwa kwa hiari na wahamiaji haramu kufuatia agizo la Rais lililoisha jana kutoka sehemu mbalimbali hapa Mkoani nyingi zikiwa ni magobore.

 Alisema  wahamiaji haramu wote watakaokamatwa  watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sharia.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment