Tuko kushoto kulia, kulaani mauaji ya kikatili ya Daud Mwangosi.
Kweli tunauchungu kumpoteza mwenzetu hivi hivi mkononi mwa polisi.
Tunataka kamera yake irejeshwe kwa nini wanaikatalia?
Mwenyekiti wa KPC Bw. John Rwekanika akitoa tamko
Wanahabari wakiwa kazini leo kulaani mauaji ya Mwangosi
Na Theonestina Juma, Bukoba
WAANDISHI wa habari mkoani Kagera leo wameandamana kulaani
mauaji ya kikatili ya mwandishi wa habari wa kituo cha Luninga cha Chanel 10,
Bw. Daud Mwangosi.
Maandano hayo yalioanza saa 3.40 asubuhi katika kituo cha
mabasi mjini hapa na kupitia katika barabara za Jamhuri, tupendane, Kagera
Studio, Samuel Luangisa ,Uganda kumalizikia katika Ofisi ya chama cha waandishi
wa habari mkoani Kagera (KPC) yalikuwa rasmi kutokana na kuruhusiwa na Jeshi la
polisi mkoani hapa na kuwapatia ulinzi.
Akizungumza mara baada ya kupokea maandamano hayo, Mwenyekiti
wa chama cha Waandishi wa habari Mkoani Kagera (KPC), Bw. John Rwekanika
alisema serikali inatakiwa kuwachukulia hatua kali za kisheria Askari wote
waliohusika katika mauaji ya kikatili ya Bw. Mwangosi.
Alisema kulingana na picha zinavyoonesha mauaji ya Mwangosi
yalikuwa ya kikatili yaliofanywa na Jeshi la polisi, kitendo ambacho
kimefedhehedha taifa, na ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Alisema askari waliohusika katika tukio la kifo hicho,
wasimamishwe kazi ili kupisha uchunguzi unaoendelea ufanyike kwa uhuru na haki
na Kamanda wa mkoa wa Iringa, Bw. Michael Kamuhanda awajibishwe na nafasi yake
apewe mtu mwingine ambaye atakuwa tayari kutekeleza kwa vitendo ulinzi na
usalama wa raia.
“Katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa Bw. Kamuhanda alikuwepo,alishindwa kumwokoa
marehemu mwangosi, hivyo ameshindwa kazi, awajibishwe nafasi yake apewe mtu
mwingine ambaye yuko tayari kulinda usalama wa raia”alisema Bw. Rwekanika.
Alisema kulingana na mauaji hayo Jeshi la polisi linatakiwa
kukaa chini na kujiuliza na kuangalia ni namna gani watakavyowalinda waandishi
wa habari wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi za kila siku katika maeneo
ya mikutano.
“Tunataka jeshi la polisi kuweka utaratibu utakaowezesha
wanahabari kufanya kazi zao bila dharau na kujengewa hofu kutokana na vitisho
vya polisi’alisema.
Halikadhalika serikali pia iandae utaratibu ambao
wanahabari, wanasiasa na polisi watatumia kufanya kazi hasa katika kipindi hiki
ambacho nchi inakuwa katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ili kuepusha
nchi situmbukie katika mazingira hatari zaidi.
Katika maandamano hayo waandishi hao wa habari walibeba
mabango yenye ujumbe mbali mbali yaliosomeka kama, tunaangalia Jeshi la polisi
kama rafiki wa mashaka, Mauaji ya Mwangosi na raia wengine ni kipimo cha kuzima
uhuru wa habari na demokrasia, Waandishi wa habari tuhakikishiwe ulinzi na
usalama wetu na Wanahabari tunalaani vitisho, mateso na mauaji wakati tukitekeleza
wajibu wetu kwa umma.
No comments:
Post a Comment