Tuesday, September 11, 2012

Sakata la wizi wa watoto wa kike kushamiri Kagera, wananchi wavamia mahabusu ya mahakama na kumtoa mtuhumiwa na kumuua mbele ya 'Hakimu'


Na Theonestina Juma, Bukoba
WANANCHI wenye hasira wamevamia mahabusu ya mahakama ya mwanzo ya Muhutwe wilayani Muleba na kuvunja milango na kumtoa mtuhumiwa na kisha kumuua papo hapo.
Hatua hiyo imekuja baada ya mtuhumiwa huyo kufanya jaribio la kutaka kumwiba mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyailigamba  wilayani Muleba kwa njia za uchawi.
Tukio hilo la aina yake ambalo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Phillip Kalangi limetokea jana  Septemba 10 mwaka huu, saa 5.00 asubuhi katika katika kata ya Muhutwe wilayani Muleba.
Mtuhumiwa aliyevamiwa katika kituo hicho cha polisi na kuondolewa ndani na kuuanza kushambuliwa na wananchi hadi kufa ni Bw. Faustine Rweyemamu (60) mkazi wa Ndolange wilayani humo.
Alisema siku hiyo ya tukio, mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Zakia Hashimu (15)  anayesoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Nyailigamba  na mkazi wa kitongoji cha Kamukuti aliondoka kwenda shule lakini watu walibaki kushangaa kumwona akiwa na mzee huyo wakielekea kusikojulikana.
Imeelezwa kuwa Bw. Rweyemamu ambaye alionekana kuandamana na mwanafunzi huyo, asubuhi  wakielekea katika maeneo ya porini, wananchi hao walimtilia shaka na kufanya mtego hadi kumkamata na kumfikisha katika kituo kidogo cha polisi Mutuhutwe.
Lakini kutokana na wananchi hao kuwa na hasira kutokana na mauaji ya kikatili ya mtoto Beatha James (12) aliyeokotwa akiwa ameuawa na kuchunwa ngozi, Saeptemba 7, mwaka huu  na kuchukuliwa baadhi ya viungo muhimu waliamua kuvunja mlango na kuingia ndani na kumtoa mtuhumiwa huyo na kupiga na kumuua papo hapo.
Imeelezwa kuwa watu hao kwa sasa wamekuwa wakiwafanyia dawa watoto hao kwa lengo la kuwavuruga akili na kufuatana nao wanakokwenda kwa lengo la kuwadhuru.
Hata hivyo, licha ya matukio ya watoto hasa wa kike kupotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine kukutwa wakiwa wameuawa kikatili, katika uchunguzi wa gazeti hili umebaini kutokuwepo kwa ufuatiliaji wowote unaofanywa na Jeshi la polisi la mkoa Kagera.
Kutokuwepo kwa ufuatiliaji huo na kutowaeleza wananchi ni kitu gani kinachoendelea juu ya utoroshaji na wizi wa watoto,  zaidi ya jeshi hilo kuwataka wananchi kutochukua sheria mkononi unawaacha wananchi  njia panda na kwa sasa kufikia hatua kujichukulia sheria mkononi.
Bw. Josephat Juma mkazi wa mjini Bukoba akizungumza na gazeti hili alisema kwa sasa imefikia hatua wananchi wanaishi maisha ya wasi wasi hasa kwa wale walio na watoto kwani wizi wa watoto unaonekana kushamiri kwa kasi katika mkoa wa Kagera.
Asilimia kubwa ya watoto wa kike ndiyo wanaonekana kuripotiwa kwa kasi kupotea, ambapo mtandao wa watu wanaowaiba watoto hao haujajulikana.

No comments:

Post a Comment