Friday, September 21, 2012

MKUU WA MKOA ATATUA MGOGORO WA SHULE KATI YA WANANCHI NA MBUNGE WAO.


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian I. Massawe hatimaye ametatua mgogoro wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri kati ya Wananchi na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Muleba Kaskazini Ruth Blasio Msafiri kwa kipindi cha mwaka 2005 hadi 2010.
Mhe. Massawe alikabidhi shule hiyo kwa Wananchi wa Kata ya Katoke jana tarehe 17/09/2012 ili waendeleze ujenzi baada ya kuwa na mgogoro zaidi ya miaka miwili kati ya Wananchi na aliyekuwa mbunge wao 2005 hadi 2010 kwa kudai shule hiyo ni mali yake binafsi baada ya kuwa ameshindwa ubunge mwaka 2010.
Shule hiyo ya Sekondari ya Wasichana ya Ruth Msafiri iliyoko katika kitongoji cha Kimbugu, Kijiji Katoke Tarafa Izigo Halmashauri ya Wilaya Muleba ilianzishwa na Ruth Blasio Msafiri wakati huo akiwa Mbuge wa Jimbo la Muleba Kaskazini mwaka  2009.
Kulingana na taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na seriklai ya kijiji Katoke Ruth Msafiri alitoa wazo la kuanzisha shule ya wasichana na kuomba ardhi katika serikali ya kijiji na kupewa Ekari 40 za ardhi kwa kuwa walikubaliana shule hiyo iwe ya wananchi wa Kata ya Katoke.
Pia wananchi walikubaliana shule hiyo iitwe kwa jina la Ruth Msafiri baada ya kuwa yeye ndiye aliyeanzisha wazo la kuwa na shule ya wasichana katika kata hiyo. Vilevile Bi Ruth Msafiri alianza kuomba michango kwa niaba ya wananchi  ili kuanzisha ujenzi wa shule hiyo mwaka 2009.
Wananchi walichangia nguvu zao pia mfuko wa jimbo ulichangia Shilingi 3,000,000/=, Benki ya NMB ilichangia shilingi 5,000,000/= Wizara ya Maliasili na Utalii shilingi 6,000,000/=, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kikwete alichangia mabati 300 na ndipo ujenzi wa shule hiyo ulianza.
Baada ya uchaguzi Mkuu 2010 Ruth Msafiri hakubahatika kuchaguliwa tena kuliwakilisha jimbo la Muleba Kaskazini na ndipo mgogoro ulianza na akadai kuwa shule ni mali yake jambo ambalo wananchi hawakukubaliana naye na kuanza kulalamika na malalamiko hayo yalimfikia Mkuu wa Mkoa.
Tarehe 20/02/2012 Mkuu wa Mkoa alitembelea kijiji cha Katoke na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi na alisikiliza mgogoro huo kwa undani na akaagiza wananchi wapitie kwenye ngazi husika za kisheria kuanzia ngazi ya kijiji Balaza la Kata na Balaza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ili kulidhia kuwa shule hiyo ni mali ya wananchi.
Aidha baada ya hatua zote Mkuu wa Mkoa alizoagiza  kufuatwa nay eye kuridhia jana tarehe 17/9/2012 Mhe. Massawe aliikabidhi shule hiyo kwa wananchi ili kuendeleza ujenzi kwaajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2013.
Kutokana na furaha ya kukabidhiwa shule yao wananchi wakiongozwa na Mhe. Massawe na Mkuu wa Wilaya ya Muleba walianza kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwa kutoa fedha taslim, ahadi na zaidi ya shilingi 1,800,000/= zilichangwa pia mawe, mchanga, sementi, misumari na mbao vilihaidiwa kuchangiwa na wananchi hao.  
Shule hiyo ina jengo la utawala pia na vyumba viwili vilivyo pauliwa tayari, na msingi wa vyumba vitatu ambavyo havijakamilika. Wananchi walimhaidi Mkuu wa Mkoa kufikia mwezi Oktoba 2012 majengo hayo tayari yatakuwa yamekamilika kwa ajili ya Januari mwakani.
Imetolewa na:
Sylvester Raphael
Afisa Habari Mkoa,
Kagera @2012

No comments:

Post a Comment