Sunday, September 15, 2013

Elimisheni wananchi wafuge kisasa ili kuendeleza bonde la Mto Mara-Pinda

IMG_0054Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikata  utepe kuzindua  maonyesho ya siku ya Mara  yaliyofanyika Mugu wilayani Serengeti Septemba 15, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) IMG_0079Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akitazama magugu maji baada  ya kufungua maonesho ya siku ya Mara kwenye uwanja wa Sokoine Mjini Mugumu, Septemba 15, 2013.(Picha na OfisiyaWaziri Mkuu) IMG_0103Watoto kutoka Kenya wakitumbuiza katika Maadhimisho ya kilele cha siku ya Mara  yaliyofanyika  mjini Mugumu wilayani Serengeti Septemba 15, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) IMG_0144Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimkabidhi Nahodha wa Timu ya Soka ya Wnawake ya  Manispa ya Musoma, Mariam Ibrahim baada ya timu yake kunyakuwa ushindi wa kwanza  katika  shindano ya kuadhimisha siku ya Mara, katika kilele cha maadhimisho ya siku hiyo mjiniMugumu Septemba 15,2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
IMG_0183 2Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akimkabidhi kikombe na cheti, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti , Joh Ngwina (wapili kulia) baada yahalmashauri yake kunyakuwa ushindi wa kwanza wa mabanda ya maonyesho  ya siku ya Mara  yaliyofanyika Mugumu , Serengeti, Septemba 15, 2013. Kulia ni Naibu Waziri wa mailiasili na talii, Lazaro, Nyarandu na wapili kushoto ni Mkuuu wa Mkoa wa Mara, John Tuoa. (picha na Ofisi y Waziri Mkuu) IMG_0202Wasanii wa kikundi cha Bonchuku cha Serengeti wakitumbuiza katika sherehe za Siku ya Mara zilizofanyika Mugumu, Serengeti, Sewptemba 15, 2013. Mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) IMG_0259Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitazama moja ya silaha zilizokamatwa na askari wa Wanyamapori kutoka kwa majangili  wakati alipofungua maonyesho ya ya maadhimisho ya  siku ya Mara yaliyofanyika Mugumu wilayani Serengeti Septemba 15, 2013.  Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyarandu.(Picha na  Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………….
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema idadi kubwa ya mifugo katika bonde la mto Mara ni mojawapo ya changamoto zinazokabili utunzaji endelevu wa bonde na amewataka viongozi wa mkoa watoe elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafuge kisasa na kuepusha uharibifu wa mazingira.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumapili, Septemba 15, 2013) wakati akifunga maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day Celebrations) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sokoine mjini Mugumu, wilayani Serengeti mkoani Mara. Maadhimisho hayo yalianza Septemba 12, mwaka huu.
“Changamoto iliyopo ni kuainisha, matumizi bora ya ardhi iliyopo kwa kuzingatia uwiano baina ya ardhi na mifugo iliyopo. Tunawajibika kupima ardhi yetu kuanzia ngazi ya vijiji ili kuepusha athari zinazotokana na kuzidisha mifugo katika maeneo tuliyonayo ikiwemo eneo la Mto Mara.
“Kupima ardhi kutasaidia kuepusha migogoro inayoweza kutokea baina ya wakulima na wafugaji. Tutaendelea na mikakati ya kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili wafuge kisasa na kupunguza idadi ya mifugo ili kuepuka uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema bonde la mto Mara ni rasilmali kwa wakazi wa Mara na kwamba kama bonde hilo likitumiwa vizuri lina fursa kubwa ya kiuchumi na hasa kwenye kilimo cha umwagiliaji maji.
Alisema wastani wa pato la mwananchi wa Mara liko chini ikilinganishwa na mikoa jirani ya Mwanza, Manyara na Shinyanga na kwamba kilimo cha umwagiliaji kwa mazao kama mpunga na mbogamboga kitasaidia kuinua pato la wananchi wa mkoa huo.
“Ili kulitunza bonde hili ni lazima tuache kazi za kilimo umbali wa mita 60 kutoka kingo za mto huu kwa mujibu wa sheria. Tuache kuchoma misitu, tuache kukata miti hovyo, na kama mnataka kufanikiwa, nawashauri mfuge nyuki. Mkiwa na mizinga yenu kwenye misitu hamtachoma moto, ni lazima mtajizuia kuchoma moto ili msiwadhuru nyuki wenu,” alisema.
Alisema bonde la mto Mara ni fursa ya kisiasa, kijamii na kiuchumi hivyo wakazi wa bonde hilo wa pande zote mbili hawana budi kulitunza kwa faida ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Aliwaomba viongozi wa Tanzania na Kenya kushirikiana kulitunza bonde hilo na kuhakikisha kwamba Mto Mara unadumu.
“Mto Mara ni mto wenye historia, ni mto wa kumbukumbu, ni mto wa shughuli za kiuchumi na shughuli za maendeleo. Lakini zaidi ya yote, mto Mara unaunganisha jamii za pande zote mbili Kenya na Tanzania. Tutumie mto Mara kama alama (Symbol) ya chanzo cha umoja wetu, mshikamano, udugu na upendo kati ya wananchi wa Kenya na Tanzania na hata nchi zote za maziwa makubwa zinazotumia Ziwa Victoria,” alisema.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na Naibu Mawaziri wa Maji, Maliasili na Utalii na TAMISEMI pamoja na viongozi kadhaa kutoka Serikali ya Kenya. Pia wakuu wa mikoa ya Arusha, na Manyara,  na wakuu wa wilaya mbalimbali.

Ndani ya siku 10 Operesheni Kimbunga, yanasa wahamiaji haramu 6,809 na ng'ombe 2,809



Na Theonestina Juma,Bukoba
OPERESHENI kimbunga inayoendeshwa kwa kushirikisha vyombo vyote vya usalama katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita ya kuwarejesha wahamiaji haramu makwao na  kuwasaka majambazi wanaotumia silaha imewezesha kuwakamata wahamiaji haramu  6,809 na  watuhumiwa wa ujambazi 32.
Hayo yamebainishwa leo na Naibu Kamisheni wa Operesheni Kimbunga,Simon Sirro ambaye pia ni Mkuu wa Operesheni nchini wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba .
Kamanda Sirro alisema jumla ya wahamiaji haramu 6,809 waliokamatwa, Wanyarwanda ni 1,446, Warundi 4,229, Waganda 647, Wakongo 443, wasomali 42, Yemen mmoja na India pia mmoja na kwamba watu hao wamekamatwa katika mikoa yote mitatu.
Alisema kati ya hao wahamiaji haramu 2,367 wamerejeshwa makwao kwa maamuzi ya mahakama, 1,866 wamerudi nchini mwao kwa hiari ,396 wameachiwa huru huku wengine 2,170 wanaendelea kuhojiwa.

 Mabomu sita risasi 265 zilizokamatwa
Watuhumiwa wa ujambazi 32 wa unyang'anyo wa  wanaotumia silaha wamekamatwa ambapo wote wamebainika ni raia wa Tanzania baada ya kukimbiwa na wenzao kutoka nchi jirani wanaoshirikiana nao katika kufanya uhalifu ambapo Kagera wamekamatwa majambazi 20, Geita watano na Kigoma saba.
Kamanda Sirro alisema pamoja na majambazi kutoka nchi jirani kuondoka baada ya kupewa wiki mbili, lakini anaamini kuwa watarejea tena na hivyo  kuwataka kuwachana na kazi hiyo kwani hailipi.
“Biashara ya ujambazi hailipi, na tunaamini kuwa watarejea tu, kuendelea kutumia silaha zao, tunawambia  hata nasi tunatumia silaha tena ndiyo kalamu zetu za kila siku, hivyo waachane na kazi hiyo watafute kazi nyingine”alisema.
Halikadhalika risasi 265 za bunduki aina ya  SMG/SAR zimekamatwa  huku za Mark iv 20 zikipatikana na 82 zikiwa ni za magobole ambapo pia  imekamatwa mitambo miwili ya kutengeneza magobole pamoja na sare za jeshi la nchi jirani.
Kamanda Sirro alisema katika operesheni hiyo,wamefanikiwa kukamata mabomu sita ya kutupwa kwa mikono na silaha 22 za aina mbali mbali za moto  zilizokuwa zikitumika katika uhalifu.
Kuhusu mifungo, ng’ombe 2,809 nao wamekamatwa ambapo katika mkoa wa Kigoma wamekamatwa 559, Geita wamepatikana 95 na Kagera ni 2,155, jambo ambalo Kamanda Sirro ameoneshwa kusitikishwa kutokana na mapori yote yamejaa mazizi ya ng’ombe na hivyo kufanya hata wanyama waliomo katika mapori hayo kutoishi kwa amani.
Upande wa baadhi ya wahamiaji haramu kulalamika kuwa wananyanyaswa hasa na Maafisa Uhamiaji, Kamanda Sirro alisema kuwa hakuna mhamiaji haramu anayenyanyaswa kama baadhi yao wanavyodai, kwani zoezi hilo linazingatia sheria, kanuni, utaratibu zilizopo na haki za binadamu.

Operesheni Kimbunga yanasa majambazi 32,mabomu sita, bunduki 22 na risasi 265

 Sehemu za risasi , mabomu na bunduki zilizokamatwa katika operesheni kimbunga inayoendelea

 Mabomu sita risasi 265 zilizokamatwa
 Mitambo ya kutengenezea magabole yalikamatwa katika Mkoa wa Kagera



 Naibu Kamishna  wa Operesheni Kimbunga, Simon Sirro akiwaonesha waandishi wa habari hawako pichani sare za Jeshi zilizokamatwa katika Operesheni hiyo.
 



Hapa Kamanda Sirro akiwaonesha waandishi namna mitambo hiyo inavyotumika kutengezea bunduki aina za magobole ambazo zinauwezo wa kuuwa wanyama hata binadamu.

Saturday, September 14, 2013

Baadhi ya wanawake Rorya wadaiwa kuwatishia kuwaua waume zao wanaopinga uvuvi haramu



Na Theonestina  Juma, Rorya
KUNDI la wavuvi  wapatao 168 wakiwa na boti 21 wamewatia kiwewe wavuvi wadogo  wa mwalo wa Busanga, Kata ya Nyamtinga wilayani Rorya kwa kuhofia samaki kuisha, baada ya kuvamia hifadhi ya samaki ya Mang’ereng’ere katika Ziwa Victoria na kuanza kuvua samaki wakitumia, sumu na makokoro yaliyo chini ya milimita saba na urefu wa mita 120.
Kundi hilo la wavuvi  hao imeelezwa kuwa walifika katika mwalo wa Busanga mwishoni mwa mwezi wa Julai, ambapo makokoro hayo hunasa kila aina samaki ikiwemo na mayai hali inayowatia wasiwasi wavuvi wadogo kuisha kwa samaki mwalo huo katika eneo hilo.
Wavuvi hao wanadaiwa kutimuliwa kila mwalo walikofika katika ziwa Victoria upande wa mkoa wa Mara kutokana na aina ya zana wanazozitumia mfano kama mwalo wa kinesi na mto mara, kutokana na kuharibu mazalia ya samaki ambapo huvua hadi mayai na samaki wachanga.
Wavuvi hao wanadaiwa kuharibu hifadhi za samaki za mang’ereng’ere  kata ya Nyamtinga na Nyabiwe kata ya kirogo maeneo ambayo yametengwa na serikali kwa ajili ya mazalia ya samaki.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wavuvi kutoka katika mwao huo, walisema kundi hilo la wavuvi kutoka maeneo ya Kibui Kata ya Nyamunga kutokana kuendesha shughuli zao za uvuvi kwa zana zisizoruhusiwa, wamekuwa wakifanya shughuli hiyo bila kutumia taa za kama inavyopaswa na badala yake hutumia mwanga wa tochi tu.
“Hawa wavuvi  wanavua samaki wengi mno,kwa siku hupata  samaki kama madebe 30-50,wachanga, wakati na wakubwa, hali inayowafanya kusafirisha kwenda kuuza nchini Kenya na wengine huwapeleka Musoma na Tarime”alisema mvuvi mmoja.
Wavuvi hao walisema si kwamba wanawaonea gele, bali hofu  kwa baadhi ya walaji wa bidhaa hiyo kwani kuna wengine wanawavua kwa kutumia sumu na pia kutoweka kabisa kwa samaki  aina zote za  samaki katika hifadhi hiyo na eneo hilo kutokana na kuharibu mazalia ya samaki.
Halikadhalika walisema kundi hilo la wavuvi wanaojiita ‘By sisi ‘ wamekuwa wakiwatambia kuwa hakuna anayeweza kuwachukulia hatua wala kuwazuia kwa sababu wanafahamiana na viongozi wote na Busanga ndiko kwao.
Kutokana na tambo hizo, baadhi ya wanawake  wa kijiji hicho, ambao ni wachuuzi wa samaki, wametishia  kuwauwa baadhi ya wanaume kwa kuwawekea sumu kwenye chakula kwa  watakaosababisha wavuvi hao kutimuliwa kijijini hapo.
“Tunapokuambia taarifa hii, hatutaki hata majina yetu yafahamike, kwani hata baadhi ya wanawake wa kijiji hiki hatutaki wasikie tunazungumza kuhusu nini, kwa sababau  imefikia hatua ya kututishia maisha kama tutathubutu hawa watu wazuieliwe kuvua samaki kwa mfumo huu ama kufukuzwa katika eneo hili”alisema mmoja wao kwa sauti ya chini mno.
Walisema samaki wanaovua ni pamoja na Nembe, Gogogo, Mumi,Sangara, Furu, Ningu, Sato na dagaa, ambapo wao hakuna aina ya samaki wanaolenga.   
Hata hivyo, wavuvi hao walionesha kutikishwa na uongozi wa kijiji hicho kuitisha mkutano wa kijiji ghafla na kuondoa wasimamizi wa mwalo huo kwa madai kuwa wanakula fedha , ambapo hayo yote yalitokana na baada ya wavuvi hao kuwasili kijiji hapo,na walikuwa wakipingwa mfumo wa uvuvi wao na BMU.
Hata hivyo upande wa mwenyekiti wa kijiji cha Busanga, Bw. Paul  Festo  hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi kila alipopigiwa na gazeti hili.
Aidha  Afisa wa Doria katika ziwa Victoria mkoa wa Mara, Bw. Meela akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu , alisema malalamiko hayo ameshayapokea katika ofisi yake kutoka kwa raia mwema ambapo anayashughulikia.
“Taarifa hizo nimezipokea, nitakujulisha baada ya kuwasiliana na afisa uvuvi wa Wilaya ya Rorya, na baadaye nitakueleza ni hatua gani tulizozichukua”.
Hata hivyo, hadi mwandishi wa habari anatuma habari hizi, tayari Afisa doria, Bw. Meela ameshawasili wiayani Rorya katika mwalo huo, na kushudia hali halisi, huku akikosa ushirikiano kutoka kwa wavuvi wa kijiji hicho, ambapo kundi hilo linadaiwa kupata taarifa mapema ya ujio wa afisa huyo na kufanikiwa kuficha makokoro yao, ambapo wamebahatika kupata za wavuvi wa eneo hilo ambao nao wanaendesha uvuvi haramu.
Hali hiyo imethibitishwa na Bw. Meela ambapo  wakazi wa eneo hilo wanashindwa kutoa ushirikiano kwao, ambapo tayari watu hao walishaficha nyavu zao na ameahidi kuzitafuta hadi zipatikane.
Habari zaidi zinasema kuwa Afisa huyo ameshuhudia samaki waliovuliwa  hadi mayai na kundi hilo na wavuvi wanaotumia zana haramu ambapo amewataka kuondoka eneo hilo mara moja na kuacha kuendesha uvuvi  usiostahili katika eneo hilo.

Thursday, September 12, 2013

Hadi 2015 kilomita 18,000 za bara bara zitakuwa zimejengwa nchi nzima-Rais Kikwete

Na Theonestina Juma
“SERIKALI inatumia pesa nyingi katika ujenzi wa barabara, hili ni jambo ambalo wananchi wanapaswa kujua, asilimia kubwa ya fedha zinazotumika katika ujenzi wa barabara hizo zinatokana na kodi zenu,  hivyo mnapaswa kuzilinda na kuzitunza kwa nguvu zote ili zidumu”.
Hiyo ni kauli ambayo haikuisha kinywani mwa, Rais Jakaya Kikwete aliyehitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Kagera hivi karibuni ikiwa ni mara yake ya pili tangu awe Rais wa awamu ya nne, na ni mara ya kwanza tangu achaguliwe katika uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2010.
Hisia na msisitizo mkubwa anatoa katika Wiraza ya Ujenzi ambapo anasema kuwa barabara ni kitu muhimu katika maendeleo ya nchi hasa katika kipindi hiki ambapo shabaha yake kuu ni kuhakikisha kuwa mitandao za barabara kuu zote za mikoa na wilaya nchi nzima zinaunganishwa kwa kiwango cha lami, ili ziweze kuwa kichocheo ya uchumi nchini.
“Barabara ni kichocheo kikubwa cha uchumi hapa nchini, kwani ndiyo njia inayowawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili ya kuuza ikizingatiwa kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini, licha ya kuwa hazitakamilika 2015 bali atakayekuja atamalizia”anasema.
Rais Kikwete akiwa mkoani Kagera amezindua na kuweka jiwe la msingi miradi mitatu yalioko  chini ya Wizara ya Ujenzi.
Miradi hiyo ni pamoja na barabara ya Kagoma Lusahunga yenye urefu wa kilomita 154 , barabara ya Kyaka –Bugene pia  yenye urefu wa kilomita 56.1 na kivuko cha Mto Ruvuvu kilichoko katika wilaya ya Ngara mpakani mwa Tanzania na Rwanda.
Rais Kikwete anasema fedha zinazotolewa na serikali, zinatakiwa zitumike kikamilifu katika ujenzi wa barabara na pale ambapo hazitumiki ipasavyo huo, ni udhaifu na uzembe wa madiwani wakishirikiana na watendaji wa halmashauri husika.
Anasema pamoja na mikakati ya serikali kujenga barabara kwa kiwango cha lami, lakini wapo maadui wa  barabara ambao ni  wanadamu, kimazingira kama jua mvuja na kutokana na vitendo wanavyotenda ndani ya barabara hizo, ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa mchanga kwenye madaraja ya barabara, watu kumwaga mafuta aina ya oil barabarani na kubeba mizigo mizito kuzidi kipimo.
Anasema kutokana na vitendo hivyo, ni wajibu kila mmoja kulinda barabara ikiwa ni pamoja na serikali kulazimika kuweka mizani kila sehemu ya barabara kwa lengo la kupima uzito.
Anasema wakati wakianza kujenga barabara ya Lusahunga hadi Kagoma, barabara ya Bwanga –Biharamulo ilikuwa bado baadaye serikali iliacha kidogo ujenzi wa barabara ya Lusahunga –kagoma baada ya kumfukuza mkandarasi wa awali kutokana na kutokuwa na vifaa ambapo iliibuka maneno,  kuwa Waziri wa Ujenzi John Magufuli alikuwa anajipendelea, lakini si kweli bali ulikuwa ni mpango wa serikali.
“Serikali ilitaka usafiri wa haraka kwenda Uganda, si kweli kuwa Magufuli alikuwa anajipendelea na kuwanyima raha wakazi wa Biharamulo, hapana kwani kwa sasa mtu anaweza kutoka Rwanda anaingia Bwanga,  Kyamunyorwa, Muleba, Bukoba kisha Uganda”anasema.
Anasema serikali haitaki mtu anayetoka Muleba, Bukoba  kwenda Isaka Burundi alazimike kwenda Geita, apitie usagara ndipo arudi Isaka kweli ni mzunguko hivyo wanatakiwa kutoka Nyakanazi kwenda Kigoma.
Anasema kwa sasa  baadhi ya barabara ambazo ziko katika mipango ya serikali ni pamoja na barabara ya Kidangwe hadi kigoma, Manyoni kuelekea  Chaya.
Halidhalika kutoka Karua kuelekea Urambo kuingia darajani  ambapo barabara kutoka Kidagwe kwenda darajani wamekubaliana na nchi ya Kuwait  wataijenga wenyewe.
Anasema mipango ya kuunganisha nchi kwa kiwango cha lami kwa sasa kimebakiwa kwa kiwango kidogo, ambapo barabara ya Nyakanazi hadi Kigoma kilomita 50 tayari benki ya Afrika wamekubali kuijenga kwa kiwango cha lami.
Anasema kwa sasa wameanza kujenga barabara ya Kidangwe kwenda Manyoni na Uvinza hadi Mpanda ambayo nayo imo katika mikakati  mpana wa kupanua nchi kwani wanataka ipanuke.
Kuhusu usafiri kutokea Bukoba hadi mbeya, anasema wakazi wa Kagera wamekuwa wakisumbuka kwa kipindi kirefu na usafiri kati ya Mbeya na Bukoba, ambapo mtu hulazimika kupita Dodoma lakini kwa sasa wanataka  mtu akitokea Bukoba akifika Zega, asipite Singida na Dodoma na badala yake wapitie barabara za Tabora, Rungwa,  Makongo ,Matinga tinga, Chunya na kisha Mbeya.
Dkt. Kikwete anasema kwa sasa wameanza kujenga barabara ya Mbeya hadi Chunya mpaka Makongo na baadaye hapo watatoka Tabora kwenda Rungwa.Anasema kutoka Tabora kwenda Mpanda kupitia Makongo Benki ya Afrika imekubali kusaidia serikali ya Tanzania kuijenga.
Kutokana na hali hiyo nchi itakuwa imekamilika kwa mikakati ya kujenga barabara na kuiunganisha kwa kiwango cha lami.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za serikali kuunganisha barabara za mikoa yote kwa kiwango cha lami, Rais Kikwete anatoa onyo kali kuwa serikali haitawaruhusu baadhi ya watu wachache kuzuia utekelezaji wa miradi mbali mbali kama miundombinu hasa barabara kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo.
"Serikali itatumia mamlaka yake kupambana na baadhi ya watu
wanaokwamisha maendeleo ya wananchi, ujenzi wa barabara katika maeneo yao"anasema.
Halidhalika anatoa rai kwa makampuni ya Makandarasi nchini kuiga mfano wa kamapuni ya CHICCO ya nchini China inayojenga barabara ya Lusahunga –Kagoma kufanya kazi nzuri kwa kujisimamia na kujindesha wenyewe licha ya serikali kutokamilisha malipo yao kwa wakati.
Anasema hadi barabara hiyo inawekewa jiwe la msingi imebaki mita 500 tu kukamilika na kwamba Kampuni hiyo imejenga barabara hiyo kwa  muda mfupi ambapo hadi sasa bado wanaidai serikali sh.bilioni 40 ambazo watalipwa muda si mrefu.
Anasema pamoja na hali hiyo, serikali itaendelea kuingia gharama kuboresha na kuhudumia sekta ya usafiri kutokana na ukweli kuwa nchi yoyote ambayo watu wake hawawezi kusafiri, uchumi wake hauwezi kukua kwa kasi.
Rais Kikwete anasema maneno haya akiwa anazidua kivuko cha mto Ruvuvu ambapo kabla ya ujio wa kivuko hicho anabainisha kuwa wananchi wa eneo la Rusumo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 50 kwa kuzunguka, kupitia barabara kuu kwenda Ngara Mjini hivyo kupatikana kwa kwa kivuko hicho ni jambo la kujivunia.
Anasema  serikali itaboresha huduma ya usafiri katika sekta ya anga, majini na nchi kavu hii ni  ni lengo na shabaha kuu ya serikali hivyo kila huduma itakayohitajika mfano barabara na njia za reli watajenga ambapo vyote wanafanya ili kuboresha huduma ya usafiri.
Naye Mtendaji Mkuu wa Temesa, Mhandisi Marcelina Magesa akizugumzia juu ya kivuko hicho anasema kuwa matengenezo yake yamegharimu sh.bilioni 2.6 za Kitanzania na kuwa kimetengezwa nchini Uholanzi.
Anasema kivuko hicho kilisafirishwa vipande vipande hadi nchini kisha kuunganishwa hapo mto Ruvuvu.
Bi.Magesa anasema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba magari madogo manne, abiria 50 waliokaa na waliosimama 30 kwa wakati mmoja.
Kuhusu urefu wa kivuko hicho anasema kuwa ni mita 27.8 na upana ni mita 8.75 ambapo kimetengenezwa kwa vifaa maalum kwa ajili ya matumizi ya majini.
Halikadhalika  kivuko hicho kinaendana na ubora wa kimataifa ambapo ukaguzi wake umefanywa na Mamlaka wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) ambayo imewahakikishia kuwa kiko salama kwa usalama wa abira.Pia kivuko hicho kina vifaa vya kisasa vya kutosha kujiokolea kwa rika zote.
Kwa upande wa Waziri wa Ujezi, Dkt.Joh Magufuli anasema kivuko hicho kimewekewa waya maalum ambayo inazuia maji yakija kwa kasi hayawezi kukisomba na kukipeleka katika mto Kagera.
Anasema kwa nchi nzima hicho ni kivuko cha 25 ambavyo vimenunuliwa kwa fedha za serikali ambapo anabainisha matumizi yake kwa wanafunzi wote wa wilayani hiyo ya Ngara kuwa kwa wale wanaovaa sare huvushwa bure ambapo nauli za kuvushwa kwa mtu mzima ni sh.200, watoto  ni sh.50, mizigo chini ya kilo 50 ni sh. 200, pikipiki 500, baikeli 200 , ng’ombe 2,000 na gari yenye tani mbili hadi saba ni sh.7,500.
Dkt. Magufuli ambaye anasema kuwa hajawahi kumpongeza Mkandarasi wa ujenzi yeyote katika maisha yake lakini kulingana na utendaji kazi wa Kampuni ya CHICCO wanapaswa kupewa pongezi.
Pamoja na hatua hiyo, hata hivyo,  Dkt.Magufuli anakerwa na  baadhi ya wasimamizi washauri wa Makandarasi wa barabara ili wasifanye nchi ya Tanzania ni kama sehemu pa kuchotea hela.
Anasema kutokana na kukosekana kwa uadilifu, kwa baadhi ya Wasimamizi Washauri wa Makandarasi nchini wamekuwa wakishindwa kuwasimamia kikamilifu huku baadhi yao wakishirikiana na baadhi ya Makandarasi kufanya Tanzania kama sehemu pa kuchotea fedha na kuondoka.
"Mheshimiwa Rais, naomba kwa ruhusa yako tuzidi kuwafukuza na kuwa simamisha kazi baadhi ya wasimamizi washauri wanaoshindwa kuwasimamia kikamilifu makandarasi wa barabara na kufanya Tanzania kama sehemu pa kuchota hela na kuondoka"anasema.
Anasema katika ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene wasimamizi Washauri ya Kampuni ya Sai kutoka India na kwa kushirikiana na Kampuni ya Data walifukuzwa kazi Januari mwaka huu tayari wakiwa wameshalipwa sh.bilioni 1.9.
Anasema kwa sasa ujenzi wa barabara hiyo inasimamiwa na Wasimamizi washauri zaidi ya saba wote kutoka Wakala wa barabara makao makuomakuu ambapo ujenzi wake umeshafikia asilimia 36.
Hata hivyo anasema maradi huo wa barabara watu zaidi ya 400 tayari wameshalipwa fidia zao isipokuwa watu wane wakiongozwa na mtu mmoja anayemtaja kwa jina, Nehemia Kazimoto ambaye
amekataa kupokea zaidi ya sh.milioni 100 kwa madai kuwa ni kiasi
kidogo.
"Bwana Kazimoto, wewe ni Kazimoto, mimi ni 'moto kazi' nyumba zako zitabomolewa, na kama hutaki kuchuku fidia yako uende mahakamani, tunaheshimu uhuru wa mahakama lakini tutaendelea na kazi yetu"anasema kwa kumtumia salaamu.
 Anasema wananchi wanahitaji maendeleo hivyo tatizo la watu wachache haiwezi kukwamisha wananchi kupatiwa maendeleo.
Anasema  wakati Tanzania ikipata uhuru mwaka 1961 nchi nzima ilikuwa na barabara za lami kilomita 1,330 huku magari yakiwa ni 38,000 tu lakini baada ya miaka kadhaa barabara za lami zimeongezeka hadi kilomita 6,500 hadi 7,000.
Anabainisha kuwa Rais Kikwete ameweza kujega kilomita 11,154 za barabara za lami tagu ameigia madarakani ambapo huenda kilomita zikaongezeka hadi kufikia 18,000 kabla ya kumaliza muda wake.
Anasema kabla ya kujengwa barabara za kuunganisha baadhi ya mikoa hapa nchini, wakazi wa mkoa wa Kagera walilazimika kupitia Kamapala , Nairobi nchini Kenya na kisha kuingia mkoa wa Pwani na ndipo walifika Jijini Dar Es Salaam
Halidhalika kwa aliyekuwa akienda mjini Bukoba akitokea Wilaya ya Karagwe umbali wa kilomita 80 alilazimika kulala njiani siku mbili.
“Wananchi wa Kyaka Bugene, tangu nchi imeumbwa hawakuwahi kuona lami inafafanaje, hadi pale walipowekea lami nyepesi ya majaribio katika barabarakilomita 10 kutoka Kayanga- Omurushaka ndipo waliweza kuona aina ya lami inavyofafa”anasema huku wananchi wakiangua vicheko.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa barabara Taifa, Mhandisi Aaron Mfugale anasema barabara ya Kyaka Bugene inajengwa na Kampuni ya Chicco kwa gharama ya sh.bilioni 64.61 ambapo muda wa utekelezaji wake ni miezi 27 na hatua ya ujenzi wake imefikia asilimia 30.
Anasema  upembuzi yakinifu ya ujenzi wa barabara hiyo ilianza Novemba 2009 na kampuni mmoja ya Kitazania kwa sh. Milioni 386.6 kwa miezi sita kwa kuzingatia vigezo mbalimbali.
Anasema  jumla ya sh.bilioni 21 ameshalipwa mkandarasi na zaidi ya sh.bilioni 2.888 zimelipwa watu kama fidia kwa mujibu wa sheria, ambapo mradi wa barabara ya Lusahunga-Kagoma ujenzi wa barabara hiyo upembuzi yakinifu ulianza mwaka 1995.
Aidha 2003 alipatikana mkandarasi na kutimuliwa kazi kutokana na uwezo mdogo na baadaye wakapatikana Kampuni ya Chicco waliojenga barabara hiyo kwa miezi 36 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.
Jumla ya fedha zinazotumika katika mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ni sh.bilioni 191.
mwisho.
 
 

Wednesday, September 11, 2013

Operesheni Kimbunga Mnyarwanda ajitia kitanzi, baada ya kutakiwa kurejea kwao

Na Mwandishi Wetu, Kyerwa

 RAIA mmoja wa Rwanda amejinyonga kwa kamba chumbani kwake, baada ya mkewe raia wa Tanzania kugoma mali zao kuuzwa ili waweze kurejea nchini Rwanda.

Kutokana na tukio hilo la kujinyinga ambalo linalohusishwa na zoezi linaloendelea hivi sasa nchini la kuwasaka wahamiaji haramu na kuwarejesha makwao.
  Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu amejulikana kwa jina la Bw. Francis Mathias (75),mkazi wa kitongoji Kikukuru kata Kikukuru, tarafa Mabira wilayani Kyerwa mkoani Kagera.

Habari hizo zina sema kuwa kabla ya kuchukua hatua hiyo ya kujinyoga familia hiyo iliingia katika mafarakano, ambapo marehemu alipendekeza wauze mali zao ili kuweza kurejea nchini Rwanda jambo ambalo Mwanamke alikataa kwa adai kuwa yeye hawezi kwenda Rwanda.

  Mwenyekiti wa kitongoji cha Kikukuru,Bw. Joseph Leo, jana alilithibitishia blog kutokea kwa tukio hilo na kuwa alipata taarifa hizo kutoka kwa binti wa marehemu juzi saa 3:00 asubuhi.
  “Baada ya kupata hizo taarifa niliongozana na mgambo, tulipofika mlango wa chumba chake ulikuwa umefungwa kwa ndani, tukafanikiwa kuuvunja tukaingia ndani na kukuta amejitundika kwa kamba,” alisema Leo na kuongeza kuwa marehemu alikuwa mfugaji na mkulima.
  Alisema kuwa kabla ya kujiua, mzee huyo alichana fedha za Kitanzania zinazokadiriwa kufikia Shilingi milioni saba zikiwamo noti za Sh. 5,000 na za Sh. 10,000, ambazo zilikutwa ndani ya chumba chake.
  Bw.Leo alisema baada kushuhudia alipiga simu kwa Ofisa Mtendaji wa Kata Kikukuru ambaye alifika na kupiga ngoma na watu walikusanyika kushuhudia kilichotokea na baadaye kwenda kutoa taarifa  katika kituo cha Polisi.
  Alipotakiwa na blog kuthibitisha kama kweli mwananchi wake aliyejinyonga alikuwa raia wa Rwanda,Bw.Leo alithibitisha na kufafanua kuwa tayari alikwisha kumuorodhesha kwa lengo la kurejeshwa kwao katika opereshani iliyoanza Jumamosi ya kuwarejesha makwao wahamiaji haramu wanaoishi mkoani Kagera.
Aliongeza kuwa aliwahi kumhoji marehemu Bw.Mathias ambaye alimweleza kuwa alikuja Tanzania kutoka Rwanda tangu mwaka mwaka 1976.
  Naye Ofisa Tarafa ya Mabira, Bw.Nicolaus Rugemalira, alisema uchunguzi wa awali wa kimazingira umeonyesha kuwa kulikuwa na mgogoro wa familia baada ya marehemu kutaka wauze mali zao zote warudi Rwanda, lakini familia yake haikukubaliana naye kutokana na mkewe kuwa raia wa Tanzania.
  “Mke wake ni Mtanzania, inaonekana baada ya familia yake kukataa uamuzi wake wa kuuza mali zote ili waondoke, aliamua kuchukua uamuzi huo,” alisema Rugemalira.
  Akizungumzia tukio hilo, binti wa marehemu, Bi. Melania Francis, alithibitisha kuwapo ugomvi kati ya baba yake na mama yake hali iliyosababisha mama yao kuondoka bila kufahamika alikoelekea.
  Alisema siku ya tukio aliamka na kuwaandaa wadogo zake kwenda shuleni na baada ya hapo alikwenda shambani kuona kama vibarua wameanza kazi ya kulima, lakini aliporudi nyumbani alishangaa kuona mlango wa chumba cha baba yake bado umefungwa wakati haikuwa kawaida yake kulala hadi saa moja.
  Melania alisema alibisha hodi bila majibu, akajaribu kufungua ikashindikana na alipochungulia aliona fedha nyingi zimetapakaa ndipo alipokimbia kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa kitongoji.
  “Nafahamu baba alikuwa na uwezo wa kumiliki fedha hizo, lakini sikufahamu anazihifadhi wapi,” alisema binti huyo wa marehemu.
  Alisema wamezaliwa watoto watano katika familia hiyo na kwamba ndugu zake wawili walitoweka na kubakia watatu na kuongeza kuwa kuwa anatambua kuwa baba yake alikuwa raia wa Rwanda.

 Alipotakiwa kueleza kama anafahamu alikoelekea mama yake, binti huyo alidai kuwa hafahamu ingawa anafahamu kuwa ni mzaliwa wa Wilaya ya Ngara, mkoani Kagera.
  Kutokana na kutoweka kwa mama huyo pamoja na wanafamilia wengine, uongozi wa eneo hilo unaendelea na ufuatiliaji ili kujua wanafamilia wengine wamekwenda wapi.
  Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, akizungumza kwa njia ya simu jana, alisema kwa sasa yuko katika operesheni inayoendelea ya kuwasaka wahamiaji haramu na kuwa angefuatilia taarifa hizo baadaye baada ya kuwasiliana na watendaji walioko chini yake.


Sunday, September 8, 2013

Operesheni Kimbunga yaanza rasmi ya kuwarejesha wahamaji haramu makwao, ni agizo la Rais Kikwete



Na Theonestina Juma, KAGERA
OPERESHENI kimbunga ya kuwarejesha wahamiaji
haramu makwao katika Mikoa ya Geita, Kagera na Kigoma imeanza rasmi ambapo ndani ya siku mbili tu, wahamiaji hamu 1851 na ng'ombe 10763 wamekamatwa.
Hayo yamebainishwa jana (leo) na  Mkuu wa Operesheni nchini,Simon Sirro ambaye pia ni Mkuu Msaidizi wa operesheni kmbunga katika mkutano na Waandishi wa habari kuhusiana na operesheni ulioanza rasmi Septemba 6, mwaka huu kufuatia agizo la Rais
Jakaya Kikwete alilotoa akiwa ziarani Mkoani Kagera mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Kamanda Sirro alisema katika Operesheni hiyo iliopewa
jina la "Operesheni Kimbunga" kwa siku mbili tu, timu ya vyombo vya usalama wanaoshiki katika zoezi hilo, wamekamata wahamiaji haramu 1851, ng'ombe 1763, silaha za moto saba ikiwemo short gun moja pamoja
na vifaa mbali mbali vya jeshi ikiwemo na sare za JWTZ. 


 Kanal Fabian Massawe akieleza mbele ya waandishi wa habari kuanza kwa operesheni ya kuondoa wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume na sheria.
  Mkuu wa Mkoa Kagera Kanal Massawe akiwa na Mkuu wa operesheni nchini na Mkuu wa operesheno Kimbunga Kamanda Simon Sirro amewataka wananchi wote kutoa ushirikiano katika zoezi zima ambalo amesema halina mwisho mpaka hapo watakaporidhika.                             
                                                     baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi mkoa wa Kagera


 
Alisema katika mkoa wa  Kigoma wamekamatwa wahamiaji haramu 855, short gun moja, gobole moja na ng'ombe 200, Mkoa wa Geita wahamiaji haramu 246
wamepatikana, gobole tatu na ng'ombe 240, sare ya jeshi moja na kibuyu cha maji cha JWTZ moja.
Halikadhalika Mkoa wa Kagera Wahamiaji 750
wamekamatwa, short gun moja, gobole sita, ng'ombe 1,323, ambapo ng'ombe 200 walikamatwa ndani ya pori la akiba la Moyovosi Kigoma na wengine 200 wamekamatwa katika pori la akiba la Burigi mkoani Kagera.
Alisema ng'ombe 1,123 wamekamatwa wilaya za Karagwe na Kyerwa na 240 kutoka maeneo mbali mbali mkoani Geita.
Alisema miongoni hao wahamiaji haramu 750 waliokamatwa mkoani Kagera, 26 wamekatwa katika Manispaa ya Bukoba.
Kamanda Sirro alisema katika zoezi hilo, wahamiaji hao wanawapakia kwenye malori na kuwapeleka hadi mipakani wa Tanzania nan chi husika na kuwakabidhi kwa viongozi wan chi husika.
“Katika harakati za kutekeleza zoezi hili, suala la haki za binadamu tunazingatia sana, kwani wahamiaji haramu tunawaondoa kwa upole na utaratibu unaotakiwa”alisema
Alisema katika utekelezaji wa zoezi hilo, ametoa onyo kali kwa mtu yeyote ambaye watawarushia risasi maofisa wao, hawatakuwa na mchezo nao, tuko tayari kupambana na yeyote atakayejaribu kuwarushia risasi"alisema.
“Huu si wakati wa kuchezeana kwa kurushiwa risasi, kwani muda waliopewa kusalimisha silaha ziliisha kama yeye ni raia mwema muda huu hatakiwi kuwa na silaha yoyote kinyume cha sharia, kama  mtu anasilaha heri aitelekeze huko huko porini”alisisitiza.
Aidha aliwataka wananchi wenye haki wasihofu lolote waendelee na shughuli zao za maendeleo.
Kwa upande wa Mkuu wa mkoa wa  Kagera, Kanali Fabian Massawe amewaka vyombo vinavyoendesha operesheni kuwa makini katika zoezi hilo kwa kuzingatia haki za binadamu.
Alisema wanatakiwa kuhakikisha wahamiaji haramu hao wanaondoka na vitu vyao na wananchi wasikubali kuwahifadhia mali zao.
"Kuna taarifa kuwa kuna baadhi ya wahamiaji haramu, wanawapatia wananchi kuwahifadhia mali zao, tunataka waondoke navyo na kama wana wauzia iwe katika maandishi mtu yeyote atakayebainika kuhifadhi vifaa vya wahamiaji haramu watakamatwa na kushtakiwa kwa kuhujumu nchi"alisema.
Aidha Kanali Massawe alisema katika zoezi hilo
halitawakumba wale wahamiaji haramu wa kike waliolewa na Watanzania wanatakiwa kwenda idara ya uhamiaji ili kuweza kupewa hati maalum na baadaye kuhalalishiwa uraia wake.
"Katika utekelezaji wa zoezi hili kuna malalamiko kuwa wanawake ambao ni wahamiaji haramu wanarudishwa,
huku baadhi yao wakiwa na watoto watatu hadi sita, hatuko kwa ajili ya kutenganisha ndoa za watu, wale walioondoka bila kujua sharia wanatakiwa kurudi kama walivyoondoka"alisema.
Alisema lengo la serikali si kwa ajili ya kuachanisha familia za watu na wala hawatamfukuza mtu kwa vile amemwoa mhamiaji hamu katika utekelezaji wa agizo la Rais Kikwete.
Alisema kabla ya kuanza kwa zoezi hili jumla ya wahamiaji haramu 11,061 waliondoka  mkoani Kagera, silaha 65 zilisalimishwa SMG zikiwa tatu,Short gun 10 na magobore 52.
 Alisema pamoja na idadi hiyo kuondoka kwa  hiari  mkoa ulitazamia kuondoka kwa wahamiaji haramu 52,000 -53,000 hivyo idadi ya wahamiaji haramu bado ni kubwa.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa timu ya operesheni kwa kuwataja wahamiaji haramu
waliko ili sharia iweze kuchukua mkondo wake.

Juali 26, mwaka huu Rais Kikwete akiwa wilayani Biharamulo alisema operesheni hiyo ambayo itaendeshwa katika mikoa hiyo itakuwa ni ya aina yake ambayo haijahi kutokea katika nchi hii.