Tuesday, July 28, 2015

Mapadri watatu na mtawa mmoja wafariki dunia katika ajali mbaya Missenyi

Na Theonestina Juma, Bukoba

MAPADRI watatu na mtawa mmoja wa kanisa katoliki Jimbo la Rulenge, Wilayani Ngara wamefariki dunia papo hapo katika ajali ya barabarani wakiwahi Karagwe kwenye misa ya shukrani ya mwenzao aliyepata daraja hilo hivi karibuni.

Kwa mujibu wa moja wa mapadri waliokuwa katika msafara huo, Erasto Nakule ajali hiyo imetokea leo saa 2:00 asubuhi katika  barabara iendayo nchi jirani ya  Uganda katika eneo la Bugorora  wilayani Missenyi mkoani Kagera.

Alisema gari aiana ya land cruser  yenye namba ya usajili T.650 BY1 la Jimbo Katoliki la Rulenge lililokuwa likiendeshwa na Padri Florian Tuombe ambaye amefia katika hospitali ya mkoa Kagera liligongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Sabuni lenye namna ya usajili T.166 AGU.

Alisema basi la sabuni lilikuwa likitoka wilayani Karagwe kwenda Mwanza, ambapo landcruser lilikuwa likitokea Biharamulo kwenda Karagwe.

 Padri Nakule aliwataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na padri, Michael Mwelinde (70), Padri, Onesmo Buberwa (40), Mwafunzi wa aliyekuwa anasomea upadri, Kamugisha na sister  Magreth Kadebe (60).

Hata hivyo, habari zaidi zinzeleza kuwa mapadri hao walikuwa ni walimu wa seminari ya Katoke wilayani  Biharamulo na kwamba walikuwa wakienda kwenye misa ya shukrani ya padre Evisius Shumbusho  inayofanyika nyumbani kwao Karagwe.

Kwa upande wa kamanda wa polisi Mkoa Kagera, Augustine Ollomi alisema chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na dereva wa landcruser kuendesha bila kuchukua tahadhari ambapo alitaka kupita basi la Sabuni na kugongana uso kwa uso.

Kamanda Ollomi alisema katika ajali hiyo watu wanne wamefariki dunia na kwamba majina yao bado hayajajulikana akiwemo na mwanafunzi anayesomea upadri katika seminari ya Katoke.

Alisema watu 13 wamejeruhiwa ambapo miongoni mwao wanaume wako 10 na wanawake wako watatu na wamelazwa katika hospitali ya rufaa  ya Kagera.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment