Sunday, August 11, 2013

Diwani wa CCM anusurika kifo, baada ya kutekwa na majambazi, wateketeza gari kwa moto katika pori la Kimisi



Na Theonestina  Juma
DIWANI wa kata ya Chonyonyo [CCM] wilayani Karagwe, Bw.Arnold Rweshekerwa amenusurika kuuawa na kundi la majambazi waliomteka nyara katika eneo la Kyanyamisa kabla ya kuwatoroka  akiwa amewafungia ndani ya gari lake kati kati ya pori la Kimisi usiku.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana mjini hapa na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Phillip Kalangi, tukio hilo la aina yake limetokea Agosti 10 mwaka huu saa 2.00 katika eneo lenye kibao kinachoonesha sehemu ya hifadhi ya akiba katika pori la Kimisi kuelekea wilayani Ngara.
Hata hivyo, baada ya kunusurika kuuawa na majambazi hayo, wameteketekeza gari la diwani huyo kwa kitu kinachokisiwa kuwa ni bomu, ambapo diwani huyo alipoteza maisha takriba saa mbili baada ya kusikia taarifa ya gari lake kuteketezwa kwa moto.
Habari hizo zinaeleza kuwa, Diwani huyo alikuwa ameenda kijiji cha Kyanyamisa kumtembelea bibi yake mzaa mama, ambapo wakati akirudi nyumbani kwake kata ya Chonyonyo, alikutana na watu wawili njiani, wakiwa na piston ambapo walimtishia nayo  na kumtaka ageuze gari kurudi alikotoka.
Katika harakati za kugeuza gari hilo, huku watu hao wakiwa wamepanda ndani ya gari lake hilo ambalo halijajulikana aina  wala namba yake, hatua kama tano hivi alikutana  na watu wengine tena.
Alisema watu walikuwa na mifuko minne yaliojaa  bunduki, magazine na risasi, ambapo akiwa anawaendesha kwenye gari lake, watu hao walikuwa wakifanya kazi ya kuingiza risasi kweye magazine  walizokuwa nazo.
Hali kadhalika watu hao walipofika karib u na kibao hicho chenye maandishi ya hifadhi ya akiba walimwamuru diwani huyo kuzima taa ya gari lake na hivyo watu hao waliendelea na kazi kuingiza risasi hizo kwenye magazine kwa kutumia tochi walizokuwa nazo.
Katika maelezo hayo yanaeleza kuwa, wakiwa kati kati ya pori la kimisi majambazi hayo walimwamuru Diwani huyo kusimamisha gari lake, kwa muda ambapo muda huo aliweza kuwaangalia mawazo yao yalikokuwa  kwa wakati huo, alilazimika kufunga [Lock}  milango yote na kisha kuruka kwenye dirisha la dereva na kutokomea porini.
“Diwani aliwafungia wale majambazi ndani ya gari lake, na kurukia kwenye dirisha la dereva, na hivyo hawakuwa na namna ya kuondoka ndani ya gari na inasemekama hunda baada ya kutoka ndani ya gari wameliteketekeza kwa bomu”alisema mmoja wa chanzo .
Habari hizo zinasema kuwa, Diwani huyo alitembea zaidi ya kilomita mbili akirudi Karagwe, ambapo aliona pikipiki moja ikiwa na watu wawili wenye silaha wakitokea Kyanyamisa kuelekea Ngara ambapo alishindwa kuwasimamisha kwani alihofia huenda wakawa ni wenzao, kutokana na alipokuwa nao aliwasikia wakiwasiliana na watu wengine.
Hata hivyo, aliendelea kutembea ambapo  aliiona hiace moja ikitokea mji mdogo wa benako wilayani Ngara saa 3.30 usiku, ambapo aliwasimimamisha na kisha kumpakia,  na aliwaeleza kisa chote na watu hao kumuelezea juu ya kuona gari likitekea kwa moto kati kati ya pori.
Watu hao wanadaiwa kuwa Kiswahili chao ni kama cha wanaotoka nchi jirani, ambapo hadi hivi sasa, polisi wanaendelea a uchunguzi wao juu ya tukio hilo, kutokana na diwani huyo alikuwa peke yake kwenye gari hilo hivyo wanashindwa kumuulizia nani.
“tukio hilo lipo,  na gari limetekezwa kweli kati kati ya pori lakini suala la utekaji wa diwani huyo, inakuwa ngumu kuthibitishwa kwani wakati wa tukio hilo likitokea, alikuwa peke yake kwenye gari hilo,  na huenda kuna mambo mengine yaliojificha ”alisema kamanda  Kalangi.
Katika tukio, watu hao hawakuweza kumdhuru diwani huyo licha ya kumpora simu yake ya mkononi, sh.100,0000 na viatu vyake alivyokuwa amevaa kwa wakati huo.
Diwani huyo amelazwa katika hospitali  teule ye Nyakahanga baada ya kupoteza fahamu.
Hatua ya utekeaji wa diwani huyo imekuja saa kadhaa baada ya Agosti 10 ikiwa ndiyo siku ya mwisho ya agizo la, Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka majambazi na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kujisalimisha na kusalimisha silaha zao.
Halikadhalika  na wahamiaji haramu kuondoka nchini kabla ya operesheni kubwa kuendeshwa  katika mikoa mitatu ya Geita, Kagera na kigoma kwa kushirikisha majeshi yote ya usalama nchini.
Hadi juzi silaha 19 zimesalishwa katika wilaya za Karagwe, Ngara, Biharamulo na wahamiaji haramu 2000 wameondoka nchini kwa njia inayojulikana na kwa wale ambao wamepitia njia za vichochoroni idadi yao haijajulikana.
Tangu Rais kikwete atangaze kuendeshwa kwa operesheni hiyo, hali ya utekaji ulikuwa umetulia katika pori hilo ambapo magari ya abiria yalikuwa yakisafiri katika pori hilo hata saa 4. Usiku tofauti na hapo awali.
Mwisho.
   

Thursday, August 8, 2013

Ajali yaua watu saba Wilayani Ngara akiwemo na mtoto wa wiki moja



Na Theonestina Juma
 WATU saba wamefariki dunia papo hapo Wilayani Ngara, baada ya gari waliokuwa wamepanda kutoka Ngara kwenda Kahama mkoani Shinyanga kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebaba mchanga katika eneo la ziro ziro, Benako njia ya kwenda Kahama .
Akizungumza na gazeti hili  jana ( leo) jioni Mkuu wa wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu amesema ajali hiyo limetokea  jana saa 6.00 mchana katike eneo la Ziro Ziro Benako barabara kuu ya kutoka wilaya ya Biharamulo kwenda Rwanda.
Alisema katika ajali hiyo, kati ya watu hao saba waliopoteza maisha papo hapo, wanawake ni wanne na wanaume ni watatu akiwemo na mtoto mchanga anae kadiriwa kuwa na wiki moja ambapo jinsi yake bado haijatabuliwa.
Bw.Kanyasu alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva aliyekuwa akiendesha gari la abiria aina ya hiace lenye namba ya usajili T 527 CLA  ambaye alikuwa mwendo kasi ambapo hakuchukua tahadhari alipofika katika eneo hilo la kona.
Katika ajali hiyo, dereva na tingo wa hiace hiyo ni miongoni mwa abiria walipofariki dunia papo hapo.ambapo miili yao yamehifadhiwa katika hospitali ya Omurugwanza wakisubiri kutambuliwa na ndugu zao.
Alisema katika ajali hiyo watu 10 wamejeruhiwa vibaya ambapo  baadhi yao wamekimbizwa katika hospitali ya  Teule ya wilaya ya Omurugwanza huku wengine nao wakilazwa katika hospitali ya Nyamiaga wilayani humo.
Mkuu huyo amewataka madereva kuwa makini wakati wakiwa wamebeba abiria kwani wanakuwa wamebeba roho za watu hasa nyakati hizi za sikukuu.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka eneo la tukio zinadai kuwa hiace hiyo ilikuwa imebabi wahamiaji haramu ambapo hata hivyo kwa upande wa mkuu wa wilaya hiyo, amesema kuwa si kweli kwani ni abiria wa kawaida tena wa raia wa Tanzania.
Mwisho.

Friday, August 2, 2013

Makamu wa Rais Tz, Dkt.Gharib Bilal alivyomwakilisha Rais Kikwete Nairobi

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (katikati) akiwa na baadhi ya Viongozi wenzake kutoka nchi za Maziwa Makuu, wakati walipokuwa katika Mkutano wa Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu, alipoiwakilisha Tanzania katika majadiliano ya mkutano huo uliofanyika Jijini Nairobi, 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na mkewe Mama Asha Bilal, (wa pili kulia) Balozi wa Tanzania Nchini Kenya, Dk. Batrida Burian, na viongozi wengine wakati alipowasili Jijini Nairobi juzi Julai 30, 2013 kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu, uliofanyika Jiji humo jana Julai, 31, 2013. Makamu anaondoka leo Jijini Nairobi kurejea nchini baada ya kumalizika kwa majadiliano hayo. Picha na OMR  

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa nchi za Maziwa Makuu uliofanyika jijini Nairobi Kenya, jana Jumatano ya tarehe 31, 2013. Mkutano huu ulihudhuriwa na Mwenyeji wa Mkutano huo, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Katibu Mtendaji wa Kamisheni yas Nchi za Maziwa Makuu Prof.Ntumba Luaba, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, wawakilishi wan chi za DRC, Zambia, Afrika Kusini, Rwanda na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
 
Mkutano huo umepokea taarifa kutoka kwa Mawaziri wa Ulinzi kutoka katika nchi za Maziwa Makuu ambayo imepokelewa na kisha kujadiliwa. Pia ripoti kutoka kwa Kamati ya Kimataifa inayoshughulikia suala la Mazungumzo kati ya Serikali ya Kongo (DRC) na wapiganaji wa kikundi cha M23 kinachojihusisha na upingaji wa serikali ya DRC kikifanya machafuko katika Mashariki mwa Kongo (DRC) imepokelewa kujadiliwa na kisha kupitishwa mapendekezo ambayo nchi washiriki zimeyasaini.
 
Wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, nchi washirika walisisitiza kutaka kuona amani inapatikana katika nchi za Maziwa Makuu na hasa DRC, Afrika ya Kati na Sudan. Wawakilishi hao walielezea kusikitika kwao kutokana na machafuko ya amani katika nchi hizo na wakawataka viongozi mbalimbali wanaotajwa kuhusika na machafuko haya kutambua kuwa athari inayotokana na machafuko haya ni kubwa na inaathiri wananchi wengi.
 
Viongozi hao walisema, nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu zinahitaji utulivu na kwamba mgogoro wa uvunjaji amani katika Kongo DRC unaotokana na kuwepo kwa kikundi cha M23, lazima upewe tiba ya kudumu ili eneo hilo libakie tulivu na watu wake waweze kupata fursa ya utulivu utakjaowasaidia kushiriki katika kazi zao za kila siku.
 
Akifunga mkutano huo kwa niaba ya Mwenyekiti Yoweri Museveni, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema ni wakati sasa nchi za Maziwa Makuu kutambua na kuazimia kwa kauli moja kuwa amani inahitajika katika nchi zote za ukanda huu. Akifafanua zaidi Mheshimiwa Rais Kenyatta alisema wananchi wa ukanda huu wanataka ajira na sio mapigano. 
 
“Hata vijana wanaotumika katika mapigano, tukumbuke kuwa baada ya mapigano watakachohitaji ni ajira. Akina mama na watoto wanataka kuona maisha yao yanaboreshwa na sio vionginevyo. Kwa namna nilivyoona tukishiriki katika mkutano huu ni dhaihiri tumeonesha nia ya dhati ya kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa na amani. Tudumishe nia hii nzuri,” alisema Rais Kenyatta.
 
Makamu wa Rais na msafara wake wanarejea nyumbani leo Alhamisi Agosti Mosi, 2013 tayari kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.

Kumpinga Meya wa Bukoba ni kanuni za halmashauri-CCM BUKOBA



Na Theonestina Juma,Bukoba
CHAMA cha Mapinduzi [CCM] katika  Manispaa ya Bukoba kimesema mambo yanayotokea kwa sasa kati ya madiwani 15 wanaompinga Meya wa Manispaa hiyo, Dkt.Anatory Amani yanakwenda kulingana na kanuni za halmashauri  nchini.
Aidha Uongozi wa CCM mjini hapa,umesema wanakubaliana na maneno aliyoyaongea, Rais Jakaya Kikwete kuhusiana na migogoro iliopo kati ya Meya na Mbunge wa Jimbo la Bukoba mjini ambaye pia  Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ya kutaka wakae chini  na kumaliza tofauti zao.
Akizungumza na gazeti hili mjili hapa, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba, Bw. Yusuph Ngaiza alisema kwa sasa yale yote ambayo Rais Kikwete  aliyasema tayari wameanza kuyatekeleza, bila kufafanua ni mambo yapi ambayo wameanza kutayetekeleza hadi hivi sasa.
“CCM wilaya imeanza  kutekeleza yale yote ambayo Rais alituasa akiwa mkoani hapa, lakini yanayotokea kwa sasa ndani ya Manispaa ya Bukoba kati ya madiwani 15 ya kumpinga Meya yanakwenda kulingana na kanuni za halmashauri hivyo kauli kuwa ‘madiwani wa CCm wamgeuka Kikwete’ sio kweli”alisema
Alisema maneno aliyoyasema Rais Kikwete ni kwa ajili ya kujenga chama pamoja na manispaa ya Bukoba.
Katika mkutano wa hadhara wa Rais Kikwete katika uwanja wa Kaitaba alimtaka Mstahiki meya wa Mansipaa ya Bukoba , Dkt. Amani na Bw. Kagasheki kukaa chini na kumaliza tofauti zao kwani hakuna kitu kisichokuwa na mwisho.
Halikadhalika aliuagiza uongozi wa halmashauri ya Manispaa ya Bukoba kuhakikisha inawalipa watu wanaodai viwanja 800 bila masharti yoyote kwani tangu mwaka 2003 ni kipindi kirefu.
Pia alitaka  uongozi wa manispaa hiyo kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa soko kuu la kisasa, lakini kabla ya kuanza zoezi hilo watafute sehemu pa kuhamishia wafanyabiashara walioko ndani ya soko hilo kwani hapo ndiko wanakopata riziki yao.
Hata hivyo, katika uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa pamoja na maneno ya Rais Kikwete kwa  CCM mjini hapa, aliponyanyua miguu yake tu kesho yake jumanne wiki hii, madiwani wanne wa CCM waliwasilisha barua kwa mkurugenzi ya kutaka uitishwe baraza la madiwani kwa lengo la kutaka kupiga kura ya kutokuwa imani Meya wa manispaa hiyo.
Mwisho.

Thursday, August 1, 2013

Serikali Kagera yasitisha utoaji vibali kwa wageni, donge nono latangazwa kwa mwananchi atakayetoa taarifa ya anayemiliki silaha

Na Theonestina Juma,Bukoba
UONGOZI wa mkoa wa Kagera umesitisha utoaji wa vibali  kwa muda vya kuingia na kukaa nchini kuanzia leo  kupisha operation wa majambazi,wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria, ikiwa ni kutekeleza agizo ya Rais Jakaya Kikwete.
Hayo yamesemwa  jana {leo} na Mkuu wa mkoa Kagera kanali Fabian Massawe katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Bukoba.
Alisema vibali hivyo vinasitishwa kutolewa na idara ya uhamiaji hadi pale msako huo utakapoisha.
Kanali Massawe  alisema mbali na hiyo pia imetangaza donge nono kwa wananchi ambao watawapatia taarifa sahihi kwa wale ambao wanamiliki silaha kinyume cha sheria pamoja na wahamiaji haramu katika maeneo yao.
Kanali Massawe alisema “kwa mtu yeyote atakaye tupa taarifa sahihi juu ya mtu ambaye anamiliki silaha kinyume cha sheria tutampatia sh. 100,000”.
Alisema  watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wanatakiwa kuzisalimisha kwa viongozi wa kata, vitongoji wenyeviti wa vijiji, tarafa, katika vituo vya polisi na hata katika ofisi ya mkuu wa mkoa.
“ kwa sasa zimebakiwa takribani siku 10 msako huo kuanza, hivyo kwa yeyote asiyetaka kusalimisha sihala na hata yule mhamiaji haramu ambaye hataki kuondoka nchini kwa utaratibu asije akatulilia”alisema.
Alisema si kwamba Watanzania hawapendi wageni, lakini wanatakiwa kuingia nchini kwa kufuata utaratibu wanchi husika, na si kuja kwa kujificha bali wanatakiwa kuja kifua mbele kwa kufuata sheria zilizopo.
Alisema ulinzi wanchi ni wa kila mmoja na ndiyo maana wanasisitiza ulinzi shirikishi na hii ni kutokana na polisi waliopo ni wachache  na hivyo hawawezi kuachiwa wao peke yao.
Aidha alitoa tahadhari kwa wale wananchi wanaowahifadhi wahamiaji kuwa wakipatikana nao watafanywa kama wahamiaji haramu hao.
Hatua hiyo inakuja baada ya Rais Kikwete kufanya ziara ya siku sita mkoani hapa, na kusitiksihwa na maisha wanaoishi wakazi wa mkoa kagera ambao hawawezi kusafiri bila kusindikizwa na polisi wenye silaha.
Julai 26, mwaka huu Rais Kikwete akiwa wilayani Biharamulo katika moja ya ziara yake hiyo, alitangaza nchi kuendesha msako mkali wa kuwasaka majambazi, wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.
Katika msako huo unaotarajiwa kuanza siku 10 zijazo majambazi , wahamiaji haramu na wanaomiliki silaha watasakwa ndani ya nyumba zao, mapori na handaki walizochimba kuficha bunduki zao.
Alisema katika msako huo hakuna cha msalia mtume, kwani wahamiaji haramu wametakiwa kuondoka kwa  amani bila kusubiri msako huo  kwani hataki ugomvi na nchi jirani bali anataka watanzania wabaki waishi kwa amani na kwamba haiwezekani  Mtanzania akiwa kama mkimbizi ndani ya nchi yake.